Na Lulu Mussa
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Zungu amesema Serikali iko katika tafiti kuhakikisha matumizi ya gesi kama mbadala wa kuni na mkaa yanakuwa ya bei nafuu kwa wananchi wote.
Hayo ameyasema hii leo Jijini Dar es Salaam mara baada ya kufanya ziara ya kikazi katika Vyombo vya Habari vya Azam Media na Mwananchi Communications.
Amesema changamoto kubwa hivi sasa ni kukithiri kwa ukataji wa miti kwa matumizi ya kuni na mkaa. Hivyo katika kukabiliana na tatizo hilo suluhu ya haraka na rafiki kwa mazingira ni matumizi ya gesi, “Tunakuja na programu ya kuweza kulipia gesi kadri unavyotumia (paymetre)” Zungu alisisitiza.
Waziri Zungu amesema kuwa kwa siku mwananchi anatumia sio chini ya shilingi 1500 -2000 kununulia mkaa, gesi tunayoongelea itagharimu kati ya Shilingi 900-1000 na tafiti zinaendelea ndani ya Serikali kwa kushirikiana na wadau. “Tunataka bei ya gesi ishuke ili wateja wawe wengi ili kunusuru mazingira yetu”.
Katika hatua nyingine Waziri Zungu amewatahadharisha wananchi kuwa makini na ununuzi wa mifuko mbadala aina ya Non-Woven ambayo haikidhi viwango vilivyoainishwa.
Amesema kuwa mifuko aina ya Non-Woven ni lazima ikidhi viwango vya ubora vilivyoainishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ikiwa ni pamoja na kuwa na uzito usiounguza (GSM 70), iwe inaweza kurejelezwa, ionyeshe uwezo wa kubeba na iwe imethibitishwa na TBS.
“Nawasihi wananchi wetu kuwa makini na mifuko isiyokidhi viwango vya ubora kwa kuwa ina athari kwa mazingira na kiuchumi. Mifuko inayotengenezwa nchini mingi inakidhi viwango vilivyoweka na hivyo inachangia ulipaji wa kodi na maendeleo ya taifa letu. Mifuko isiyokidhi viwango inatoka nchi jirani na inaua viwanda vya Tanzania” Zungu alisisitiza.
Amesisitiza kuwa walinzi wakubwa wa mazingira ni wananchi wenyewe hivyo ametoa wito kwa umma kutoa taarifa kwa wote wanaokiuka Sheria ya Mazingira ili Sheria ichukue mkondo wake.
0 comments:
Post a Comment