Bibi mmoja kutoka Machakos nchini Kenya ambaye alifariki dunia mwaka 2004 amezikwa miaka 17 baada ya kupumua pumzi yake ya mwisho akiwa na miaka 93.
Esther Nzakwa Kitovo aliaga dunia Agosti 31, 2004, na maiti yake imekuwa ikihifadhiwa katika Makafani ya Machakos kwa miaka 17 kwa sababu ya mzozo wa shamba ambao ulichelewesha mazishi yake.
Ripoti zinadai kuwa marehemu alikuwa mke wa kwanza wa mume wake ambaye alifariki 2000.
Alikuwa na wake wengine na kulingana na tamaduni ya Wakamba, mke wa kwanza anatakiwa kuzikwa kando ya mume wake.
Hata hivyo, mipango ya mazishi yake ilisitishwa mwaka 2004 baada ya mtoto wa kambo wa Kitovu kudai kuwa na amri ya Bodi ya Kudhibiti Ardhi inayothibitisha ndiye mmiliki halali wa shamba hilo.
Miaka 17 baadaye, hakuna jaji aliyeamua kuwa ajuza huyo mwenye miaka 93 ndiye mmiliki halali wa kipande hicho cha ardhi.
Siku ya Jumamosi, Aprili 24,2021 alizikwa nyumbani kwa mwanawe bila ya kesi hiyo kuamuliwa na korti.
Mazishi yake yalichukua muda wa saa moja kuafikiana na masharti ya COVID-19.
"Tunahisi afueni tunawashukuru waliosimama na sisi. Tumelia na kuomboleza.Huu ndio mwisho wa kipindi kirefu cha kutamausha. Lakini tuna furaha kuwa haya yameisha kwa amani," alisema mmoja wa familia hiyo.
CHANZO - TUKO NEWS
0 comments:
Post a Comment