Mgombea Ubunge jimbo la Solwa kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ahmed Salum akiwaomba wananchi wamchague tena kuwa Mbunge wa Jimbo la Solwa.
Na Victoria Robert - Michuzi blog
Mgombea Ubunge jimbo la Solwa kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ahmed Salum amewaomba wananchi wamchague tena 'wampe miaka mitano mingine' ili aendelee kuwaletea maendeleo huku akiwataka wachimbaji wadogo kuendelea kuchimba madini ya dhahabu kwa kujiamini bila kubughuziwa akiahidi kuwasogezea masoko madogo madogo katika kata ya Mwakitolyo.
Ahmed ameyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa kampeni za Uchaguzi CCM katika jimbo la Solwa ambapo alisema anazitambua changamoto zinazowakabili wananchi wa Solwa ikiwemo miundombinu ya barabara huku akidai kuwa baadhi ya barabara hizo zipo katika utekelezaji wa kiwango cha lami.
Salum aliwaomba wananchi wa Solwa wamchague kuwa Mbunge wao pamoja na Rais Magufuli na madiwani wa CCM kwani Ilani ya uchaguzi ya CCM inagusa maisha ya Watanzania na CCM imedhamiria kuwaletea maendeleo wananchi.
Akimnadi Mgombea ubunge wa jimbo hilo Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa aliwaomba wananchi kuchagua wagombea wa CCM ili waweze kuwaletea maendeleo yatakayowanufaisha wananchi.
Naye Naibu Waziri wa Ujenzi ambaye ni Mgombea Ubunge aliyepita bila kupigwa katika jimbo la Ushetu Elias Kwandikwa alisema serikali ya CCM inaendelea kuboresha miundombinu ya barabara pamoja na utoaji wa maeneo kwa wachimbaji wadogo wadogo katika eneo la Mwakitolyo hivyo ni muhimu kwa wachimbaji kuchangamkia fursa hiyo.
Kwa upande wake Mjumbe wa NEC, Gaspar Kileo ambaye pia ni Meneja kampeni wa mgombea ubunge jimbo la Shinyanga mjini. Patrobas Katambi aliwaomba kuchagua wagombea wa Chama Cha Mapinduzi ili waendelee kutekeleza ilani yao katika kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo la Solwa.
Akimuombea kura mgombea ubunge jimbo la Solwa,mgombea Ubunge wa viti maalumu mkoa wa Shinyanga Lucy Mayenga aliwaomba wanawake kumpigia kura Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Rais wa Tanzania ,Wabunge pamoja na madiwani wa CCM.
Mgombea Ubunge jimbo la Solwa kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ahmed Salum akiwa kwenye mkutano wa Uzinduzi wa Kampeni za CCM ambapo amewaomba wananchi wamchague tena kuwa Mbunge wa Jimbo la Solwa.
Kushoto ni Naibu Waziri wa Ujenzi ambaye ni Mgombea Ubunge aliyepita bila kupigwa katika jimbo la Ushetu Elias Kwandikwa akiwaombea kura wagombea wa CCM. Kulia ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa
Wananchi na wanachama wa CCM wakiwa kwenye uzinduzi wa kampeni za uchaguzi
Wananchi na wanachama wa CCM wakiwa kwenye uzinduzi wa kampeni za uchaguzi
0 comments:
Post a Comment