Serikali ya Tanzania inatarijia kukutana na Timu ya wataalamu kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwa ajili ya kujadili Programu mpya ya Ushauri wa Kisera (PSI) yenye dhima ya kusimamia sera za kiuchumi kwa lengo la kutatua changamoto zitakazoonekana pamoja na namna ya kutumia fursa mbalimbali zilizopo nchini.
Haya yameelezwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi mpya wa IMF nchini, Bw. Jens Renke, aliyekuja kujitambulisha rasmi kwa Waziri huyo jijini Dodoma baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo hapa nchini.
Dkt. Mpango alisema kuwa pamoja na kufanya majadiliano na wataalamu hao, Serikali inatarajia kuwa wataafikiana nao ili kuanzisha programu hiyo ya Serikali ambayo Shirika hilo limekuwa likishauri.
“Tumekuwa tukishirikiana na IMF kwa muda mrefu na imekuwa ikitushauri mambo mbalimbali ya kusimamia Sera za Kiuchumi katika kuondoa changamato ya umasikini na kuwa na maendeleo endelevu kwa usimamizi wa Sera za Uchumi “, alieleza Dkt. Mpango.
Aidha Dkt. Mpango alimueleza Mwakilishi huyo kuwa vipaumbele vya Serikali na juhudi mbali mbali zilizofanyika katika kukabiliana na tatizo la umaskini ni pamoja na kujenga uchumi jumuishi, kusimamia fedha za umma vizuri, kuhakikisha kwamba nchi inaendelea kuwekeza katika kilimo pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kisasa.
Waziri Mpango alibainisha kuwa vipaumbele vingine ni pamoja na kuziba mianya ya rushwa na kukusanya mapato ya ndani ipasavyo ili kuweza kutumia rasilimali zote za nchi vizuri na kuboresha huduma muhimu za wananchi kama elimu na afya.
Aidha, alimueleza mgeni huyo kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana nae katika kuleta maendeleo nchini.
Naye Mwakilishi Mkazi mpya wa IMF nchini, Bw. Jens Renke, aliahidi kuwa balozi mzuri wa Tanzania katika Shirika hilo na kuiomba Serikali ushirikiano katika kazi zake.
Aliiomba Serikali imtumie katika kutatua matatizo mbalimbali na yuko tayari kutoa ushauri wa kisera na kichumi, na kubainisha kuwa atafanya kazi kama sehemu ya Serikali katika kutatua matatizo na kuleta maendeleo nchini.
Bw. Renke alisema anapenda kujifunza mengi nchini na atatembelea katika mikoa, Serikali za Mitaa pamoja na vyuo mbalimbali ili kuona mambo ambayo Serikali imeyafanya katika kujikwamua kiuchumi.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment