TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeteua wabunge wa Viti Maalumu na kuwasilisha orodha ya wateule hao katika vyama husika vya siasa.
Vyama ambavyo vimepata nafasi ya kuwa na wabunge hao ni vitatu ambavyo vimekidhi vigezo vya kikatiba na kisheria vya kupata angalau asilimia 5 ya kura zote halali za wabunge.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva, alisema vyama vilivyokidhi vigezo hivyo ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama cha Wananchi (CUF).
Hata hivyo Jaji Lubuva alisema, majina ya wabunge wa Viti Maalumu yatapatikana katika vyama husika kwa mujibu wa orodha iliyowasilishwa NEC na kila chama, ili Tume ifanye uteuzi. Alisema kulingana na vigezo vya kupata kura asilimia tano, CCM imepata wabunge 64, Chadema 36 na CUF wabunge 10.
Kwa uteuzi huo, CCM iliyokuwa na wabunge wa majimbo 182, sasa inakuwa na jumla ya wabunge 246, huku Chadema yenye wabunge wa majimbo 35 ikiwa na jumla ya wabunge 71 na CUF yenye wabunge 39 wa majimbo, ikipata jumla ya wabunge 49.
ACT na NCCR-Mageuzi wamebakia na mbunge mmoja kila chama. Kwa kufuata aina ya ushirikiano wa vyama vya upinzani chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kambi Rasmi ya Upinzani itakuwa na jumla ya wabunge 121 sawa na asilimia 46.8.
Katika Bunge la 10, ambalo limemaliza muda wake, kulikuwa na wabunge wa majimbo 254, kati ya hao CCM ilikuwa na wabunge 186, CUF 23, Chadema 24, NCCRMageuzi wanne na UDP mmoja.
“Kigezo cha kupatikana kwa wabunge wa viti maalumu ni kura zote halali walizopata wabunge wa vyama vyote katika majimbo yaliyofanyika uchaguzi,” alisema Jaji Lubuva.
Alisema kwa mujibu wa Ibara ya 66(1)(b) na Ibara ya 78 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 vikisomwa pamoja na kifungu cha 86A cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343, Tume imepewa mamlaka ya kutangaza viti maalumu vya wabunge wanawake visivyopungua asilimia 30 ya wabunge wote.
Hata hivyo kwa mujibu wa uamuzi wa Serikali wa mwaka 2010 idadi ya wabunge wa viti maalumu iliongezwa na kufikia asilimia 40 na hivyo katika uchaguzi uliofanyika mwaka huu, idadi ya wabunge wa viti maalumu ni 113.
“Kutokana na kuwepo majimbo nane ambayo hayakufanya uchaguzi mgawanyo wa viti maalumu kwa sasa ni 110. Viti vitatu vilivyobaki, vitagawanya baada ya uchaguzi kufanyika katika majimbo hayo,” alisema Jaji Lubuva.
Jaji Lubuva alisema, pia kuna idadi ya wabunge watano ambao wanateuliwa na Baraza la Wawakilishi na hao watapatikana baada ya mchakato wa uchaguzi kukamilika. Alitaja kura halali na zilizopatikana na vyama vyao ni CCM kura 8,333,953, Chadema 4,627,923 na CUF 1, 257,051, ambazo zimetumika kupata wabunge hao wa viti maalumu.
0 comments:
Post a Comment