Sunday, 9 February 2020

MZEE WA MILA ZA KISUKUMA AWAMWAGIA SIFA WANAWAKE....AWAPA MBINU ZA KUSHIKA NAFASI ZA UONGOZI

...
Mzee Mila na Tamaduni za Kabila la Kisukuma Sonda Kabeshi.
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mtafiti wa kujitegemea wa masuala ya mila na tamaduni za kabila la Wasukuma mzee Sonda Kabeshi ambaye ni Mkazi wa mtaa wa Mwasele kata ya Kambarage Manispaa ya Shinyanga ameitaka jamii kuwapa nafasi za uongozi wanawake kwani ni waaminifu na waadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao ukilinganisha na wanaume. 

Akizungumza na Malunde1 blog leo Jumapili Februari,2020 Mzee Kabeshi amesema masuala ya uongozi katika dunia ya sasa ni ya wote,wanaume na wanawake, hatupo kwenye enzi za utawala wa Kitemi ulioambatana na mila zilizokuwa zinakandamiza wanawake na kuwa na mtazamo kuwa hawawezi kuongoza jamii. 

Mwaka 2020 ni mwaka wa uchaguzi mkuu wa Tanzania,kuchagua madiwani,wabunge na Rais, Mzee Sonda Kabeshi anavikumbusha vyama vya siasa kuwapa nafasi za uongozi wanawake huku akiwasisitiza wanawake kuacha uoga,wajiamini kuwa wanaweza kugombea na kushinda katika uchaguzi na kuwa viongozi. 

“Mwanamke ni mtu mwaminifu sana katika masuala ya utekelezaji,apewe uhuru,nafasi ya kutobanwa.Kitendo cha kumchukulia kuwa mwanamke ni mtu wa kuongozwa tu huo ulikuwa ni mfumo wa kitemi uliokuwa unamkandamiza mwanamke”,amesema Kabeshi. 

“Katika enzi za utawala wa Kitemi, wanaume walikuwa wamejiwekea sheria zao na baadhi ya watu bado wanarithi baadhi ya mila. Mila hizo za zamani zilikuwa zinabagua na kukandamiza kwa mfano Mwanamke hakutakiwa kula hata nyama ya ulimi kwa madai kuwa atamtawala mwanamme,atakuwa sauti ‘ataongea’ kuliko mwanaume. Dunia ilipofikia sasa mila na tamaduni hizo zimepitwa na wakati”,ameeleza Kabeshi. 

Mzee Kabeshi amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuwapa nafasi za uongozi wanawake kutokana na uchapakazi na uaminifu wao katika utendaji kazi akibainisha kuwa hata Watemi waliwaamini wanawake, ndiyo maana mtoto wa mwanamke ndiyo alikuwa anapewa Utemi badala ya mtoto wa mwanaume kwa sababu mwanamke wanajua kutunza siri. 

Amebainisha kuwa wanawake wana huruma, wanajua kupanga bajeti na wanafanya kazi kwa nidhamu kubwa kuliko wanaume ambao mara nyingi ndiyo wamekuwa wakijihusisha na ufisadi,ubadhirifu wa mali za umma.

"Endapo mwanamke akifanya kazi bila kuingiliwa na mwanaume utendaji kazi wake utakuwa mzuri sana. 
Ukikuta mwanamke anafanya kazi vibaya,anaharibu kazi ujue kuna mkono wa mwanaume,pengine anapewa maelekezo na ushauri mbaya na mwanaume au pengine ni visa tu vya mwanaume pale anapokataliwa na mwanamke hivyo anaanza kumkwamisha mwanamke huyo”,amefafanua Kabeshi. 

“Muda wa kazi huwezi kumkuta mwanamke yupo baa na sare zake lakini Mwanaume huwa ni mtu wa kwanza kutoka ofisini kwenda kutafuta mambo yasiyohusiana na mambo ya ofisi,mfano kwenda kwenye vijiwe vya kahawa na pombe”,amesema Kabeshi. 

Amewashauri wanawake wenye kiu ya kuwa viongozi katika jamii hususani ngazi za kisiasa kujitafakari na kujiamini kuwa wanaweza kuwa viongozi wazuri wenye kuleta mabadiliko chanya katika jamii hivyo kuwataka wanaume kuwaunga mkono na kuwapa ushirikiano wanawake. 

“Wapo baadhi ya wanawake wanahofia kugombea nafasi za uongozi katika jamii kwa kuogopa kuvunja ndoa zao kwani kuna wanaume wanahofia wake zao wakiwa viongozi ndoa zao zitavunjika wanadhani wake zao wakiwa viongozi watawasaliti na kuwadharau.Bado kuna wanaume wana mawazo hasi,wanawazia zaidi kuhusu wake zao badala ya kazi za wake zao”,ameeleza Kabeshi. 

“Naomba wanaume waondoe mawazo hasi kwani mwanamke akipata nafasi ni faida yako,ni faida yako. Mke wako akiwa kiongozi mwanaume unapata sifa na unachukuliwa pia kama kiongozi,kama mkeo ni mbunge basi nawe unapata heshima,unakuwa nusu mbunge”,ameshauri Kabeshi. 

Aidha amesema msingi wa uongozi unaanzia nyumbani na baraka inaanzia nyumbani.

 “Mwanamke usitafute uongozi kama unatoroka,mshirikishe mme wako,ndugu zako,wakupe baraka usije akatoka tu na kumwambia mme wako kuwa tayari umejaza fomu,utaleta balaa utaonekana umemdharau mmeo na atasema umepata washauri wengine”,amesisitiza Kabeshi. 

Aidha mzee huyo wa mila amewasihi wanawake wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi,pale wanapoona dalili za malengo ya kuonekana yanataka kushindika waombe ushauri kwa watu wanaowazunguka badala ya kukata tamaa. 

“Mwanamke mwenye kiu ya uongozi ukiona mmeo hakupi ushirikiano tafuta watu walio karibu na mme wako ili wakupe ushauri na wamshauri na kuwe na mifano hai kwa kuelezea juu ya wanawake walioshika nyadhifa za uongozi.

“Ewe Mwanaume usimpe kikwazo mkeo. Kama wewe hujaandikiwa kuwa kiongozi,hujapangiwa na Mwenyezi Mungu kuwa kiongozi,muachie nafasi mkeo,kwani yeye ana karama zake na niwakumbushe kuwa nyota ya mme na mke ukizichanganya familia inakuwa bora",amesema Mzee wa mila Kabeshi.

Amebainisha kuwa mambo ya uongozi hayana jinsi ni ya kila mtu, ni akili yako,kipaji chako na karama kutoka kwa mwenyezi Mungu na kwamba unaweza kufanya karama yako isionekane kwa kutojiamini kutenda jambo ambalo lipo ndani ya uwezo wako. 

Mwanaume usimzuie mke wako kwa sababu anaweza kuwa na karama ya uongozi,amejaaliwa karama ya uongozi wewe ukawa kikwazo kwa sababu Mungu kampa karama hiyo….Wanaume waunge mkono wanawake,ikiwezekana wanaume wawe wapiga debe wa wake zao”, ameongeza.

Mzee Kabeshi amesema wanawake wana marafiki wengi zaidi kuliko wanaume katika jamii hivyo endapo watagombea nafasi za uongozi watapata mashabiki wengi na watasaidia kutatua changamoto zinazoikabili jamii. 

“Wanawake ni mama zetu, tukiwapa uongozi wao watatuhesabu sisi kama watoto wao,kwa sababu wana huruma na siku zote kile anachokipata mwanamke huwa anakileta katika familia na jamii tofauti na wanaume ambao wao ni kutoa tu”,amesema. 

“Wanawake wanalindana na kuhurumiana,lakini wanaume wanazomeana pale mwenzao anapopata tukio au balaa.Hata kwenye msiba wanaolia wenye uchungu zaidi ni wanawake.Sisi wanaume hatuna huruma”,ameeleza Kabeshi. 

Mzee Sonda Kabeshi ni Mtafiti wa Kujitegemea wa Mila na Tamaduni za kabila la Wasukuma, mkazi wa mtaa wa Mwasele kata ya Kambarage Manispaa ya Shinyanga anapatikana kwa simu namba 0785009781 

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger