Aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema) chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
Edward Lowassa (wa pili kulia), akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam jana juu ya hali ya kisiasa nchini. Wengine ni
Kaimu Mwenyekiti wa Cuf, Twaha Taslima (wa kwanza kushoto), Makamu
Mwenyekiti wa Chadema, Prof. Abdallah Safari (wa pili kushoto) na
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia (wa kwanza kulia). PICHA: MPOKI
BUKUKU
Aidha, amewataka Watanzania kutoyakubali matokeo hayo na kuyapinga
kwa nguvu zao zote bila ya kuandamana na kufanya fujo na kwamba umoja
huo hautashirikiana na serikali ya Dk. Magufuli kwa madai haikuingia
madarakani kihalali.
Lowassa alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa jijini
Dar es Salaam jana juu ya hali ya kisiasa nchini na mustakabali wa
Zanzibar baada ya kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa visiwa hivyo.
ATAJA SABABU ZA KUPINGA
Lowassa alisema yeye na wenzake ndani ya Ukawa hawaukubali na
ushindi alioupata Dk. Magufuli kwani wana ushahidi wa kutosha juu ya
namna Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake kilivyopora ushindi
wake (Lowassa) kwa kuyakachakua matokeo.
Hata hivyo, Lowassa hakuwa tayari kuuweka wazi ushahidi, akisema atafanya hivyo wakati muafaka ukifikaa ambao pia hakuutaja.
Alitaja sababu nyingine za kutokukubali na ushindi wa Dk. Magufuli
kuwa ni, matumizi makubwa ya vyombo vya dola wakati wa uchaguzi.
Alisema wakati wa uchaguzi huo serikali ilitumia nguvu kubwa na
vitisho vya askari wenye silaha za kivita ikiwamo kutumia magari yenye
maji ya kuwasha yaliyonunuliwa kwa mabilioni ya fedha, ambayo yalikuwa
yanarandaranda mitaani, ili matokeo aliyodai ya wizi huo wa kura
yakubalike.
Sababu nyingine aliyoitoa Lowassa ni hatua ya serikali kupinga
maandamano ya Ukawa na kuvitisha vyombo vya habari kufanya kazi zake kwa
uhuru.
Nyingine alisema ni hatua ya serikali kupiga marufuku mikutano ya
kisiasa iliyopangwa kufanywa na viongozi wa Ukawa na kuwanyima viongozi
hao fursa ya kuwashukuru wananchi kwa kuwapigia kura baada ya uchaguzi.
“Wanatumia gharama zote hizo huku bei ya vitu mbalimbali hasa
vyakula inapanda kwa kasi kubwa, kama CCM inadai imeshinda kwa nini wana
hofu kubwa mpaka kuhujumu uhuru wa vyombo vya habari, kupiga marufuku
mikutano ya kisiasa na kunyima viongozi wa Ukawa hata fursa ya
kuwashukuru wananchi kwa kutuunga mkono katika safari yetu ya kuleta
mabadiliko, hii ni aibu kwa taifa letu,” alisema Lowassa na kuongeza:
“Tuna ushahidi wa kutosha jinsi matokeo ya uchaguzi wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano yalivyochakachuliwa na kiasi cha kura zilizoibwa,
wakati muafaka tutaweka bayana ushahidi huo ili Watanzania wajue kwa
nini Ukawa inasema kwa dhati kwamba haitambui matokeo yaliyotangazwa na
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na kwa nini haitashirikiana na serikali
ya sasa ambayo ni batili kisheria.”
Lowassa alisema endapo Katiba ingekuwa inaruhusu matokeo ya urais
kupingwa mahakamani wangefanya hivyo, lakini kwa kuwa hairuhusu
wataendelea kutoitambua serikali hiyo, huku akiwataka wananchi kukataa
matokeo hayo katika hali ya utulivu wakati Ukawa ikiendelea na harakati
nyingine za kisiasa katika nyanja mbalimbali ili kutekeleza azma yao ya
kuleta mabadiliko ya kweli nchini.
ZANZIBAR
Aidha, Lowassa alisema Ukawa unamuunga mkono mgombea urais wa
Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi(Cuf), Maalim Self Sharif Hamad, kama
mshindi wa uchaguzi mkuu visiwani humo na kuitaka Tume ya Uchaguzi
Zanzibar (Zec) imtangaze mara moja.
Alisema kinyume na Tanzania Bara ambako uchaguzi uligubikwa na
mizengwe, uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa wazi na wa amani, huku vyama
vyote vya siasa na hata waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa walisema
uchaguzi huo ulifanyika kwa amani, lakini wanashangaa Zec kufuta
uchaguzi huo.
Alisema uamuzi huo wa Zec unalaaniwa vikali na Ukawa na kwamba
uamuzi wa kutaka uchaguzi huo urudiwe hawakubaliani nao kwa kile
alichosema hizo ni mbinu mpya ambazo zimepangwa kuhujumu uchaguzi huo
na una lengo la kuhatarisha amani na utulivu visiwani humo.
“Wakuu wa Ukawa walikataa dhana kuwa uchaguzi uleule unaodaiwa
kufutwa kwa kuwa ulikuwa na mizengwe, ulizaa matokeo halali ya wabunge
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya urais wa Jamhuri,
lakini ni batili kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Rais wa
Zanzibar, dhana hii haina mantiki yeyote bali ni ubabe wa kisiasa,”
alisema Lowassa na kuongeza:
“Haiwezekani chungu kimoja kikapika halali na haramu kwa pamoja.
Kigezo cha Zec kuwa uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa batili, basi matokeo
yake yote ikiwa ni pamoja na yale ya urais wa Jamhuri pia ni batili. Hii
ina maana kuwa hata ushindi unaodaiwa wa Dk. Magufuli, mbali ya kuwa ni
matokeo haramu ya wizi kwa kura za Tanzania Bara, pia ni batili
kisheria kwani hana ridhaa ya watu wa pande zote mbili za Muungano.”
KATIBA MPYA
Lowassa alisema bado wataendelea kupigania kuandikwa kwa Katiba
mpya ambayo watahakikisha inazingatia maoni na matakwa ya Watanzania.
Alisema pasipo Katiba hiyo, matatizo mengi yanayojitokeza hivi sasa
hayatapatiwa ufumbuzi ikiwamo kuwa na tume huru ya uchaguzi na
serikali inayowajibika, huku akisisitiza kuwa katika mazingira ya sasa
na chini ya Katiba inayotumika sasa, Tanzania haitakuwa na demokrasia na
itaendelea kuwa nchi inayotawaliwa kwa mizengwe na udikiteta .
AELEZA HATMA YAKE
Lowassa alisema hatarudi nyuma wala kustaafu siasa, bali ataendelea
kuimarika katika nyanja hiyo kwa kuwa mstari wa mbele kupigania Ukawa
na mabadiliko.
MBATIA
Kwa upande wake, Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia, alisema
vurugu zinazoendelea hivi sasa na mauaji ya Watanzania katika matukio
tofauti na matumizi ya mabavu, itafika mahali Watanzania watakosa
uvumilifu na endapo machafuko yakitokea Rais Mstaafu wa awamu ya tatu,
Benjamin Mkapa, Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete pamoja na
Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva, wote watafikishwa katika mahakama
za kimataifa.
Mbatia alidai Kikwete atawajibika pamoja na mambo mengine kwa
kutumia nguvu kubwa kununua vifaa vya kivita vyenye thamani ya Sh.
bilioni 409 katika uchaguzi wa mwaka huu, huku akimtaja Jaji Lubuva
kwamba atawajibika kwa kukiuka sheria za uchaguzi kwa kuibeba CCM na
Mkapa atawajibika kwa kusababisha mauaji katika uchaguzi Mkuu 2001,
Zanzibar.
Akizungumzia kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa
Geita, Alphonce Mawazo, aliyeuawa juzi kwa kukatwa mapanga na watu
wasiojulikana, Mbatia alihusisha kifo chake na mauaji mengine ambayo
yamekuwa yakihusishwa na chuki za kisiasa.
Lowassa aliungana na Mbatia kulaani mauaji hayo na kulitaka Jeshi
la Polisi kufanya uchunguzi wa haraka ili kubaini waliohusika na
kuwachukulia hatua.
MALALAMIKO VITI MAALUM
Akizungumzia malalamiko kutoka maeneo mbalimbali nchini kuhusu
mgawanyo wa viti maalum kwenye nafasi ya ubunge ndani ya Chadema, Makamu
Mwenyekiti wa chama hicho, Prof. Abdallah Safari, alisema Chadema
imepokea malalamiko mengi kuhusiana na mgawanyo wa wabunge wa vitihivyo
na kwamba kinayafanyia kazi na yale ya msingi yatafanyiwa uamuzi na
yasiyo ya msingi yataachwa.
Naye Kaimu Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (Cuf), Twaha Taslima,
alisema masuala ya wabunge wa viti maalum yanazungumzwa ndani ya chama
na si katika vyombo vya habari.
Katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu, Nec ilimtangaza Dk. Magufuli wa CCM
kuwa mshindi wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano kwa kupata
asilimia 58.46 ya kura halali zilizopigwa, huku Lowassa akipata
asilimia 39.97.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment