Mwenyekiti mpya wa Chama Cha wafanyakazi wa Viwanda Biashara, Fedha Huduma na Ushauri TUICO mkoa wa Shinyanga Ebenezer Mende akiwashukuru wanachama kwa kumchagua na kuahidi kutatia changamoto zote zilizopo. Picha na Suzy Luhende.
Sehemu ya wanachama wa TUICO wakiwa ukumbini
Wanachama wa TUICO wakiwa katika picha ya pamoja.
CHAMA Cha Wafanyakazi wa Viwanda Biashara, Fedha Huduma na Ushauri (TUICO) mkoa wa Shinyanga kimefanya uchaguzi na kupata viongozi wapya ambao watafanya kazi kwa muda wa miaka mitano kwa ajili ya kushughulikia migogoro mbalimbali ya kikazi.
Akisimamia uchaguzi huo leo Ijumaa uliofanyika mjini Shinyanga, Katibu wa TUICO mkoa wa Shinyanga Fabian Samkumbi, amesema wamefanya uchaguzi huo kwa kufuata utaratibu na kanuni za Sheria baada ya viongozi waliokuwepo kumaliza muda wao wa miaka mitano.
"Nategemea kuona nyote mliochaguliwa kimkoa matawini na sehemu za kazi, wawakilishi mtakiongoza chama chetu kwa ufanisi mkubwa ili kukivusha katika kipindi kingine Cha miaka mitano 2020 mpaka 2025",amesema Samkumbi.
Samkumbi amebainisha kuwa viongozi waliomaliza muda wao walichaguliwa mwaka 2015 mpaka 2020, hivyo wamemaliza muda wao na kuchagua uongozi mwingine unaoongozwa na Mwenyekiti mpya Ebenezer Mende.
"Chama chetu hapa kwa kushirikiana na wanachama waliochaguliwa leo, tutahakikisha wanachama wetu wanazielewa vyema sheria za kazi na tutaendelea kuingiza wanachama wapya na kuimalisha matawi aliyopo", ameeleza Samkumbi.
Aidha Samkumbi amemtaka Mwenyekiti aliyechaguliwa na uongozi wake kusimamia ipasavyo wafanyakazi wote kwani bado kuna changamoto mbalimbali ambazo zinawakabili , kwani baadhi ya waajili wamekuwa na kawaida ya kuwazuia wafanyakazi wao kujiunga na chama hicho.
Mwenyekiti ambaye amemaliza muda wake Fue Mlindoko ambaye kura zake hazikutosha amemshauri Mwenyekiti aliyechaguliwa Ebenezer Mende kusimamia vizuri wafanyakazi ili waweze kutendewa haki katika sehemu za kazi zao.
Kwa upande wake Mwenyekiti aliyechaguliwa kukisimamia chama hicho Ebenezer Mende amesema changamoto zinazowahusu wafanyakazi ni nyingi hivyo atahakikisha anawatembelea wafanyakazi na kujua kero zao ili aweze kuzitatua kwa wakati.
"Nitatakiwa kuwa na mawasiliano ya karibu baina ya waajili na wafanyakazi ili kutatua changamoto mbali mbali kwa kufuata kanuni na kuhakikisha sitahiki za wafanyakazi zinapatikana kwa wakati na kuhakikisha amani inakuwepo katika sehemu ya kazi",amesema Mende.
"Natarajia kuleta muungano kwa waajili na wafanyakazi kwani mfanyakazi anatakiwa kufanya kazi kwa uadilifu ili aweze kulipwa sitahiki zake kwa wakati na mwajili amlipe mfanyakazi wake sitahiki zake kwa wakati unaotakiwa ili kuondoa migogoro makazini",amesema Ebeneza.
Baadhi ya wafanyakazi waliohudhuria mkutano huo wa uchaguzi akiwemo Neema Wilson na Husna Waziri wamesema uchaguzi umefanyika kwa amani na ulikuwa wa haki, hivyo wanawaamini viongozi waliochaguliwa ni wachapa kazi.
Katika uchaguzi huo waliojiteza kuwania nafasi ya Mwenyekiti walikuwa watatu kwa mara ya kwanza,ambao ni Rajabu Maulid ,Ebenezer Mende na Fue Mlindoko lakini kutokana na sheria na kanuni ya chama hicho mshindi hakufikisha idadi ya kura zinazotakiwa ambazo ni nusu ya wanachama waliopiga kura, hivyo uchaguzi ulirudiwa kwa watu wawili waliofuatana ambao ni Fue Mlindoko na Ebenezer Mende.
Fue Mlindoko na Ebenezer Mende walipigiwa kura Mlindoko alipata Kura 22 na Mende alipata kura 33 ambaye ndiye aliibuka kuwa mshindi na kuwa mwenyekiti wa TUICO mkoa wa Shinyanga.
Waliochaguliwa katika kamati tendaji sekta ya biashara ni Husna Waziri kutoka kutoka Shirika la umeme Tanesco Shinyanga, na Wolfgan Kalikawe kutoka Tanesco Maswa, sekta ya fedha walichaguliwa Fatuma Masha na Godfrey Hamba.
Katika sekta ya huduma na ushauri alichaguliwa Grace Kilenga kutoka Kahama na Twaiba Kweka kutoka Islamic Kahama, pia mjumbe wa mkutano mkuu Kanda ni Samson Sita, Sekta ya biashara ni Wolfgan Kalikawe, sekta ya fedha ni Godfley Hamba.
Pia sekta ya huduma na ushauri Kanda alichaguliwa Rajabu Maulid, na mkutano mkuu Taifa sekta ya viwanda alichaguliwa Kondo Diharibika kutoka Kahama, sekta ya biashara Maria Mazelengwe, sekta ya fedha Fatuma Masha, huduma na ushauri Twaiba Kweka na wawakilishi wa vijana ambao wataingia mkutano mkuu Taifa ni Tawfiq Omary na Salama Mhajin
0 comments:
Post a Comment