Friday, 18 September 2020

MWALIMU DELPHINA KUPITIA CUF AANIKA VIPAUMBELE VYAKE AKICHAGULIWA KUWA MBUNGE JIMBO LA SINGIDA KASKAZINI

...
Mgombea wa nafasi ya ubunge Jimbo la Singida Kaskazini Mkoani Singida Mwl Delphina Frank kupitia Chama cha Wananchi CUF akiomba kura kwa wananchi.
  Mgombea Ubunge akicheza za wananchi wa Kata ya Kinyagigi akicheza za wananchi wa Kata ya Kinyagigi
Wananchi wakimsikiliza mgombea Ubunge wa chama cha Wananchi CUF


Na Ismail Luhamba, Singida.
Mgombea wa nafasi ya ubunge Jimbo la Singida Kaskazini Mkoani Singida Mwl Delphina Frank kupitia Chama cha Wananchi CUF amesema akichaguliwa kuwa Mbunge atahakikisha anaimarisha sekta ya Afya, Elimu,Maji na Nishati katika Jimbo hilo.

Akizungumza na Wananchi wa Kata ya Kinyagigi kwenye mwendelezo wa kampeni zake za kunadi sera za chama hicho,mgombea Ubunge wa Jimbo la Singida Kaskazini Mwl Delphina Frank ametaja vipaumbele vinne ambavyo atavitekeleza endapo atachaguliwa kuwa Mbunge.

“Wananchi mnaonisikiliza hapa napenda kuwaambia kwamba nina mambo makubwa manne ya kuwafanyia nyinyi katika kipindi cha miaka 5, endapo mtanipa ridhaa ya kuwaongoza nitaanza na Sekta ya Afya, Elimu, Mifugo na Maji”, alisema Delphina.

Akizungumzia suala la Afya amesema atahakikisha kila Zahanati iliyojengwa na Serikali inakuwa na vifaa tofauti na sasa,kwani kwa sasa  kuna majengo tu huku kukiwa na ukosefu wa vifaa ndani ya hayo majengo.

“Ifikapo tarehe  28 Oktoba Jumatano mjitokeze kwa wingi kupiga kura ili kuhakikisha tunakiweka chama madarakani kutimiza ahadi tulizoziahidi”, alisema Delphina.

Delphina alisema kama CUF watapata ridhaa ya kuongoza katika Jimbo la Singida Kaskazini ndani ya miaka hiyo 5 watahakikisha wanasimamia vyema masuala yote yanayowahusu wafugaji na wakulima, kutunga na kutengeneza sera bora ili kuwa na ufugaji wenye tija na kilimo kwa ujumla.

“Hakika nawaambia wananchi wangu chagueni chama cha wananchi ili kiende kushirikiana na wataalamu wa kilimo, Maafisa mifugo tufuge na tulime kisasa ili tuondokane na umaskini tulionao,sasa tar 28 msifanye makosa kwa mgombea urais wetu Prof. Ibrahim Lipumba  na mimi”, alisema Delphina

Akifunga mkutano huo wa kampeni Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya Shabani Jumanne, aliwapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kusikiliza sera za mgombea Ubunge,na anaamini wamemuelewa na tar 28 watakwenda kufanya maamuzi ya haki kukipatia kura chama chicho.

"Nimefurahi sana tumefanya mkutano wetu kwa amani ila napenda kuwaambia tusifanye siasa za mazoea twendeni tukafanye mabadiliko sasa tumetawaliwa kwa muda mrefu sana bila maendeleo yeyote, hebu tazameni hatuna umeme, maji safi na salama, barabara mbovu chagueni Chama cha Wananchi  CUF kikaisimamie Serikali na kuhakikisha maendeleo haya yanapatikana katika Jimbo letu." alisema Jumanne.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger