Saturday, 8 February 2020

Zaidi Ya Ekari Laki Mbili Zatengwa Kwa Ajili Ya Kuwezesha Shughuli Za Vijana – Naibu Waziri Mavunde

...
NA: MWANDISHI WETU
Serikali imetenga takribani ekari laki mbili katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwa ni mikakati wa kukuza na kuendeleza shughuli za maendeleo ya vijana.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde (Mb) Februari 7, 2020 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Grace Tendega aliyetaka kufahamu juu ya utekelezaji wa Serikali katika kuendeleza shughuli za vijana.

Naibu Waziri Mavunde alieleza kuwa Serikali imetenga maeneo ya shughuli za uzalishaji mali kwa lengo la kuhamasisha vijana waweze kushiriki katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo na itakayo wanufaisha kiuchumi.

“Serikali itaendelea kuzihamasisha Halmashauri zote nchini kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya shughuli za Vijana ikiwemo kilimo, viwanda na ufugaji ili kuwapa vijana fursa ya kuyatumia maeneo hayo katika shughuli zitakazowaletea maendeleo,” alisema Mavunde.

Wakati huo huo, Mhe. Mavunde alitoa ufafanuzi kwa Mbunge wa Iringa Mjini Mhe. Simon Msigwa (Mb) ambaye aliuliza kuhusu Mpango wa Serikali katika kutoa mafunzo kwa vijana ambao wamehitimu ili waweze kukidhi soko la ajira?

Alieleza kuwa Serikali Kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inatekeleza Programu ya Kukuza Ujuzi nchini ambayo inalenga kuimarisha nguvukazi inapata ujuzi unaotakiwa katika soko la ajira.

Akifafanua baadhi ya Programu ambazo zinatekelezwa ikiwa ni pamoja na Mafunzo ya Kurasimisha Ujuzi uliopatikana nje ya Mfumo usio rasmi, Mafunzo ya Uanagenzi ambayo yanatolewa kwa njia ya ufundi wa fani mbalimbali na Mafunzo ya Kilimo cha Kisasa kwa Teknolojia ya Kitalu Nyumba “Greenhouse”, Mafunzo ya Vitendo Mahali pa Kazi kwa wahitimu n.k.

Aidha alielezea suala la ukosefu wa ajira kwa vijana waliohitimu katika elimu ya juu kwa kigezo cha kutokuwa na uzoefu, “Jitihada za Serikali imekuwa ikiwapeleka vijana hao katika makampuni na viwanda mbalimbali ambapo wanapata mafunzo kwa vitendo kwa muda wa miezi 6 hadi 12 na baada ya hapo  wanapatiwa cheti cha Utambuzi “Certificate of Recognition”, cheti hiko kinawasaidia vijana hao kuwa wanauzoefu wa kazi Fulani,” alisema Mavunde.

Aliongeza kuwa Serikali imekuwa ikiwafadhili vijana kwa kuwapatia mafunzo ya Ufundi stadi katika Vyuo vya Veta, Don Bosco na Vyuo shirikishi ili kuwawezesha vijana wanapata ujuzi unaostahili katika soko la ajira.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger