Klabu ya soka ya Yanga, mbali ya kufaidika na mfumo mpya wa uendeshaji, pia itapata fursa ya mafunzo kwa wachezaji, makocha na viongozi kutoka klabu ya Sevilla ya Hispania.
Mkataba huo ambao msingi wake ni kuifanya Yanga kuwa na mfumo wa kisasa wa uendeshaji, umeenda mbali zaidi ambapo licha ya kucheza mechi mbili kwa mwaka baina ya Sevilla na Yanga, pia utatoa fursa kwa wachezaji chipukizi kujiunga na shule ya michezo ya timu hiyo yenye historia kubwa ya soka.
Kwa mujibu wa ofisa habari wa Yanga, Hassan Bumbuli kutakuwa na mechi mbili kwa mwaka baina ya timu yao na Sevilla ambayo moja itafanyika Hispania na nyingine hapa nchini.
Mbali ya mapendekezo ya mfumo wa uendeshaji, pia kutakuwa na suala mabadiliko ya Katiba ya klabu ambapo mpango wa klabu ya Yanga ni kuwahsirikisha wanachama na wadau wote kwa muda wa siku 21.
Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msolla alisema wawakilishi wa matawi kutoka kila pande za Tanzania watapata mafunzo maalumu jijini Dar es Salaam na kupewa makabrasha ambayo watayatumia kuendesha elimu ya mabadiliko hayo pindi watakaporejea kwenye matawi yao