Tuesday, 4 February 2020

DKT NCHIMBI AJA NA MJALI MTOTO WA KIKE KWA MAENDELEO YA TAIFA,RAS DKT LUTAMBI APIGILIA MSUMARI

...



Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi  (mwenye nguo za kijani ) akiwapatia wanafunzi  wa Shule ya Sekondari Ikungi boksi la  taulo za kike. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi(mwenye suti nyeusi) Edward Mpogolo, kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Ikungi Justice Kijazi


 Wanafunzi wa shule ya Sekondari  ya Ikungi wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi  mara baada ya kupokea maboksi ya taulo za kike kutoka kwa wadau mbalimbali.
Mkuu wa Mkoa wa Singida  Dkt. Rehema Nchimbi (mwenye skafu) na Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Lutambi wakijadiliana  mara baada ya kutoka kwenye mkutano wa mafanikio  ya miaka 4 ya Rais Magufuli ambapo Waziri wa TAMISEMI Suleimani Jaffo alipongeza jitihada za Mkoa wa Singida kwenye utoaji wa huduma za afya.


Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Ikungi Justice Kijazi (mwenye suti ya Bluu)  akiwa  pamoja na Mganga Mkuu wa Mkoa Singida, Victorina Ludovick (mwenye sketi nyeusi)na Afisa Elimu Taaluma Mkoa wa Singida(mwenye suruali nyeusi), Mwalimu Eva Simon Mosha wakicheza kuhamasisha uchangiaji wa taulo za kike.

Na John Mapepele

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi  ametoa onyo kali kwa wawekezaji na wafanyabiasha wa kutengeneza na kuuza taulo za watoto wa kike  kuacha  mara moja tabia ya kutengeneza taulo zisizo  na ubora kwa kuwa Mkoa wake umeanzisha msako wa kiintelijensia na kistratejia wa kuzisaka taulo zisizo na ubora  ambapo  atakayebainika sheria itachukua mkondo wake mara moja.

Dkt Nchimbi ameyasema haya leo wilayani Ikungi wakati wa zoezi maalum la uzinduzi wa uchangishaji wa taulo za mtoto wa kike katika Mkoa wa Singida lililopewa jina la “Mjali mtoto wa kike kwa maendeleo yake na Taifa lake” ambapo ametoa rai kwa wadau wote kushiriki kikamilifu katika kuwabaini na kutoa taarifa za wafanyabiashara watakaojaribu kuuza taulo zisizo na ubora ili kuwalinda watoto wa kike

Alisema kutokana na mageuzi makubwa ya kiuchumi yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Magufuli nchi yetu imekuwa kwenye mashindano ya kiuchumi duniani hivyo mikakati madhubuti ya kudhibiti ubora unahitajika katika kipindi hiki kuliko kipindi kingine chochote.

Dkt Nchimbi alisema vyombo vya dola, viongozi wa dini na wazazi wana mchango mkubwa katika kumlinda mtoto wa kike kwa ustawi wa taifa letu.
“Ndiyo maana tunasema na tunamaanisha kuwa tunataka kujua mipango ya udhibiti wa ubora kwa watengenezaji hawa kwa kuwa majuto ni mjukuu, tusisubiri kufika huko “ alisisitiza Dkt .Nchimbi

Aliongeza kuwa ubora wa taulo za kike ni ubora wa maisha yao hivyo ni muhimu  kuchukua hatua za kuangalia na kudhibiti mnyororo mzima wa uzalishaji na usambazaji wa taulo sizizo kuwa na ubora.

Aidha alitoa wito wa wajasiliamali kuja na andiko zuri la utengenezaji wa taulo bora za kisasa zitakazotengenezwa kwa kutumia malighafi za hapa nchini ambapo alisema mshindi atakayepatikana atamzawadia tuzo  ya shilingi milioni moja.

Aliwataka watoto wa kike kote nchini kujiamini kwa  kuumbwa wanawake na kwamba hedhi ni kitu cha thamani kwa kuwa hedhi ni uhai ambapo alisisitiza  elimu ya jinsia na mtoto wa kike kutambua mabadiliko ya miili yao iendelea kutolewa ili kuwajenga watoto wa kike kujua thamani ambayo mungu amewajalia kwa kuwaumba wakamilifu.

Aliwataka wadau wote kuendelea kuchangia kwa kutambua thamani ya mtoto wa kike ambapo katika  uzinduzi wa huu lengo lilikuwa ni kuchangia paketi 8000 za taulo za kike lakini zilipatikana jumla ya paketi 9089 kulingana na fedha zilizotolewa.

Lengo la jumla kwa mwaka 2020 katika Wilaya ya Ikungi ni kuchangia taulo 192,000 kwa watoto wote wa kike kwenye shule 36 za Sekondari,  na shule  131 za Msingi  zenye jumla ya  watoto wa kike 16,000

Naye KatibuTawala Mkoa wa Singida Dkt Angelina  Lutambi amesema Serikali imeendelea kutoa kipaumbele katika huduma za afya zenye ubora na zinazowafikia wananchi wote ili kuboresha afya zao.

Dkt. Lutambi amesema Serikali inatambua umuhimu wa afya bora kwa wananchi wake kwani afya bora ni raslimali muhimu kwa maendeleo. Maendeleo ya Taifa letu la Tanzania yataletwa na wananchi wenye afya na wenye uwezo wa kuzalisha mali.

Aliongeza kuwa katika kuhakikisha kuwa wananchi wana afya bora, Serikali imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutoa huduma za afya kwa kuzingatia sera na miongozo iliyopo.

“Serikali haitamfumbia macho mdau yoyote wa utoaji wa huduma ya afya ambaye atafanya kazi   kwa mazoea bila kuzingatia  sheria na taratibu za utoaji huduma na kwamba kuanzia sasa Serikali itakaa na kupanga  kwa pamoja ili kuwapatia wananchi huduma  bora wakati wote kwa wananchi wa Mkoa wa Singida na taifa kwa ujumla” amesisitiza Dkt. Lutambi

Aidha, Waziri wa Nchi,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Selemani Jafo, amepongeza juhudi zinazofanywa  na Serikali ya Mkoa wa Singida kwenye  utoaji wa huduma za afya  wakati akiwasilisha  mafanikio ya TAMISEMI kwa kipindi cha miaka mine ya Rais Magufuli
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa wazo la kutaka Halmashauri zote katika Mkoa wa Singida kutoa elimu ya jinsia mashuleni na kuwachangia wa watoto wa kike taulo hizo kwa kuwa jambo lenye manufaa kwa taifa kwa kuwa ukimuelimisha mtoto  wa kike umeelimisha taifa zima.

Alizitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili watoto wa kike kuwa ni pamoja na mimba za utotoni,kubakwa,kuozeshwa katika umri mdogo na kufanyishwa kazi  nyingi nyumbani.

Mratibu wa program hii ya  uchangiaji wa taulo za mtoto wa kike ambaye pia ni Afisa Maendeleo wa jamii wilaya ya Ikungi Haika Massawe alipendekeza wazazi wahusishwe kikamilifu katika  program hii.

Alisema vyombo vya Serikali  kama polisi na mahakama  vitende  haki katika kushughulikia haki za mtoto wa kike aidha  wazazi wa wanafunzi wa kike mashuleni  waelekezwe kutoa fedha  maalum kwa ajili ya kununua taulo za watoto wao.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger