MARAIS wanane wa Afrika ni miongoni mwa viongozi mbalimbali kutoka nje ya nchi, watakaohudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli.
Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Magufuli ataapishwa rasmi kuwa Rais wa Awamu ya Tano kesho kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Dk Magufuli (56) alitangazwa mshindi wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, baada ya kupata kura 8,882,935, sawa na asilimia 58.46 ya kura halali zilizopigwa, hivyo kumrithi Rais Jakaya Kikwete katika Ikulu ya Magogoni, ambayo tayari imeshakaliwa na marais wengine wanne.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa iliyotolewa jana Dar es Salaam, sherehe za uapisho zitahudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa mbalimbali, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na Kikanda na Wawakilishi mbalimbali kutoka nje ya nchi. Iliwataja miongoni mwa marais watakaohudhuria sherehe hizo ni Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Rais Paul Kagame wa Rwanda na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini.
Wengine ni Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji na Rais Edgar Lungu wa Zambia. Taarifa ya Mambo ya Nje ilieleza kuwa Malawi itawakilishwa na Makamu wa Rais, Saulos Chilima wakati Namibia itawakilishwa na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje, Netumbo Nandi-Ndaitwah. Aidha, Serikali ya China itawakilishwa na Makamu Mwenyekiti wa Chama Tawala.
“Vilevile nchi nyingine ambazo zimethibitisha kushiriki na zitawakilishwa na kati ya Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Spika au Balozi ni pamoja na Burundi, Comoro, Angola, Botswana, Lesotho, Madagascar na Mauritius. “Nyingine ni Norway, Oman, Sudan Kusini, Sweden, Umoja wa Falme za Kiarabu, Marekani, Uingereza, Shelisheli, Swaziland, Algeria, Misri, Benin, Denmark, Ethiopia, Finland, Ufaransa, Ghana, India, Japan, Kuwait, Uholanzi na Nigeria,” ilifafanua taarifa hiyo.
Ilieleza kuwa Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na Kikanda, waliothibitisha kushiriki au kutuma wawakilishi wao ni Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Ulaya (EU) na Jumuiya ya Ukanda wa Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR).
Wabunge wapya kuwasili Dar Katika hatua nyingine, wabunge wapya waliochaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wanatarajiwa kuwasili Dar es Salaam leo kwa ajili ya kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais Mteule, Dk John Magufuli zitakazofanyika kesho.
Akizungumzia kuwasili kwa wabunge hao, Ofisa Habari Mwandamizi wa Bunge, Prosper Minja alisema wabunge hao wanatarajiwa kuwasili leo Dar es Salaam wakiwa na vyeti vyao vya kuteuliwa kuwa wabunge vinavyotolewa na Msimamizi wa Uchaguzi wa eneo husika.
“Tunategemea kesho (leo), wabunge wapya watawasili kwa ajili ya kuhudhuria sherehe ya kuapishwa kwa rais mteule na tunategemea waje na cheti hicho pamoja na kitambulisho kingine kinachomtambulisha,” alisema Minja.
Alisema mara baada ya wabunge hao kuwasili, wanatakiwa kwenda Ukumbi wa Karimjee kwa ajili ya kutambuliwa na kupewa kitambulisho cha siku ya sherehe za kuapishwa kwa Rais Mteule, Dk Magufuli.
Tamko la Jeshi la Polisi Wakati huo huo, Jeshi la Polisi nchini limejipanga kuhakikisha usalama na ulinzi unaimarishwa wakati wa kuelekea sherehe za kumwapisha Rais Mteule, Dk John Magufuli.
Akizungumza jana Dar es Salaam, Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo, Makao Mkauu ya Polisi, Paul Chagonja alisema jeshi lake kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama, litahakikisha kunakuwa na usalama wa raia na mali zao katika kuelekea sherehe za kumuapisha Rais Mteule.
“Niwaombe wananchi kutupa ushirikiano kwa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi pindi waonapo vishawishi ama vitendo vyovyote vya uvunjifu wa sheria,” alisema Kamishna Chagonja. Aidha, Chagonja aliwataka wananchi kuendelea kuheshimu sheria za nchi na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa raia na mali zao.
“Jeshi la Polisi linawataka wananchi kote nchini kuendelea kuheshimu sheria za nchi na kujiepusha na vitendo vya aina yoyote ile ambavyo vinaweza kuhatarisha usalama wa raia na mali ikiwemo maandamano yanayopangwa bila kufuata taratibu,” alisema Chagonja na kuongeza: “Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali kwa mtu au kikundi chochote kitakachoonesha viashiria vya uvunjifu wa sheria ama kutaka kuvuruga amani ya nchi yetu.”
Mbali ya kuwashukuru wananchi na wadau waliotoa ushirikiano kuhakikisha amani ya Watanzania inadumu katika kipindi cha uchaguzi na wakati huu wa kuelekea kuapishwa kwa Rais Mteule, alikiri jeshi hilo kuwashikilia watu kadhaa na baadhi yao kufikishwa mahakamani kutokana na kufanya makosa wakati wa uchaguzi.
Bila kutaja idadi, Chagonja alisema, “Ni kweli kuna watu kadhaa tumewakamata kwa makosa mbalimbali wakati wa uchaguzi, kuna wengine wamefikishwa mahakamani, na kuna wengine bado wanashikiliwa kwa mahojiano zaidi na wengine wamewekewa dhamana.” Imeandikwa na Ikunda Eric na Anastazia Anyimike.
0 comments:
Post a Comment