Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo (Mb) amewataka Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo kufanya kazi kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu zinazotumika kusimamia taasisi hizo na sikuwa kikwazo katika kutoa huduma bora kwa wananchi.
Waziri Mkumbo aliyasema hayo alipokuwa akitoa mwelekeo wa utekelezaji wa majukumu ya Wizara katika kikao na Wakuu wa Taasisi hizo kilichofanyika tarehe 09/04/2021 katika ukumbi wa Chuo cha Biashara jijini Dodoma.
“Taasisi zote zilizochini ya Wizara ya Viwanda zinamchango mkubwa katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara hivyo nawasihi muendelee kufanya kazi kwa mujibu wa Sheria Kanuni na taratibu zinazosimamia taasisi zenu katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi na si kuwa kikwazo”
Aidha, Wakuu wa Taasisi waliohudhuria kikao hicho kutoka TBS, WMA, BRELA, TANTRADE, SIDO, NDC, EPZA, FCC, FCT, WRRB, TIRDO, CAMARTEC, TEMDO na CBE walipata fursa ya kutoa maoni na changamoto mbalimbali zinazozikabili taasisi hizo katika utekelezaji wa majukumu yake kwa Mhe.Waziri wa Viwanda na Biashara.
Waziri Mkumbo ameahidi kuendelea kupokea ushauri wa kitaalamu kutoka katika taasisi hizo pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zinazozikabili taasisi hizo katika utekelezaji wa majukumu yake ikiwemo upatikanaji Bodi zinazofanya kazi katika kila taasisi ili kurahisisha utoaji wa maamuzi sahihi na kwa wakati.
Naye Naibu Waziri akiongea na Wakuu wa Taasisi hizo, alisema kuwa mchango wa taasisi hizo ni muhimu na zinategemewa katika kuifanikisha Wizara kufikia malengo ya taifa katika ukuaji wa viwanda na biashara shindani na hivyo kukuza uchumi wa nchi
0 comments:
Post a Comment