Mfano wa nyaya za umeme
**
Na Yeremia Ngerangera - Namtumbo
Dereva wa pikipiki katika kijiji cha Mgombasi wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma Kaimu Kinokwite (28) amekufa kwa kukatwa shingo na waya wa umeme baada ya kunaswa na waya uliokuwa umekatisha barabara.
Kwa mujibu wa walioshuhudia tukio hilo akiwemo mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mgombasi Hance Mwailima alisema kuwa walimwona kijana huyo akirushwa kutoka katika pikipiki na kutupwa mbali baada ya kunaswa na waya huo.
Mwailima alidai marehemu alimbeba abiria wakitokea mgombasi madukani (kijiweni) wakielekea kijiji cha Mtumbatimaji katika harakati za kununua mahindi na walipofika katika kitongoji cha Dodoma jirani na shule ya msingi Mgombasi walipatwa na mkasa huo na mwenzake alikimbia .
Aidha mwailima alidai katika eneo hilo la tukio hapakuwa na alama yoyote iliyowekwa kuashiria kuwa kuna kazi ya kuweka nyaya za umeme katika nguzo za umeme hali iliyomfanya dereva wa bodaboda huyo kukumbana na mkasa akiwa katika mwendo kasi .
Kaimu mtendaji wa kijiji cha Mgombasi bwana Saidina Assedi Sandali alikiri kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa marehemu alifikishwa kituo cha afya Namtumbo licha ya kuwa alishafariki katika eneo la tukio .
Mtendaji wa kata ya Mgombasi bwana David Julius Kitalika pamoja na kukiri kutokea kwa kifo hicho aliwataka madereva wa pikipiki kuwa waangalifu muda wote wakiwa barabarani hasa katika kipindi hiki cha utengenezaji na uwekaji nyaya za umeme unaendelea katika vijiji vya kata ya mgombasi.
Marehemu karimu alizikwa katika makaburi ya minazini kata ya Rwinga katika mamlaka ya mji mdogo wa Namtumbo wanakoishi wazazi wake.
Via Michuzi blog
0 comments:
Post a Comment