Thursday, 20 February 2020

UKEKETAJI BADO TISHIO…WAZAZI LINDENI WATOTO BILA UBAGUZI

...
Mabinti wakiwa  kwenye maandamano wakati wa kufunga kambi okozi ya ATFGM Masanga Januari 3,2019 .Picha zote na Frankius Cleophace.
Mabinti wakiwa kwenye mstari kwa ajili ya kuanza maandamano katika  kufunga kambi okozi ya ATFGM Masanga  Januari  3,2019.
Baadhi ya mabinti wakiwa wamekaa wakati wa kufunga kambi okozi ya ATFGM Masanga Januari 3, 2019

Na Frankius Cleophace Mara.
Watoto ni tunu ya leo na kesho bila kujali jinsia zao ukizingatia kwamba Wazazi wote wawili wana jukumu la malezi bora kwa mtoto hasa kuanzia miaka 0-9 na kuendelea.


Pia watoto wote wana haki ya kucheza, kupata elimu,mavazi pamoja na malezi bora, lakini baadhi ya wazazi wameacha hilo jukumu au baadhi yao wameachia jukumu hilo mzazi mmoja wapo, sasa imefika hatua wazazi wajitambue na kuthamini watoto wote.

Katika jamii tofauti hapa nchini, suala la mila na desturi limekuwa changamoto hususani pale mila kandamizi zinapoendelea kushamiri na kuumiza watoto wadogo ambao hawajui kinachoendelea katika dunia ya sasa, kwa maana hiyo naweza kusema wazazi hawana budi kubeba dhambi za watoto hao.

ATFGM Masanga ni shirika lisilokuwa la kiserikali lililopo wilayani Tarime Mkoani Mara ambalo linapinga  ukatili wa kijinsia ili kuhakikisha wanalinda mtoto, ili aweze kukua katika malezi bora bila kubaguliwa kwa aina yeyote au kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia, ukiwemo ubakaji, vipigo, kuchomwa moto pamoja na suala la Ukeketaji.

Sister Stella Mgaya ni Mkurugenzi wa Shirika la ATFGM Masanga anasema kuwa shirika hilo limekuwa likipokea watoto wa umri tofauti ambapo baadhi yao hukimbia suala la ukeketaji lakini baadhi yao huja kwa lengo la kupatiwa elimu ya kupinga ukatili  lakini ukeketaji unapoanza mapema baadhi yao hukimbia mapema kabla ya shule kufungwa na wengine kukosa haki zao za msingi za kupatiwa elimu ikiwa ni pamoja na mitihani ya kufunga mihula kushindwa kuifanya.

Mkurugenzi anataja makundi matatu ambayo mara nyingi hupokelewa kambini hapo kipindi cha  mwezi Desemba pale ukeketaji unapokuwepo kwa mwaka mara nyingi unaogawanyika kwa mbili.

Sister Stella anasema kuwa kundi la kwanza ni lile linaloletwa na wazazi wote wawili ambao wanapinga ukeketaji lakini jamii inakuwa inataka kuwakeketa, kundi la pili ni mzazi mmoja wapo kati ya baba au mama anapinga ukeketaji sasa mzazi moja wapo huleta mtoto huyo kambini ili asikeketwe lakini kundi la tatu ni lile ambalo unakuta wazazi wote na jamii kwa ujumla wanataka kukeketa binti huyo hivyo huchukua hatua za kukimbia ili asikeketwe.

Stella anaongeza kuwa kambi la mwaka 2019 limekuwa la tofauti kwa sababu suala la ukeketaji mpaka sasa mwezi wa pili 2020 linaendelea jambo ambalo linawashangaza sana lakini baadhi ya watoto ambao wamerejeshwa nyumbani kwao baadhi yao wanakatamatwa kwa nguvu na kukeketwa.

“Mwezi wa pili mpaka sasa 2020 ukeketaji bado unaendelea tunao watoto kambini hapa 13 tayari wamekeketwa baada ya kurudi nyumbani hivyo sasa kambi linazidi kuongezeka. Watoto zaidi ya 100  wapo kambini jambo ambalo ni tofauti na miaka mingin, pia kuna watoto wengine ambao wamekataliwa na wazazi wao kwa sababu walikimbia ukeketaji bila kushirikisha wazazi au jamii” ,anaeleza Sister Stella.

Mkurugenzi huyo anasisitiza kuwa licha ya watoto kuwa kambani hapo wazazi pamoja na jamii imekuwa ikiwavizia  kwa ajili ya kuwachukua kwa nguvu ili kuwakeketa na wakati mwingine  wanawavizia njiani wakitoka shuleni ambapo wameamua watoto wanaotoka eneo la kambi ilipo Masanga kupelekwa shule za serikali zenye bweni na wengine kwenye shule ya msingi Masanga na Goronga Sekondari lengo ni kuendelea kupata elimu kwani wengi wao ni wanafunzi wa shule za msingi na sekondari  na ambao hawasoni wanafanyiwa utaratibu wa kupelekwa vyuo vya ufundi.

“Mfano tumepeleka watoto 26 shule ya sekondari Inchugu ambayo ni ya bweni na watoto 08 shule ya sekondari Bung’eng’e na watoto takribani 60 shule ya msingi Masanga kwa sababu jamii inawavizia njiani kwa ajili ya kuwarejesha nyumbani ili kuwakeketa na hivi karibuni  mwanafunzi mmoja aliokolewa na wanafunzi wenzake baada ya mzazi kumkamata kwa nguvu kwa lengo la kumrejesha nyumbani ili kukeketwa”, amesema Mkurugenzi.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi anaeleza kuwa kwa sasa kituo hicho kinakabiliwa na changamoto ya upungufu wa fedha, chakula pamoja na mavazi kwa sababu wafadhili wao huleta fedha kulingana na msimu ambapo msimu uliopita watoto zaidi ya 500 walikuwa kambini huku baadhi wakitoka nchi jirani ya Kenya hivyo kambi humalizika mwezi wa kwanza ili watoto warejee nyumbani kwao kwa ajili ya kuendelea na masomo lakini mwaka huu imekuwa tofauti bado watoto zaidi ya 100 wapo kambini hapo na wengine wanazidi kurejea kutokana na ukeketaji kuendelea.

“Tunaanza kambi okozi mwezi wa kumi na mbili na kambi hiyo kuisha mwezi wa kwanza hivyo mfadhili anatoa fedha kwa ajili ya miezi hiyo ya watoto wanapokuwa kambini sasa  mwaka huu imekuwa tofauti ukeketaji unatajwa kuendelea mpaka mwezi wa sita kuliko miaka yote jambo ambalo linatushangaza na watoto wanarudi tena kwa mara ya pili kwa kuogopa kukeketwa kwani baadhi tayari wamekeketwa”, amesema mkurugenzi.

Ashura Ayoub ni Afisa Ustawi wa Jamii katika shirika hilo amesema kuwa  kambi hiyo ilifungwa tarehe tatu mwezi Januari 2019  na kuanza kurudisha watoto nyumbani kwao lakini changamoto wengi wameenda nyumbani lakini mazingira yamekuwa siyo rafiki ambapo mpaka sasa kambini hapo wapo watoto 119 wasichana na Mvulama mmoja jumla kufanya watoto 120 ambao baadhi wamerudi na wengine wamekataliwa na wazazi wao kwa sababu ya kukataa kukeketwa.

“Idadi inazidi kuongezeka kila kukicha kutokana na ukeketaji kuendelea, tulidhani watoto wote baada ya kambi tulijua watakuwa salama lakini bado wanafanyiwa ukatili jambo ambalo sisi kama shirika hatutakubali, lazima tulinde watoto hawa”, amesema Ashura.

Dora Luhimbo ambaye ni Mwanasheria wa kituo hicho anasema kuwa katika kambi hiyo wamekuwa kipokea watoto kuanzia miaka 04,05 hadi 07 na kuendelea ambapo wengi huanzia miaka saba lakini hawa wadogo mara nyingi wanakuja na dada zao pale wanapokimbia ukeketaji.

“Hawa wadogo mara nyingi wanakuja na dada zao ambao unakuta wamekimbia kukeketwa lakini sheria ya mtoto ya mwaka 2009 hairuhusu suala la Ukeketaji wala mtoto yeyote kufanyiwa Ukatili wa aina yeyote, sasa lazima sheria zifuatwe ikiwa na kutoa adhabu kali kwa wale wanaobainika kutenda vitendo hivyo”, amesema Dora.

Kwa kuliona hilo kama  watoto wadogo ambao wanapaswa kupata malezi ya wazazi lakini wanahangaika na kukimbia jambo ambalo linawaongezea ukatili, sasa ifike hatua wazazi pamoja na jamii kwa ujumla kuondokana na ukatili ili watoto wasiishi kama watumwa katika  nchi yao.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara Adam Malima kipindi akiongea na Mkurugenzi wa shirika hilo kuhusu nini kifanyike kwa ajili ya kusaidia watoto hao ambao mpaka sasa wapo kambini hususani suala la mavazi na chakula, Malima amesema kuwa alipokutana na wazee wa mila katika  eneo la Nyamwaga walikubaliana kuondokana na ukeketaji sasa jambo hilo linazidi kusikitisha serikali ya mkoa wa Mara.

“Tulikutana na wazee wa mila tukaongea mengi na kukubaliana kuacha ukeketaji kwa mtoto  wa kike na  kwa wavulana kufanya tohara salama lakini cha kushangaza wamekiuka sisi kama serikali hatutachoka kushughulikia suala hili”, amesema Malima.

Malima anasema jambo hilo la ukeketaji linazidi kufedheesha mkoa kwa sababu ya mila na desturi ambazo zinatesa watoto wadogo kuanzia miaka  mitatu watoto wanakimbia majumbani badala ya kukaa na wazazi wao ili kupata malezi bora.

“Nilishangaa kuona binti mmoja alikimbia ukeketaji huku mgongoni akiwa amebeba mdogo wake wa miaka minne wakati mtoto huyo bado anahitaji malezi ya wazazi, sasa kwanini wazazi hatuonei huruma watoto wetu ifike hatua jamani tubadike”, amesema Mkuu wa Mkoa.

Vile vile Mkuu wa Mkoa  aliahidi kuongea na wadau mbalimbali kwa ajili ya kuchangia chochote ili kukipatia kituo hicho walau chakula, Mavazi  ili kusaidia wahanga hao.

“Nimezungumza na Barrick, Watu wa TANAPA, Gachuma na wadau wengine ili waweze kusaidia chochote  wadau ambao wako nje ya Mara wajitokeze kusaidia siyo kuleta fedha mwenye, mahindi, mchele magodoro tutapokea kupitia timu ya katibu tawala wa mkoa wa Mara” amesema Malima.

Mmoja wa watoto ambao jina lake limehifadhiwa kutoka kijiji cha Kenyamsabi alisema kuwa alichukuliwa vizuri kutoka kambini hapo lakini alipofika nyumbani alikamatwa na kukeketwa na kisha kutelekezwa vichakani kwa siku nzima na baadaye kuokolewa na Shirika la ATFGM Masanga.

“Mimi sina baba wala mama, nilichukuliwa vizuri kutoka kambini hapa lakini ilipofika usiku walitokea mlango wa nyuma kunipeleka kukeketwa lakini waliposikia watu wa Masanga wanakuja nyumbani walinipeleka vichakani  wakanifunga macho wakaniacha nikakaa siku nzima", amesema Mtoto huyo.

Vile vile mtoto mwigine mwenye umri wa miaka 12 mwanafunzi wa darasa la nne amesema kuwa ukoo wao umekuwa ukilazimisha akeketwe jambo ambalo limemlazimu kukimbia ili asikeketwe.

“Ukoo ulikuwa unataka kunikeketa lakini mama alipiga simu polisi na ndipo niliokolewa. Mimi nasoma shule ya msingi Kimusi darasa la nne pia nataka kusoma sitaki ukeketaji”, anasema mtoto huyo.

Watoto wengi ni wanafunzi hivyo wanapokataliwa na wazazi ikumbukwe wanakosa haki yao ya masomo, licha ya shirika hilo kuamua baadhi ya wanafunzi kupelekwa shuleni na wazazi wanawavizia njiani kuwakamata kwa nguvu ili kurejeshwa makwao  lakini wanafunzi huenda wakashuka kitaluma kwa sababu ya msongo wa mawazo kwani baadhi  wanawaza ukeketaji, kukataliwa na wazazi , mazingira mapya ya masomo ambayo hawakuyategemea au  sasa ifike hatua Mila kandamizi zitokomezwe  na sheria zifanyiwe kazi pale waharifu wanavyobainika.

Ikumbukwe katika siku 16 za kupinga ukatili hatuna budi kuendelea kupaza sauti kwa lengo la kusaidia watoto wadogo ambao hawana uwezo wa kupaza sauti hivyo waandishi wa habari Mashirika mbalimbali na serikali ni jukumu letu kutetea na kulinda watoto wasio na hatia.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger