Saturday, 15 February 2020

MADIWANI USHETU WAOMBA MTAALA MPYA MAADILI KWA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI

...


Kaimu mkuu wa kanda,ofisi ya Rais sekretarieti ya maadili ya viongozi Gerald Mwaitebele akizungumza na madiwani na wakuu wa idara na vitengo katika halmashauri ya Ushetu hawapo pichani

Baadhi ya watumishi wa halmashauri ya Ushetu wakisikiliza kwa makini mafunzo ya maadili kwa viongozi wa umma.
Mwenyekiti wa halmashauri ya Ushetu Juma Kimisha akifungua mafunzo ya maadili kwa viongozi wa Umma kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Kahama ambaye alikuwa ni mgeni rasmi.
Madiwani wa halmashauri ya Ushetu wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi kutoka tume ya maadili ya viongozi wa umma kanda ya Magharibi (Tabora).
***

Na Salvatory Ntandu - Malunde 1 blog
Baraza la madiwani la halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga limeiomba wizara ya elimu sayansi na teknolojia kuanzisha mtaala mpya utakaohusu maadili katika shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu utakaowawezesha wanafunzi kuwa na maadili pindi wamapomalizapo masomo yao.

Ombili hilo limetolewa Febuari 13 mwaka huu katika mafunzo ya siku moja ya uzingatiaji wa maadili kwa viongozi wa umma na namna bora ya kujiepusha na migongano ya kimaslahi yaliyotolewa na Ofisi ya sekretarieti ya maadili ya viongozi wa UmMa kanda ya magaharibi (Tabora) yaliyofanyika katika makao makuu ya halmashauri hiyo Nyamilangano.

Esta Matone ni diwani wa viti maalumu kata ya Bulungwa alisema kuwa elimu ya maadili ni muhimu kutolewa kwa ngazi zote hususani wanafunzi kuanzia ngazi ya awali hadi chuo kikuu ili kujenga taifa la watu waaminifu wasiotanguliza maslahi yao pindi wanapokabidhiwa mamlaka katika serikali.

“Tunaipongeza ofisi ya maadili kwa kutupatia mafunzo haya muhimu kwetu sisi viongozi nawaomba mwende ngazi zote za elimu ili suala la maadili liweze kupewa kipaumbele ili taifa letu liweze kusonga mbele katika nyanja za kimaendeleo”,alisema Matone.

Akitolea ufafanuzi wa suala hilo kaimu mkuu wa kanda,ofisi ya Rais sekretarieti ya maadili ya viongozi Gerald Mwaitebele alisema suala hilo linafanyiwa kazi ambapo hadi sasa wameanzisha klabu za maadili katika shule za msingi na sekondari ambazo zinajukumu la kuwafundisha kuhusiana na maadili.

“Tunaendelea kutoa elimu ya maadili katika shule za msingi na sekondari kwa kuwafundisha wanafunzi wetu kuwa waadilifu ili kuhakikisha taifa linapata viongozi waaminifu na wachapa kazi wasiotanguliza maslahi yao”,alisema Mwaitebele.

Alifafanua kuwa elimu ya maadili ni muhimu ndiyo maana ofisi yake inaendelea kuzunguka katika mkoa yote ya kanda ya maghabi ili kuwakumbusha viongozi wa umma kuhusiana na sheria ya maadili ya viongozi wa umma ili waweze kutoa huduma nzuri kwa wananchi wanao wahudumia.

Awali akifungua mafunzo hayo mwenyekiti wa halmashauri ya Ushetu, Juma Kimisha diwani wa kata ya Nyamilangano ambaye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha aliwataka viongozi na madiwani kuzingatia maadili ili kuepuka kujiingiza katika migongano ya maslahi hususani katika usimamizi wa miradi ya maendeleo.

“Wahudumieni wananchi bila ya upendeleo,tangulizeni uzalendo kwa kuzingatia sheria ya maadili ya viongozi wa umma namba 13 ya mwaka 1995 ambayo inatutaka tufanye kazi kwa weledi na kujiepusha na vitendo vya rushwa”,alisema Kimisha.

Mafunzo hayo ya siku moja yamehudhuriwa na madiwani wa kata 20 zilizopo katika halmashauri ya Ushetu pamoja na wakuu wa idara na vitengo.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger