Friday, 30 April 2021

PROF. KOMBA ATAKA TSC IONE FAHARI KUHUDUMIA WALIMU WENYE MAADILI

...
Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Prof. Willy Komba, akifunga mafunzo kwa Kamati za Wilaya za Mikoa ya Kanda ya Ziwa, zinazoshughulikia masuala ya Ajira na Nidhamu kwa Walimu, Aprili 29, 2021 jijini Mwanza.
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Mwl. Paulina Nkwama, akitoa hotuba ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, ambaye ni Mwenyekiti wa Tume hiyo, Prof. Willy Komba kufunga mafunzo kwa Kamati za Wilaya za Mikoa ya Kanda ya Ziwa, zinazoshughulikia masuala ya Ajira na Nidhamu kwa Walimu, Aprili 29, 2021 jijini Mwanza.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo kwa Kamati za Wilaya za Mikoa ya Kanda ya Ziwa, zinazoshughulikia masuala ya Ajira na Nidhamu kwa Walimu, wakimsikiliza Mgeni Rasmi ambaye ni Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Prof. Willy Komba (hayupo pichani), wakati akifunga mafunzo hayo, Aprili 29, 2021 jijini Mwanza.
Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Suzan Nussu kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI (kushoto) na Assela Luena kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa katika mafunzo kwa Kamati za Wilaya za Mikoa ya Kanda ya Ziwa, zinazoshughulikia masuala ya Ajira na Nidhamu kwa Walimu, jijini Mwanza, Aprili 29, 2021.

**********************

Na Veronica Simba – TSC

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) Profesa Willy Komba, ametoa hamasa kwa watendaji wote wa Tume hiyo kusimamia vema suala la maadili kwa walimu ili wajisikie fahari kuwahudumia.

Alitoa kauli hiyo mwishoni mwa juma wakati akifunga mafunzo ya wajumbe wa kamati za wilaya katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, zinazoshughulikia ajira na maadili kwa walimu, chini ya usimamizi wa TSC.

Akifafanua, Prof. Komba aliwataka washiriki wa mafunzo husika, wanaporejea katika vituo vyao vya kazi, kwenda kuwajibika kwa kuwakumbusha walimu maadili na miiko ya kazi yao.

Alisema kuwa, endapo Kamati hizo za Nidhamu zitafanikiwa kuwafikia walimu wote, TSC itafanikiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya walimu wanaolalamikiwa kukiuka maadili ya kazi yao.

“Sisi sote tuone fahari ya kuwahudumia walimu wenye maadili ambayo watayaambukiza kwa watoto wanaowafundisha na jamii kwa ujumla,” alisema.

Aidha, Mwenyekiti huyo wa TSC aliwasisitiza washiriki wa mafunzo kujenga utaratibu wa kujisomea sheria, kanuni, taratibu, miongozo na nyaraka za serikali kuhusu masuala mbalimbali wanayoyashughulikia ili kujiongezea ufahamu wake.

Vilevile, aliwataka wasisite kuomba ufafanuzi kutoka kwenye Ofisi au Mamlaka nyingine hususan katika masuala yenye changamoto ili kuepuka kukosea katika utendaji wao.

Awali, akitoa hotuba ya kumkaribisha Mgeni Rasmi kufunga mafunzo hayo, Katibu wa TSC, Mwl. Paulina Nkwama alieleza kuwa lengo lilikuwa ni kuwawezesha washiriki kufahamu na kutekeleza majukumu yao ya Tume kwa haki.

Mwl. Nkwama alizitaja mada zilizowasilishwa katika mafunzo hayo kuwa ni pamoja na Kusudi la kuanzishwa kwa Tume ya Utumishi wa Walimu, Muundo na Majukumu ya Tume pamoja na Majukumu ya Tume kuhusu masuala ya Ajira na Maendeleo ya Walimu.

Aliongeza kuwa, mada nyingine zilizowasilishwa ni kuhusu Maadili na Miiko ya Kazi ya Ualimu pamoja na Majukumu ya Mamlaka za Nidhamu na Rufaa kwa Walimu.

Mafunzo hayo ya siku mbili yalifanyika Aprili 28 na 29 mwaka huu jijini Mwanza na kuzishirikisha wilaya zote za Mikoa ya Kanda ya Ziwa ambayo ni Mwanza, Mara, Kagera, Simiyu na Shinyanga.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger