Wakazi wanne wa Kijiji cha Isela Kata ya Samuye Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa Tuhuma ya Kumwozesha Mwanafunzi wa Darasa la Tano mwenye Umri wa miaka 12 (Jina limehifadhiwa) kwa mahari ya ng’ombe 8 pamoja na shilingi laki 6.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Septemba 20,2020 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga (ACP) Debora Magiligimba alisema kuwa Watuhumiwa hao walitenda kosa hilo Septemba 14 Mwaka huu katika kijiji hicho majira ya saa 12 jioni huku wakijua wazi kuwa kitendo hicho ni kinyume na sheria za nchi.
Alisema kuwa Jeshi la Polisi lilibaini kuwepo kwa harusi hiyo walilazimika kutuma kikosi kazi cha Maafisa wake wa Dawati la Jinsia na watoto kwa kushirikiana na Maafisa maendeleo ya Jamii walikwenda eneo la tukio na kukuta harusi ikiendelea nyumbani kwa bwana harusi aliyefahamika kwa jina la Khalifan Japhari (23).
“Tumefanikiwa kuwakamata wahusika wote wa tukio hilo ambao ni wazazi wa Pande zote walihusika na kuandaa harusi hiyo na tunaendelea kuwahoji na baadae tutawafikisha Mahakamani ili waweze kusomewa Mashitaka yanayowakabili,”alisema Magiligimba.
Kamanda Magiligimba aliwataja waliokamatwa katika tukio hilo ni pamoja na Japhari Khalifan (53)baba mzazi wa bwana harusi, Geni Bundala (52),Jumanne Shigimahi (52),Hawa Ramadani (37) ambao wote kwa pamoja waliaanda harusi ya mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya Msingi Samuye.
Alifafanua kuwa Uchunguzi wa awali umebaini kuwa mwanafunzi huyo aliozeshwa kwa taama ya Wazazi kupata Mali ambapo walipokea fedha Taslimu shilingi laki sita na Ng’ombe 8 kutoka upande wa waoaji na Jeshi hilo linaendelea kumtafuta bwana harusi Khalifan Japhari (23) ambaye ametokomea kusikojulikana.
“Nitoe wito kwa wazazi na walezi kuacha tabia ya kuwaozesha wanafunzi kwani vitendo hivyo ni vya kikatili na vinasababisha kukatisha ndoto zao katika elimu,tuungane kwa pamoja kutokomeza ndoa za utotoni mkoani Shinyanga kwa kuwafichua wazazi wenye tabia hizi,”alisema Magiligimba.
Mwanafunzi huyo alishakabidhiwa katika kituo cha kulelea watoto ambao ni wahanga wa ukatili na ndoa za Utotoni cha AGAPE AIDS cha Mjini Shinyanga ili kuendelea na Masomo.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment