Wazalishaji wa bidhaa mbalimbali mkoani Singida wametakiwa kutambua kuwa suala la viwango ni la kisheria hivyo ni lazima kuthibitisha ubora wa bidhaa ili kumlinda mlaji na kupata uhakika wa soko la bidhaa wanazozizalisha.
Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Dkt Rehema Nchimbi alipokuwa akifungua mafunzo ya wazalishaji wa bidhaa za vyakula yakiwemo mafuta ya alizeti na wauzaji wa vipodozi na vyakula yaliyofanyika katika ukumbi wa VETA mkoani Singida.
Dkt. Nchimbi alisema suala la ubora wa bidhaa linapaswa kuzingatiwa katika mnyororo wote wa uzalishaji ili mlaji awe salama na kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na kutozingatia viwango.
“Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ndiyo hakikisho la wazalishaji na fursa zinazotengenezwa zitakuwa dhahiri iwapo masuala ya viwango yatazingatiwa, vilevile TBS ni daraja kati ya mzalishaji na soko, hivyo mzalishaji ni lazima kufuata utaratibu,” alisisitiza Dkt. Nchimbi.
Alisema maisha ya binadamu ni chakula hivyo ni muhimu kuzingatia usalama wake, kwani bidhaa hafifu zinagharimu afya ya walaji na kwamba magonjwa mengi yanatokana na jinsi tunavyoandaa chakula na tunavyokula, hivyo wazalishaji wanapaswa kuwa waaminifu katika kuzalisha bidhaa yoyote.
Dkt. Nchimbi alisema TBS siyo adui wazalishaji hawapaswi kuichukia na wajenge dhana kuwa TBS ni usama hivyo wazalishaji wa Singida wahakikishe kuwa wanazalisha bidhaa bora wakati wote ili kudhidhirisha kauli kwamba Singida ni njema wakati wote.
Akizungumzia kwa upande wa TBS, Dkt. Nchimbi alisema Shirika linapaswa kuangalia namna ya kuongea na wajasiriamali ili kuhakikisha kuwa yale wanayowafundisha wanaelewa kikamilifu. Mafunzo haya yawe na kipimo ili kujua kama yameeleweka vizuri na kwamba watakaopokea mafunzo ndiyo watakaowapima.
Kwa upande wake Meneja wa Mafunzo na Utafiti kutoka TBS Bw. Hamisi Sudi alisema Shirika litaendelea kutoa mafunzo kwa wajasiriamali ili kuhakikisha kuwa wanazalisha bidhaa kwa kuzingatia viwango.
Alisema Shirika linatambua kuwa wajasiriamali wana mchango mkubwa katika kukuza pato la taifa na kutengeneza ajira kwa wananchi walio wengi hivyo Shirika lina mchakato endelevu wa kutoa elimu kwa jamii hasa wajasiriamali kwakuwa ni mojawapo ya majukumu yake ya kila siku.
Shirika likiwa mkoani Singida limetoa mafunzo kwa wajasiriamali 221 Katika wilaya za Iramba, Singida na Manyoni, ambayo pia yamewashirikisha watendaji wa Halmashauri wakiwemo maafisa Biashara, Maendeleo ya Jamii na Afya pamoja na Maafisa kutoka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO).
Pia Shirika linatarajia kutoa mafunzo katika wilaya za Kondoa, Kongwa na ikiwa ni muendelezo wa mafunzo katika Kanda ya Kati.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment