Serikali imezitaka timu zote za mpira zinazoajiri makocha na wachezaji kutoka nje ya nchi kutoa taarifa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya waajiriwa walionao wanaotakiwa kulipa kodi.
Hayo yameelezwa bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipokuwa akijibu swali la Nyongeza la Mbunge wa Chemba Mhe. Juma Selemani Nkamia, aliyetaka kujua Serikali inatambuaje Kocha au Mchezaji wa Nje aliyelipa na asiyelipa kodi kwa kuwa malipo yao hufanywa kiholela kwa kuwa hakuna mfumo rasmi.
Dkt. Kijaji alisema kuwa Kila mtu anayepata mapato yatokanayo na ajira ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anawajibika kulipa kodi ya mapato kulingana na kipato chake.
“Kila mgeni akifikisha miezi 6 anahesabika ni mkazi (local resident) na anapaswa kulipa kodi, ni jukumu la mwajiri kutoa taarifa ya nani analipwa nini ili kodi zote stahili ziweze kulipwa kwa mujibu wa sheria”, alieleza Dkt. Kijaji.
Alisema kuwa ulipaji wa kodi ya ajira ni kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004 na ni jukumu la mwajiri kwenda kutoa taarifa kwenye Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) ya waajiriwa walionao wanaotakiwa kulipa kodi hiyo.
Dkt. Kijaji alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2017/2018 jumla ya Sh. milioni 1,733.6 zilikusanywa kama malipo ya kodi ya ajira kutoka kwa makocha na wachezaji wa kigeni wanaofanya kazi hapa nchini.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment