Tuesday 29 October 2019

Taarifa Kwa Umma; Gavana Wa BOT Hajafungua Akaunti Ya “Facebook”

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inapenda kuutangazia umma kwamba Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Florens Luoga, hajafungua akaunti ya mtandao wa kijamii wa Facebook, kinyume na taarifa na picha zinazojitokeza katika katika mtandao huo kwa jina lake.

Kwa taarifa hii, tunapenda kuutangazia umma kupuuza chochote kinachopatikana katika akaunti hiyo bandia inayojiita Florence Luoga, na ambayo inatumia picha mbalimbali za Gavana wa BoT kinyume cha sheria.

Aidha, Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuwapa pole watu wote ambao kwa namna moja ama nyingine wameathirika kutokana na yote ambayo yamejitokeza katika akaunti hiyo bandia, ikiwemo kutumia jina la Gavana Luoga kutapeli na hata kutumiwa ujumbe wa matusi.

Pamoja na taarifa hii, hatua za kisheria zinaendelea kuchukuliwa ili kumbaini mhalifu huyu kwa kutumia akaunti hiyo kuchafua sifa ya Gavana Luoga katika jamii.

Tunauhakikishia umma kwamba, Gavana Luoga hajafungua akaunti kwa jina hilo na hivyo taarifa zozote zinazotolewa kwenye akaunti hiyo ya Facebook hazina uhusiano wowote na Prof. Florens Luoga.


Share:

WATER MISSION TANZANIA YAFANIKISHA MIRADI YA MAJI SALAMA KWENYE KAMBI ZA WAKIMBIZI MKOANI KIGOMA

 Mhandisi wa maji kutoka shirika la Water Mission Tanzania, OpitaTarcicous (kushoto) akitoa maelezo kwa ujumbe wa Balozi wa Denmark nchini Mette Nørgaard Dissing-Spandet (katikati) wakati wa uzinduzi wa mradi wa maji salama katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu mkoani Kigoma mwishoni mwa wiki ambao umetekelezwa na water Mission Tanzania , Poul Due Jensen Foundation, na wadau wengine.
Wakurugenzi kutoka taasisi za water Mission Tanzania , Poul Due Jensen Foundation wakitembelea mind main ya mradi.

 Ujumbe wa Balozi wa Denmark nchini na Wakurugenzi wa mashirika ya water Mission Tanzania , Poul Due Jensen Foundation na Water Mission International ukikaribishwa wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi wa maji wa Nyarugusu.  
Na Mwandishi Wetu. 

SHIRIKA la Kimataifa lisilo la Kiserikali la Water Mission Tanzania, linaendelea kuwanufaisha watu kwenye maeneo yenye shida ya maji nchini kwa kutekeleza miradi ya kuwapatia maji salama ikiwemo maeneo ya kambi ya Nyarugusu, mkoani Kigoma. 

 Water Mission Tanzania, imekuwa ikitekeleza miradi yake kwa kushirikiana na taasisi za Poul Due Jensen Foundation, Grundfos Corporation, UNHCR, Wizara ya Maji na Wizara ya Mambo ya Ndani, kuhakikisha kambi za wakimbizi Tanzania zinakuwa na uhakika wa kupata maji salama. 

 Mbali na miradi ya maji kwenye kambi za wakimbizi mkoani Kigoma, Tanzania, Water mission Tanzania, imetekeleza miradi ya maji ipatayo 24 katika maeneo mbalimbali ya vijijini nchini yenye changamoto ya kupata maji safi, tangu ilipoanza kutoa huduma zake nchini mnamo mwaka 2014.

 Hadi leo hii, wenyeji 30,000 wa Zeze, Kasanda, Kakonko, Heru Ushingo, Mvugwe na Kazilamihunda-Juhudi wanapata maji safi na salama. 

Katika siku zijazo, Water Mission Tanzania na washirika wake wanatumai kuwahudumia hadi watu 80,000 katika jamii zinazozunguka kambi nchini Tanzania kwa kujenga miradi ya maji safi na salama. 

 Akiongea wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi wa maji wenye uwezo wa KW 100 kupitia nguvu ya jua katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu mkoani Kigoma, Balozi wa Denmark nchini, Mette Nørgaard Dissing-Spandet, amepongeza mpango huu wa ushirikiano wa mashirika yasiyo ya serikali na Serikali katika kukabiliana na changamoto katika jamii kama kufanikisha miradi ya kusaidia jamii kama miradi ya maji . 

 Mkurugenzi Mkuu wa taasisi ya The Grundfos Foundation (Poul Due Jensen Foundation), Kim Nøhr Skibsted amesema, mradi huu ulianza kufanyiwa kazi mwaka 2016 wakati taasisi za Grundfos Foundation na Water Mission zilipo dhamiria kuondoa miundo mbinu ya mradi wa zamani uliokuwepo na kujenga mradi unaotumia teknolojia za kisasa na umeme wa jua, lengo likiwa ni kuwapatia maji safi na salama maelfu ya wakimbizi kwenye kambi ya Nyarugusu na maeneo ya vijiji jirani. 

Skibsted, aliongeza kusema kuwa mradi huu ni wa pekee miongoni mwa miradi ya maji iliyotekelezwa na taasisi hiyo kwa kuwa mbali na kuwezesha jamii kupata maji safi zinawezeshwa kupata maarifa ya kutunza mradi na matumizi ya nishati mbadala kuendesha miundombinu yake

 “Mfumo wa ushirikiano wa wadau kufanikisha miradi kwa maeneo yenye mahitaji unapaswa kutumika sehemu mbalimbali duniani kama ambavyo wadau mbalimbali wameshirikiana kuhakikisha eneo hili la wakimbizi wanapata maji salama na kuondoa hatari ya milipuko ya magonjwa yatokanayo na ukosefu wa maji salama”,alisisitiza. 

Naye Makamu wa Rais wa miradi ya kimataifa kutoka Water Mission International, Bw. Seth Womble, amesema kuwa kufanikisha kwa miradi ya maji katika makambi ya wakimbizi kumewaongezea kujiamini katika utekelezaji katika maeneo mengine nchini na kanda nzima. 

“Ushirikiano wetu na wadau wengine unadhihirisha jinsi unavyoweza kufanikisha miradi kwenye maeneo mengine yenye changamoto maji salama kama ilivyo dira ya shirika la Water Mission”.
Share:

KAMPUNI YA AGGREY & CLIFFORD YANG’ARA TUZO ZA TOP 100 MID-SIZED COMPANIES


Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Kampuni ya Aggrey & Clifford, Ibrahim Kyaruzi, akipokea tuzo kwa niaba ya kampuni kutoka kwa Mkurugenzi wa kampuni ya Bankable Tanzania Limited Lawrence Mafuru (Kushoto).

Kampuni ya matangazo na ukuzaji masoko ya Aggrey & Clifford, kwa mara nyingine imepata tuzo kutokana na kuwa miongoni mwa makampuni 100 ya kati yanayofanya vizuri kibiashara.

Kampuni ya Aggrey & Clifford ambayo hivi karibuni ilisherehekea miaka kumi tangu kuanzishwa kwake, ilitunukiwa tuzo hiyo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam kwenye hafla fupi iliyofanyika Serena Hotel.

Share:

UVCCM: Wanaosaka Ubunge Kwa Njia Ya Rushwa Kukiona Cha Mtema Kuni

NA FREDY MGUNDA,IRINGA.
MWENYEKITI wa umoja wa vijana wa ccm (UVCCM) mkoa wa Iringa Kenani Kiongosi amewataka wanasiasa mbalimbali wanaousaka ubunge wa jimbo la Iringa Mjini  kufuata misingi ya chama ili wapite kwenye kanuni na taratibu za chama.

Akizungumza na viongozi wa UVCCM mkoa wa Iringa Kihongosi alisema kuwa viongozi wote wanaoutafuta ubunge katika jimbo la Iringa mjini wanatakiwa kufuata utaratibu unatakiwa na chama cha mapinduzi ili kumpata kiongozi bora.

“Katika kipindi cha miaka kumi sasa tumekuwa tukipoteza jimbolaIringa mjini kwa kuwa na makundi kutokana na viongozi warafi na waroho wa madaraka kwakutoa rushwa kwa wapiga kura ili waweze kupata ubunge,kwa sasa hatuwezi kukubali swala hilo kwa kuwa tunahujumiwa kutokana na makundi ambayo yamekuwa yakitokeza kipindi cha uchaguzi” alisema Kihongosi

Kihongosi alisema kuwa kumekuwa na viongozi wanaoutaka ubunge Iringa Mjini wameanza kufanya kazi wanavyojitakia wao bilakufuata njia sahihi ambazo zinatakiwa,badala yake wamekuwawakitoa fedha kwa baadhi ya wadau kwa lengo la kutengeneza makundi ambayo hayana faida kwa wananchi wa Manispaa ya Iringa.

Aidha Kihongosi aliwataka vijana wa chama cha mapinduzi kukataa mara moja kutumika kuwa daraja kuwatafutia ubunge viongozi ambao hawana msaada katika jumuiya katika kuleta maendeleo kwa vijana ambao ndio wamekuwa wakitumia kuleta ushindi kwamgombea wa chama cha mapinduzi.

“Vijana acheni mara moja kutumika kwa viongozi wasaka tonge ambao wamekuwa wakipata madaraka hawakumbuki mchango wa vijana wakati wa kukitafuta cheo chake”alisema Kihongosi

Kihongosi alisema mwaka 2015 kulikuwa namakundi makubwa mawili ambayo yalikuwa katika ya wenyeviti na makatibu na kupelekea kupoteza jimbo la Iringa Mjini na kulikuwa na mvurugano mkubwa kweli ambao ulimpa tena ubunge Mchungaji Petter Msigwa.

“Nitasikitika sana kuona kijana mmoja ambaye ni kiongozi kumbeba mgombea furani,nikikutambua mapema nitakupeleka kwenye kamati husika na tutakuondoa kwenye nafasi ambayo uponayo hivi sasa ili usituvuruge kwenye harakati zetu za kulikomboa jimbo la Iringa Mjini” alisema Kihongosi


Share:

HALMASHAURI YA NGARA KUKARABATI KITUO CHA AFYA RUKOLE KILICHOKUWA KINATUMIWA NA WAKIMBIZI


Na Ashura Jumapili,Ngara 
Halmashauri ya Wilaya ya Ngara mkoani Kagera imetenga kiasi cha shilingi milioni 600 kwa ajili ya kujenga upya kituo cha Afya cha Rukole kilichopo kata Kasulo kilichokuwa kinatumiwa na Wakimbikizi kabla ya kuharibika.


Kauli hiyo  ilitolewa na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri  ya Ngara Aidan Bahama,wakati akiongea na waandishi wa habari wilayani humo  Oktoba 27 mwaka huu.

Bahama alisema awali kituo kilikuwa kinatumiwa  na wakimbizi  waliokuwa wanaishi kambi ya Rukole kata ya Kasulo kabla ya kurudi kwao.

Alisema majengo hayo yalikuwa yamejengwa kwa udongo  na nyumba chache ndiyo zilikuwa za kudumu na kutokana na majengo hayo kujengwa  kwa tope  pia  yalikuwa  yameharibika.

Alisema majengo yaliyokuwa yameharibika katika kituo hicho ni pamoja na jengo la wagonjwa wa nje  (OPD ),chumba cha kuhifadhia maiti ( Mochwari )na hapakuwa  na chumba cha upasuaji (Theather).

Alieleza kuwa kiasi cha shilingi milioni 600 kimetolewa  kwa ajili ya kujenga kituo hicho upya  lengo likiwa ni kunusuru vifo vya mama na mtoto wilayani humo.

Alisema majengo yatakayojengwa kwa sasa  ni jengo la wagonjwa wa nje (OPD ),Chumba  cha upasuaji (Theather ),chumba cha kuhifadhia maiti (Mochwari )maabara na nyumba moja  ya watumishi.

Alisema kituo hicho kitakapokamilika kitakuwa miongoni  mwa vituo bora ambacho kitatoa huduma zote muhimu ikiwemo upasuaji.

“Tunamshukuru mheshimiwa Rais John Magufuli,ambaye amekuwa akituletea fedha na hizi milioni 600 ni miongoni mwa shilingi karibia bilioni 10 ambazo zimeletwa wilayani Ngara kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo”alisema mkurugenzi huyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Ngara Aidan Bahama
Shughuli za ujenzi wa kituo cha Afya Rukore zikiendelea
Share:

Muungano wa Tigo na Zantel unavyokusudia kuboresha soko la mawasiliano nchini

Sekta ya mawasiliano ya simu za mkononi imekua kwa kiasi kikubwa sana katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.

Katika kipindi hiki cha ukuaji huu makampuni ya simu yametanua wigo wa huduma na matumizi ya simu za mkononi imekuwa sehemu muhimu ya maisha ya kila siku kwa mamilioni ya Watanzania tofauti na zamani ambapo simu ilikuwa kama anasa na ni wachache tu waliweza kuwa nazo. Maendeleo haya yanazidi kukua siku hadi siku kutokana na kuongezeka kwa ubunifu katika teknolojia. 

Simu ya mkononi sasa imebadilika na kuwa si tu kifaa cha kupiga, kupokea na kutuma meseji baina ya watumiaji lakini pia imeleta mapinduzi katika namna tunavyoweka akiba ya fedha, kulipana, kulipa bili mbalimbali na kuendesha maisha yetu ya kila siku.  
 
Mfano wa namna ambavyo simu za mkononi zimebadili maisha yetu ni kampuni ya Tigo Tanzania. Mfumo wa Tigo Pesa wa kutuma na kupokea pesa unatupa nafasi ya kutumiana na kupokea pesa bila haja ya kwenda na kupanga foleni benki.

Vivyo hivyo wenye maduka na biashara mbalimbali nao wametengenezewa mfumo wa Tigo Pesa Merchant ambao unawapa uwezo wa kupokea malipo kutoka wateja wote wa Tigo Pesa ambao kwa sasa ni zaidi ya watu milioni 16.   

Tigo Tanzania pia ni moja ya makampuni yanayoongoza kwa kutoa huduma ya 4G ambayo ni teknolojia yenye ina kasi zaidi katika mawasiliano nchini.

 Huduma hii inakupa uhakika wa kutazama vitu kama videos mtandaoni bila wasiwasi wa kukwama kwama au hata kufanya mikutano kwa njia ya video (conferencing)

Hata hivyo katika siku za karibuni umekuwepo wasiwasi kwamba sekta ya mawasiliano ya simu za mkononi imejaa watoa huduma ambao wengi hawana tija na wasiolipa soko afya katika kuhudumia wateja.

Hali hii inaelezwa kuleta changamoto kwa ubunifu na utoaji huduma wenye tija na viwango bora kwa wateja. 

Katika sekta nyingi za uchumi uwepo wa watoa huduma wengi huwa ni faida kwa mteja. Bahati mbaya ukweli huu haupo kwenye sekta ya mawasiliano ya simu za mkononi. 

Utafiti unaonyesha kuwa kupunguza idadi ya watoa huduma katika sekta ya mawasiliano ya simu za mkononi huwezesha makampuni machache yalipo sokoni kuongeza faida ambayo huwawezesha kuwekeza zaidi katika mitambo na teknolojia yenye kutoa huduma bora zaidi kwa wateja wake. 

Katika soko la Tanzania, siku za karibuni zimekuwepo hatua mbalimbali za kibiashara kupunguza watoa huduma ili kuongeza uwekezaji kwenye teknolojia na ubora wa huduma kwa wateja.

Makampuni mawili ya Tigo Tanzania na Zantel yamekuwa na mjadala kuungana. 

Hatua hii ya Tigo Tanzania na Zantel kuungana ni habari njema sana kwa wateja wa Zantel. Maana yake ni kwamba sasa wateja hao wa Zantel wataweza kufurahia huduma zote ambazo sasa wateja wa Tigo Tanzania wanazipata.

Muungano huo pia utasaidia sekta ya mawasiliano ya simu za mkononi nchini kuendelea kuwa bunifu na kutoa huduma bora kwa mamilioni ya wateja wake nchi nzima.


Share:

Heri Ya Kuzaliwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr John Pombe Magufuli

Leo Oktoba 29, 2019, Rais Magufuli anasherehekea kumbukizi ya siku yake ya kuzaliwa. 

Rais Magufuli alizaliwa tarehe kama ya leo Oktoba 29, 1959 na ametimiza miaka 60, tunamtakia afya njema na Mungu azidi kumuongoza katika majukumu yake.


Share:

Mkuchika Asema Wanaowahamisha Watumishi Vituo Vya Kazi Kabla Hawajathibitishwa Atawashughulikia.

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Kepteni George  Mkuchika amesema atawashughulikia wale wote anaohamisha watumishi vituo vya kazi kabla hawajathibitisha kwani ndio wanaochangia kuwepo kwa changamoto ya baadhi ya Mikoa kuwa na upungufu wa watumishi.

Akizungumza Jijini hapa jana wakati akizindua Baraza Kuu la nne la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma Kepteni Mkuchika amewataka utumishi wa Umma kutambua kuwa kila wakati wanapaswa kuwa tayari kufanya kazi mahali popote kwa ajili ya kuwatumikia wananchi.

Amesema katika ziara yake Mikoani amegundua Mikoa ya pembezoni ina uhaba mkubwa wa watumishi, akitolea mfano Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma ambayo ina watumishi chini ya asilimia 50.

Kuhusu suala la Rushwa, amesema taasisi zilizopo chini ya Ofisi Rais zinatakiwa kuwa kioo katika kukema vitendo vya rushwa, kwani Ofisi hiyo ndio inayoshughulikia wasiowaadilifu na si kujihusisha na vitendo hivyo.

Kwa pande wake Makamu Mwenyekiti wa Baraza hilo Leah Ulaya amesema watumishi wa Umma wanajua kazi kubwa inayofanywa na Rais katika kuleta maendeleo kwa wananchi hivyo wataendelea kufanyakazi kwa weledi na uadilifu ili kuunga mkoni juhudi za Seriali.

Kuhusu malalamiko yaliyopo kwa watumishi wanaopandishwa madaraja lakini kiwango cha mshahara hakibadiliki,Wizara hiyo amewahakikishia kuwa suala hili litapatiwa ufumbuzi haraka iwezekanavyo, huku ikimesema kuondolewa kwa watumishi 19,708 waliobainika kuwa na  vyeti vya kughushi kupitia zoezi la uhakiki kumeifanya Serikali kuokoa kiasi cha Sh 19.838 bilioni.
Mwisho.



Share:

Wanawake Washauriwa Kujitokeza Na Kuogombea Nafasi Mbalimbali Za Uongozi

Wanawake Mkoani Kagera wametakiwa kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajia kufanyika mnamo septemba 24 mwaka huu.
 
Hayo yamebainishwa na Mbunge wa viti maalumu kutoka Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Mh Conchester Rwamulaza wakati akiongea na mpekuzi blog kuelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mapema mwaka huu.
 
Mh Conchester amesema kuwa wanawake wengi wamekuwa na hofu ya kutotaka kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na kuongeza kuwa wanayo nafasi kubwa yakuweza kugombea nafasi za uongozi kwa mwaka huu  kwa ajili ya maedeleo ya nchi kwa kuwa wana kauli mbiu ya wanawake wanaweza na kusema kuwa isiwe kauli ya maneno bali ata kwa vitendo.
 
Amesema kuwa ushindani wa mwaka huu ni mkubwa na watu wengi wana mwamuko wa kugombea kwa ajili ya maendeleo ya nchi na kuongeza kuwa uongozi unaanzia chini katika ngazi ya vitongoji na vijiji kwa kuwa viongozi hao wanakuwa karibu na wananchi.
 
Aidha Mh Conchester ameongeza kuwa wananchi wajitokeze  kwa wingi mnamo septemba 24 mwaka huu kuweza kupiga kura huku wakitambua umuhimu wa uchaguzi huo na akiwataka wananchi kutobeza uchaguzi huo kwa kuwa ni muhimu sana.
 
Pia mh Conshester amesema kuwa  ili jambo la wanawake kujitokeza kugombea nafasi mbali mbali lifanikiwe inabidi akina baba kutowakataza wanawake  kugombea katika uchaguzi huo ili waweze kutimiza malengo yao.




Share:

Uzalishaji Makaa Ya Mawe Waongezeka Nchini

Na Asteria Muhozya
Imeelezwa kuwa, wastani wa uzalishaji wa Makaa wa Mawe nchini umekuwa ukiongezeka tofauti na ilivyokuwa  awali huku sababu kadhaa zikichangia ongezeko la uzalishaji huo ikiwemo mazingira mazuri ya uwekezaji, zuio la  Serikali kuingiza makaa ya mawe kutoka nje, ongezeko la viwanda vinavyotumia makaa ya mawe na  kuboreshwa kwa mundombinu ya usafirishaji. 
 
Hayo yamebainishwa na Kamishna wa Madini Mhandisi David Mulabwa wakati akiwasilisha kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu  hatua zilizofikiwa katika  uendelezaji wa miradi ya makaa ya mawe kwa niaba ya Waziri wa Madini.
 
Mhandisi Mulabwa amesema katika kipindi cha miaka 8 kuanzia mwaka 2011 hadi 2018, uzalishaji uliongezeka kutoka tani 81,384.67 mwaka 2011 na kufikia  627, 651.00 mwaka 2018, ikiwa ni  wastani wa takribani tani 52,304.25 kwa mwezi.
 
‘’ Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha miezi 9 kwa mwaka 2019, uzalishaji  uliongezeka  hadi kufikia tani 543,621.39 ikiwa ni wastani wa tani 60,402.38 kwa mwezi,’’ amesema Mhandisi Mulabwa.
 
Ameongeza kuwa, pamoja na ongezeko la uzalishaji huo, bado ni mdogo ikilinganishwa na kiasi cha makaa ya mawe kinachokadiriwa kuwepo nchini. Amesema Tanzania inakadiriwa kuwa na mashapo ya makaa ya mawe  yanayofikia tani bilioni 1.9 na yaliyothibitishwa ni tani bilioni 1.4 huku ikitajwa kuwa nchi yenye akiba kubwa ya makaa hayo  kwa nchi za Afrika Mashariki.
 
‘’ Mheshimiwa Mwenyekiti akiba kubwa zaidi kwa sasa inapatikana katika bonde la Mchuchuma ambapo kuna akiba ya zaidi ya tani milioni 400,’’ amesema Mhandisi Mulabwa.
 
Akizungumzia  mwenendo wa mauzo amesema kipindi cha kuanzia  mwezi Julai, 2018 hadi  Juni, 2019 kiasi cha makaa ya mawe kilichozalishwa na kuuzwa  ni tani 799,628.41 zenye thamani ya shilingi 102,922,127,876.61. Ameongeza kati ya kiasi hicho kilichozalishwa, tani 421,400.07 ziliuzwa nchini na tani 378,2228.34 ziliuzwa katika masoko ya  nje ya nchi
 
Ameeleza kutokana na mauzo hayo, Serikali ilipata kiasi cha  shilingi 4, 116,885, 115.06 , ambapo shilingi 3,087,663,836. 30 ni mapato yatokanayo na mrabaha na  shilingi 1,029,221,278.77 ni mapato yatkanayo na ada ya ukaguzi.kipindi cha kuanzia mwezi Julai.
 
Kuhusu uzalishaji wa makaa ya mawe kwa mwaka wa fedha 2019/20, kuanzia mwezi Julai 2019 hadi Septemba 2019 amesema  kiasi kilichozalishwa katika migodi yote ni tani 157,341 zenye thamani ya shilingi 16,691,662,474. 
 
‘’ Mhe. Mwenyekiti kutokana na mauzo hayo serikali ilikusanya mapato ya shilingi 949,834,017.71 ambapo shilingi  807,074,032.73 ni mapato yatokanayo na malipo ya mrabaha na shilingi 142,759,984.98 ni mapato yaliyotokana na ada ya ukaguzi.
 
Akizungumzia hatua zilizochukuliwa na serikali kuendeleza miradi ya makaa ya mawe amesema kuwa ni pamoja na kuendelea kuhamasisha uanzishwaji wa Viwanda mbalimbali ili kujenga uchumi wa viwanda; kuendelea kusimamia tafiti maeneo mbalimbali ili kupata taarifa sahihi za kiasi cha mashapo na ubora wa makaa ya mawe nchini; wizara kwa kushirikiana na taasisi nyingine za serikali imeendelea kuboresha mazingira ya biashara katika sekta ya makaa ya mawe; serikali imeendelea kufuatilia uanzishwaji wa miradi ya makaa ya mawe ya Mchuchuma na Liganga na kuendelea kuweka zuio la uingizwaji   wa makaa ya mawe kutoka nje ya nchi ili kuongeza biashara ya makaa ya mawe yanayozalishwa nchini.
 
Aidha, ameyataja baadhi ya mafanikio kuwa ni pamoja na kuongeza kwa matumizi ya makaa ya mawe yanayozalishwa nchini kufuatia zuio la uingizaji wa makaa ya mawe kutoka nje,  kuongezeka kwa kiasi cha makaa ya mawe yanayozalishwa hapa nchini kutoka wastani wa tani 81,384.67 kwa mwaka 2011 hadi kufikia tani 627,651.00 mwaka 2018 kutokana na ongezeko la watumiaji wa ndani.
 
Pia, ameyataja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na  kuongezeka kwa biashara ya makaa ya mawe ndani  na nje ya nchi, ambapo watumiaji wa nishati ya makaa ya mawe wameendelea kuongezeka kutokana na upatikanaji wake, kuongezeka kwa mapato ya serikali kutokana na uuzaji wa makaa ya mawe na kuongezeka kwa ajira kutokana na shughuli za uchimbaji wa makaa ya mawe ambapo hadi kufikia Septemba 2019, takribani watu 500 wameajiriwa katika migodi mbalimbali  ya uchimbaji wa makaa ya mawe.
 
Kwa upande wa Kamati ya Bunge baada ya kupkea taarifa hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dustan Kitandula imeitaka wizara kuweka msukumo mkubwa wa uanzishwaji wa miradi ya Linganga na Mchuchuma pamoja na mradi wa Kiwira kutokana na manufaa yake kiuchumi. 
 
Akijbu hatua zilizochukuliwa na wizara, Waziri wa Madini Doto Biteko amesema tayari wizara kwa upande wake imekwishafanya masuala yote yanayohitaji msukumo wa wizara katika miradi husika huku mengine yakisimamiwa na mamlaka nyingine hata hivyo ameeleza kuwa serikali inaendelea kuyafanyia kazi ili kuwezesha miradi hiyo kutekelezwa.
 
Naye, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo ameileza Kamati hiyo kuhusu hatua kadhaa zilizochukuliwa na wizara katika kuboresha miundombinu ya barabara katika maeneo ya uchimbaji wa makaa ikiwemo ya kilomita 8 kutoka Kiwira mpaka Kabulo na kueleza kuwa, tayari serikali imekwisha tenga shilingi Bilioni 2 kwa ajili ya ujenzi wa barabara na shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa daraja. 
 
Vikao kati ya  Kamati, Wizara na taasisi zake vimeanza Oktoba 28, 2019 na vinatarajiwa kuhitimishwa Novemba 1,2019.


Share:

Umoja wa Ulaya waurefusha tena muda wa Brexit

Umoja wa Ulaya umekubali  kuchelewesha kwa muda wa miezi mitatu Uingereza kujitoa kutoka Umoja huo hadi Januari 31.

Kiasi siku tatu kabla ya tarehe ya mwisho ya Uingereza kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya hapo Oktoba 31, mchakato wa Brexit bado haujulikani mwelekeo wake wakati wanasiasa wa Uingereza hawako karibu ya kufikia muafaka juu ya vipi, lini na hata iwapo hatua ya kuachana na Umoja wa Ulaya itawezekana.

Mataifa 27 ya Umoja wa Ulaya yanamefikia makubaliano kuchelewesha Brexit hadi Januari 31, pamoja na uwezekano wa Uingereza kujitoa mapema iwapo bunge la Uingereza litaidhinisha makubaliano ya kujitoa.


Share:

Mwakyembe: Ni heshima kutembelewa na Miss World 2018

Na Eleuteri Mangi, WHUSM, Arusha
Ni heshima kubwa kwa Tanzania kutembelewa na Mwenyekiti na Mwendeshaji wa Shindano la Miss World Bi Julia Morley pamoja na Mshindi wa Miss World 2018 Vanessa Ponce.
 
Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe wakati wa uzinduzi wa taulo za kike zinazojulikana kama Uhurupads uliofanyika leo katika shule ya sekondari Moshono iliyopo jijini Arusha.
 
“Ujio wao leo hapa Arusha, ni heshima kwa taifa. Katika mataifa yote duniani, wameichagua Tanzania, hii ni heshima kubwa na wametuletea zawadi ya Uhurupads ambazo zitawaweka huru watoto wetu katika kutimiza ndoto zao hasa wanapokuwa shuleni” amesema Waziri Dkt. Mwakyembe.

Aidha, Waziri Dkt. Mwakyembe amesema kuwa bidhaa ya taulo hizo alizozindulia  ni rafiki kwa mazingira kwa kuwa zinaweza kutunzwa mahali popote na zisiwe na madhara kwenye mazingira kwa kuwa haina  mchanganyiko wowote wa plastiki. Taulo hizo zinazotengenezwa na kikundi cha wanawake 12 kiachojulikana kama timu ya Uhuru Kit Ltd ambao wanaunga mkono juhudi za Serikali katika kutunza mazingira kwa marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki nchini Julai, 2019.
 
Katika kuhakikisha Tanzania inatumia vema fursa ya ujio wa Mshindi wa Miss World 2018 Vanessa Ponce wa Mexico, Dkt. Mwakyembe amesema kuwa Serikali itaandaa ziara maalum kwa Uongozi wa Miss World ukiongozwa na Mwenyekiti na Mwendeshaji wa Shindano la Miss World Bi Julia Morley kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini ikiwemo mbuga za Serengeti, hifadhi ya Ngorongoro pamoja na mji wa kihistoria wa Zanzibar.
 
“Uwepo wa Miss World 2018 Vanessa Ponce, dunia nzima macho yao yapo hapa nchini, ni vema kuitangaza nchi yetu kimataifa kupitia ujio wake” amesema Waziri Dkt. Mwakyembe.

Kwa upande wake Mwenyekiti na Mwendeshaji wa Shindano la Miss World Bi Julia Morley amesema kuwa amefurahishwa na hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania ambapo ni mara ya kwanza kwake kuja nchini.
 
“Nimefurahi sana Tanzania ni nchi nzuri, nilipopanda ndege kuja hapa nilipata matangazo yanayosisitiza marufuku ya kutumia mifuko ya plastiki, Serikali imefanya vizuri kujali kutunza mazingira” alisema Bi Julia Morley.

Nao Miss World 2018 Vanessa Ponce kutoka Mexico pamoja na Miss Tanzania 2019 Sylivia Sebastian wamesema kuwa urembo ni heshima, UhuruPads zitawasaidia wasichana kupata elimu wakiwa huru wakizingatia kauli mbiu ya ‘Uzuri wenye malengo.’ 
 
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Mwenyekiti na Mwendeshaji wa shindano la Miss World Bi Julia Morley, Mshindi wa Miss World 2018 Vanessa Ponce kutoka Mexico, Mshindi wa Miss Tanzania 2019 Sylivia Sebastian Bebastian Bebwa pamoja, mwandaaji wa Mashindano ya Miss Tanzania Bi. Basilla Mwanukuzi pamoja na walimu na wanafunzi wa shule ya sekondari Moshono ya jijini Arusha.



Share:

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumanne October 29






















Share:

Monday 28 October 2019

Waitara Amewaomba Wananchi Kuchagua Viongozi Wenye Hofu Ya Mungu

Na Paschal Dotto-MAELEZO.
Katika kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao utafanyika nchi nzima Novemba 24, 2019, Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mwita Waitara amewaomba viongozi wa Dini kuwahamsisha wananchi kuchagua viongozi weneye Mungu.

Akizungumza katika Mkutano wa Kujadili namna Taasisi za Dini zinzvyochangia Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam, Mhe. Waitara amesema kuwa ni muhimu kuwachagua viongozi wenye hofu ya Mungu na waadilifu kwa wananchi ili kuiunganisha Serikali katika kuleta maendeleo kwa wananchi.

“Viongozi wa Dini nyie mnahubiri amani na haki, watu wakipata haki maana yake nchi inatulia, kwa hiyo hakikisheni mnawahubiria watu wenu kuhusu kuchagua viongozi walio na hofu ya Mungu ambao pia ni waadilifu kwa wananchi ili kuondoa migogoro mbalimbali ambayo imekuwa ikisababishwa na viongozi wala rushwa kwenye mitaa yetu ikiwemo ile ya ardhi”, ameeleza Mhe.Waitara.

Waziri Waitara alisema kuwa viongozi waadilifu huwa wanawajibika bila shida yeyote, kwa hiyo ni muhimu kuunganisha juhudi za Mhe. Rais John Pombe Magufuli kwa wananchi kwani uwajibikaji wake ni mkubwa katika kuwaletea maendeleo wananchi.

Alianisha sifa nzuri za kiongozi kuwa ni yule mwenye maono, maamuzi sahihi, anayesimamia maono na maamuzi yake, sifa ambazo Rais Magufuli anazo, kwa hiyo ili kuendelea kuleta maendeleo ni lazima viongozi wa Serikali za Mitaa ambako maendeleo yaanzia wawe waadilifu na wenye hofu ya mungu.

Waziri Waitara alisema kuwa mpaka Oktoba 17, 2019 wananchi milioni 19,686,000 walikuwa wamejiandikisha, sawa na asilimia 86 ikilinganishwa na mwaka 2014 ambapo wananchi Milioni 11 walijiandikisha sawa na asilimia 63.

Aidha Waitara alisema kuwa katika hatua za uchaguzi huo wagombea wataanza kuchukua fomu za kugombea kuanzia oktoba 29, 2019 na kwamba itakapofika Novemba 5, 2019 wasimamizi wa Uchaguzi watabadika majina ya wagombea kwa hiyo viongozi wa dini wanatakiwa kuwasaidia wananchi kujua kiongozi mwadilifu na pia kusali kwa ajili ya kupata kiongozi bora katika mitaa mbalimbali nchini.

Waziri Waitara alisema kuanzia Novemba 17 hadi 23, 2019, itakuwa ni muda wa kampeni ambapo amewataka wagombea kuomba kura kwa kujenga hoja kwa wananchi na kuwataka Wakuu wa Mikoa na Viongozi wa Dini kusimamia kikamilifu suala ya amani wakati wa kampeni.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema kuwa watu wanatakiwa kubadilika na kufuata kasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wasaidizi wake kwani wanakimbizana kuwaletea maendeleo wananchi.

“Kuna watu bado hajabadilika na hawataki kubadilika, lakini ukiangalia makusudi ya Rais wetu, Makamu wake, Waziri Mkuu na Mawaziri wanakimbizana kuleta matokeo kwa wananchi, lakini huku chini ni shida kidogo, kwa hiyo nawaomba viongozi wetu wa Dini tuwahamasishe wananchi wetu Novemba 24, 2019 wajitokeze kuwachagua Wenyeviti wa Serikali za Mitaa wenye hofu ya Mungu”, alieleza Makonda.
 


Share:

Zoezi La Kuchukua Na Kurejesha Fomu Za Kugombea Uchaguzi Serikali Za Mitaa Kuanza Kesho 0ktoba 29,2019

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Seleman Jafo ametangaza siku maalum ya Uchukuaji wa Fomu za Kuwania uongozi Serikali za Mitaa kuwa ni kuanzia Kesho Oktoba,29,2019 .
 
Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba ,28,2019 Jijini Dodoma ,Mhe.Jafo amesema zoezi la uchukuaji wa fomu hizo  pamoja na kuzirudisha litadumu kwa muda wa siku saba kuanzia Oktoba 29,2019 hadi Novemba 4,2019.
 
Hivyo Waziri Jafo amesema muda huo ni Muafaka kwa wagombea mbalimbali kuchukua fomu  na kurudisha ndani ya Muda husika kama ilivyopangwa.

Aidha,Waziri  Jafo amewataka wakuu wa wilaya na wakuu wamikoa kote nchini kuhakikisha wanasimamia suala la ulinzi ,usalama na amani katika zoezi hilo.
 
Fomu hizo zitatolewa katika ofisi za wasimamizi  Wa Uchaguzi ambao ni watendaji wa mitaa na  vijiji.

Hata hivyo,Waziri Jafo amesema nafasi mbalimbali zimezibwa pale ambapo pako wazi   kwa watendaji wa Mitaa na wapo watumishi wa umma wamekaimu nafasi hizo.

Ikumbukwe kuwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unatarajia kufanyika Novemba ,24,2019.


Share:

Rais Magufuli apokea hati za utambulisho za Mabalozi wa Umoja wa Ulaya, Finland na Rwanda. Ikulu Jijini Dar es Salaam.




Share:

Hatima Ya Wanafunzi Wanaotuhumiwa Kumuuwa Mwanafunzi Mwenzao Yaanza Kuonekana

Na Silvia Mchuruza,Bukoba.
KESI ya mauaji inayowakabili wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Katoro Islamic ya mkoani Kagera wanaotuhumiwa katika mauaji ya mwanafunzi mwenzao, Mudy Muswadiku imeharishwa hadi Novemba 11 mwaka huu kutokana na upelelezi kutokamilika.

Kesi hiyo ya mauaji namba 18/2019 inayosikilizwa na Hakimu Frola Kaijage imetajwa tena leo (jana) katika Mahakama ya Wilaya Bukoba mkoani Kagera ambapo Wakili wa Serikali, Juma Mahona amesema upelelezi wa kesi hiyo unakaribia mwishoni.

Mahona alisema watuhumiwa hao wakiwa gerezani hivi karibuni walitembelewa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa (RCO) ambapo alisema shauri la watuhumiwa hao liko katika hatua ya mwisho.

“Kwa utaratibu wa makosa ya namna hii RCO anapokamilisha upande wake analeta jarada kwetu na likishafika kwetu tunalipitia ili kuandaa nyaraka kwa ajili ya kupeleka shauri hilo Mahakama Kuu.

Hivyo tumewaambia watuhumiwa wawe wavumilivu, taratibu hizo zitakapokamilika tutawajulisha na kupeleka nyaraka Mahakama Kuu na zikitoka Mahakama Kuu na kurudi Mahakama ya Wilaya hapo ndipo upelelezi utakuwa umekamilika,” Alieleza Mahona.

Kwa upande wa watuhumiwa waliokuwa wakisoma kidato cha nne kufanya mitihani wa Taifa unaotarajia kuanza Novemba 4 mwaka huu, Mahona amesema hawezi kuzungumzia suala hilo maana watuhumiwa waliiomba Mahakama iwaruhusu kufanya mtihani huo.

“Waliiomba Mahakama hivyo wa kulizungumzia suala hilo ni Mahakama yenyewe,” alisema.

Watuhumiwa katika kesi hiyo ya mauaji ya mwanafunzi Mudy aliyekuwa anasoma kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Katoro Islamic ya mkoani Kagera ni wanafunzi Sharifu Amri (19), Fahadi Abdulazizi Kamaga (20), Husama Ramadhan (17), Sharifu Huled (19), Abdalah Juma (19) na Hussein Mussa (20), Majaliwa Abud (35) mwalimu na Badru Issa Tibagililwa (27) mlinzi.

Kesi hiyo imehairishwa hadi Novemba 11 mwaka huu ambapo pia itatajwa tena kwani Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shitaka hilo na watuhumiwa wamerudishwa rumande hadi siku kesi itakapotajwa tena.

Mauji hayo yalitokea Aprili 14 mwaka katika shule ya sekondari ya Katoro Islamic iliyoko katika Halmashauri ya Bukoba Vijijini mkoani Kagera.


Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger