Monday 2 September 2019

MAHAMUDU AWAOMBA VIONGOZI WA DINI KUENDELEA KUHIMIZA AMANI

 Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Kagera Hamimu Mahamudu  
Na Lydia Lugakila - Malunde 1 blog

Viongozi wa madhehebu ya dini mkoani Kagera wameombwa kuendelea kuhimiza amani kwa waumini wao ili kuwa na ustaarabu wa kumjua Mungu ikiwemo kuishi na watu vizuri na kuwaombea viongozi wa nchi.

Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 2, 2019 na Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Kagera Hamimu Mahamudu  katika hafla ya kuMpongeza Mzee Twail Ismail Tabilane aliyerejea kutoka Makka Saudi Arabia kuhiji iliyofanyika wilayani Misenyi Mkoani Kagera .

Mahamudu amesema nchi ya Tanzania licha ya kuendelea kuwapokea wageni kutoka sehemu tofauti lakini bado ni kisiwa cha amani hivyo amani ili iendelee kuwepo, lazima viongozi wa dini waelekeze kwa waumini wao ili kusisitiza amani hiyo izidi kutawala.

Amesema amani ni tunu kubwa hivyo ni vyema itunzwe na kuenziwa huku akiwaomba viongozi wa dini ,waumini wamuombee sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Joseph Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya na kutaja kufurahishwa na uamzi wake wa kuwaita watendaji wa kata nchi nzima Ikulu kwa ajili ya mazungumzo ya kuwaletea maendeleo wananchi.

Mahamudu amewataka viongozi wa dini na waumini wao kuwa na ustaarabu wa kumjua Mungu ikiwemo ustaarabu wa kuishi na watu vizuri lakini na kuifanya dunia iwe mahali bora pa kuishi.

"Nimeguswa sana na umoja huu wa waumini wa dini ya kiislamu na wasiokuwa waumini wa dini hii katika matukio mbalimbali hasa ya kidin, hakuna ubaguzi wala hamchagui, umoja huu na ushirikiano huu naomba uendelee amesema’’,amesema.

Katika hatua nyingine Katibu huyo amewahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Share:

SHEIKH TWAHILI ISMAIL TABILANE AREJEA KUTOKA MAKKA KUHIJI...AFANYIWA HAFLA YA MAPOKEZI MISENYI


Na Lydia Lugakila - Malunde1 blog 
Sheikh Twahili Ismail Tabilane (70)  mkazi wa kijiji cha Burembo kata ya Mushasha wilayani Misenyi mkoani Kagera amerejea salama hapa nchini akitokea Mji wa Makka Saudi Arabia katika kutekeleza ibada ya Hija ya dini ya kiislamu.


Akizungumza kwenye hafla ya kupongezwa kutoka katika ibada ya Hijja iliyofanyika Septemba 2, 2019, nyumbani kwake Burembo, Sheikh Ismail ambaye kwa sasa ni Khaji amesema kutokana na Umoja uliopo Makka ikiwemo ushirikiano na upendo ni ishara kuwa kila Muislamu aige na kujifunza.

Ameitaja safari hiyo kuwa  ni ya neema kubwa iliyosababisha yeye kurudi hapa nchini akiwa salama hivyo ametamani tena kurudi nchini makka.

Shekhe huyo amesema kila Muislamu aione habari ya kwenda hija kama ya kawaida na kuwa kila muumini wa dini hiyo atekeleze suala la kufika makka

"Namshukuru Mungu hali niliyoikuta kule Makka ni nzuri natamani kurudi mwaka ujao, hii ni neema kule hakuna cha tajiri wala maskini kule ni haki sawa kwa wote", amesema.

Amesema safari ya kwenda Hija haina ubaguzi kwani hija hiyo inawapa Waislamu wote haki sawa, ikiwemo chakula cha bure, malazi na mahitaji mengineyo muhimu pamoja na kupewa mafunzo ikiwemo kusoma vitabu vya Quran Tukufu vyenye maudhui ya kuiheshimu dini hiyo.

Kwa upande wake Sheikh Mkuu wa mkoa wa Kagera, Haruna Kichwabuta amewahimiza waislamu mkoani Kagera kuendelea kuwa wamoja na kumuomba Mungu ili kila muumini wa dini hiyo aweze kufikia Makka

Hata hivyo Sheikh Kichwabuta ameyashukuru madhehebu tofauti mkoani Kagera yaliyoshiriki kwa kumpokea Sheikh Twail aliyekwenda kuwakilisha dhehebu hilo katika ibada hiyo.

Amewataka Waislamu kujitokeza kwa wingi mwaka ujao 2020 kuudhuria ibada ya Hija. 

Naye Sheikh Mkuu Wilaya ya Misenyi mkoani, Abduzaydi Kyagulani ametoa pongezi kwa shekhe huyo kurejea salama hapa nchini na kuhimiza umoja kwa waumini hao na madhehebu tofauti ikiwemo kuiombea nchi amani 

Amesema Masheikh kutoka Kanyigo,Buyango, Kilimilile, Mtukula,Bugandika , Burembo wote wamerejea kwa usalama bila matatizo ambapo ameongeza kuwa madhumuni mazito ni kujenga nguzo tano za kiislamu sambamba na umoja.

Shekhe wa mkoa wa Kagera Haruna Kichwabuta akimpongeza Shekhe Ismail kwa kurejea kutoka Makka. Picha zote na 
Lydia Lugakila - Malunde1 blog 

Kushoto ni Sheikh Twahili Ismail Tabilane (70)  mkazi wa kijiji cha Burembo kata ya Mushasha wilayani Misenyi mkoani Kagera akizungumza baada ya kurejea kutoka Makka.

Shekhe wa mkoa wa Kagera Haruna Kichwabuta akizungumza wakati wa kumpokea 
Sheikh Twahili Ismail Tabilane  akitokea Makka.

Shekhe wa wilaya ya Misenyi mkoani Kagera Abduzayid Kyagulani akizungumza 
wakati wa kumpokea Sheikh Twahili Ismail Tabilane  akitokea Makka.


Share:

Picha 12 : RAIS MAGUFULI AKIWA NA MAAFISA WATENDAJI WA KATA NCHI NZIMA LEO IKULU


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora) Mhe. George Mkuchika, Rais wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Suleiman Jaffo, Katibu Mkuu Ikulu Dkt. Moses Kusiluka, Katibu Mkuu Utumishi Dkt. Laurian Ndumbaro, Katibu Mkuu TAMISEMI Mhandisi Nyamhanga na Naibu Katibu Mkuu Utumishi Dkt. Francis Michael katika picha ya pamoja na Maafisa Watendaji wa Kata baada ya kukutana na kuzungumza nao Ikulu jijini Dar es salaam leo Septemba 2, 2019. Picha na Ikulu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipata chakula cha mchana na Maafisa Watendaji wa Kata wa nchi nzima baada ya kukutana na kuzungumza nao Ikulu jijini Dar es salaam leo Septemba 2, 2019
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Maafisa Watendaji wa Kata wa nchi nzima wakati wa chakula cha mchana baada ya kukutana na kuzungumza nao Ikulu jijini Dar es salaam leo Septemba 2, 2019
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Maafisa Watendaji wa Kata wa nchi nzima baada ya kukutana na kuzungumza nao Ikulu jijini Dar es salaam leo Septemba 2, 2019
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Maafisa Watendaji wa Kata wa nchi nzima alipokutana nao Ikulu jijini Dar es salaam leo Septemba 2, 2019
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora) Mhe. George Mkuchika, Rais wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Suleiman Jaffo, Katibu Mkuu Ikulu Dkt. Moses Kusiluka, Katibu Mkuu Utumishi Dkt. Laurian Ndumbaro, Katibu Mkuu TAMISEMI Mhandisi Nyamhanga na Naibu Katibu Mkuu Utumishi Dkt. Francis Michael katika picha ya pamoja na Maafisa Watendaji wa Kata wa Mkoa wa Lindi baada ya mkutano wao Ikulu jijini Dar es salaam leo Septemba 2, 2019.
Picha na Ikulu
Share:

AMSHAMBULIA EX BAADA YA KUMNASA AKIPANGA MIPANGO YA KUOLEWA NA BWANA MWINGINE


Mkulima wa Kijiji cha Nangaru, mkoani wa Lindi Abdallah Shaibu Nyuki (30), amehukumiwa na Mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara, kwenda jela miaka 8, baada ya kupatikana na makosa 2 ya kutaka kuuwa bila kukusudia.

Akitoa hukumu hiyo Jaji Mfawidhi Mkuu wa Mahakama hiyo Joel Paul Ngwembe, amesema anamhukumu mshtakiwa kifungo cha miaka 4 kwa kosa la kwanza la kujaribu kuua na miaka 4 tena kwa kosa la kujeruhi.

Awali Mwanasheria wa Serikali, Emmanuel John amesema kuwa mshtakiwa akiwa na panga mkononi Disemba 08, 2018, aliwashambulia Hashimu Bakari Mnocho na Zakia Salum Kindumba, ambaye ni mwanamke aliyeachana naye, baada ya kuwakuta wako pamoja wakizungumzia mipango ya ndoa.

Mwanasheria huyo amesema kuwa baada ya kuwakuta wakiwa wanazungumza mshtakiwa akiwa na panga mkononi aliwajeruhi kwa kuwashambulia mwilini, ambapo baada ya kufanya tukio hilo alikimbia Kijiji cha jirani.
Chanzo- EATV
Share:

ROGATHE AENDELEA KUOMBA MSAADA WA MATIBABU AMALIZIE DOZI...AWASHUKURU WALIOJITOKEZA MWANZO



Muonekano wa ngozi ya Rogathe Kabla ya kuanza kupatiwa huduma ya matibabu


Muonekano wa ngozi ya Rogathe Kabla ya kuanza kupatiwa huduma ya matibabu


Rogathe Cycprian Makala akionesha namna matibabu yalivyomsaidia kutibu ugonjwa wake wa ngozi kwa fedha za wasamaria wema na sasa hawashwi tena kama hapo awali na anaendelea na masomo yake ya Kidato cha Tano.

Rogathe Cycprian Makala (kushoto) akiwa na mama yake Happines Stephen Makala wakitoka kupatiwa matibabu leo Septemba 2,2019, na kuomba msaada wa fedha ili amalizie matibabu kwa miezi sita iliyosalia na kutoa shukrani wa wasamaria ambao walimsaidia awali na kupata matibabu kwa miezi mitatu.

*****
Happiness Stephen ambaye ni mkazi wa mtaa wa Busulwa kata ya Kitangili Manispaa ya Shinyanga anaendelea kuomba msaada fedha za matibabu kwa binti yake aitwaye Rogathe Cycprian Makala (18), ambaye anasumbuliwa na tatizo la ugonjwa wa ngozi kwa muda wa miaka 16 sasa.

Anatoa shukrani kwa wadau ambao awali waliojitokeza kumsaidia fedha za matibabu kwa binti yake ambazo zimetumika kumtibu kwa miezi mitatu na kusalia miezi sita kwani anatakiwa atibiwe kwa muda wa miezi tisa hivyo anaomba wasamaria wema waendelee kumsaidia ili apate kupona.

Anasema kwa matibau ambayo ameyapata binti yake sasa hivi hali yake inaendelea vizuri hajikuni tena usiku kucha kama hapo awali na anaendelea na masomo yake ya kidato cha Tano kama Kawaida.

Awali kabla ya kupatiwa matibabu binti huyo alikuwa halali usiku kucha anashinda anajikuna tu na hata wakati wa jua kali, huku vipele vikimtoka mwili mzima.

Amesema binti yake huyo kwa sasa anapatiwa matibabu na daktari bingwa kutoka apolo india ambaye hua anakuja mkoani shinyanga kila baada ya mwezi, na matibabu yake yatachukua miezi tisa kwa gharama ya shilingi milioni 4,536,000.

Anasema dozi ya dawa ambayo anatumia kila mwezi ni shilingi 504,000/=, ambapo kwa miezi hiyo tisa ni sawa na shilingi 4,536,000/=.

Kwa yeyote atakaye guswa kumsaidia awasiliane kwa namba zifuatazo:

Vodacom : 0764206669 ukitaka kutuma kwa m-pesa jina litasoma Happines Makala

Tigo: 0676368559, jina litasoma Happines Makala (Tigopesa)

Halotel: 0626845953, jina litasoma Eliud Makala (Halopesa)
Share:

RADI YAUA NG'OMBE 22 KIGOMA

Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog Kigoma
Ng'ombe  22 wenye thamani ya shilingi milioni 12 ,wamekufa baada ya kupigwa na radi iliyoambatana na mvua na upepo mkali katika kijiji cha  Kaziramihunda  kata ya Gwanumpu wilayani Kakonko mkoani Kigoma.


Wakizungumzia tukio hilo wamiliki wa ng'ombe hao,akiwemo Abdu Kasungu,wamesema tukio hilo limetokea Septemba 1,2019 majira ya saa kumi na moja jioni wakati vijana waliokuwa wametoka kuwanywesha  maji ng'ombe katika Kijiji cha Msenga lakini wakiwa njiani ulitokea upepo mkali ulioambatana na radi na kuwapiga ng'ombe 22 ambao walikufa papo hapo.

Kasungu amesema kati ya ng'ombe 20 alizokuwanazo amepoteza ng'ombe 16  na kwamba anashukuru Mungu kwa kuwa watu waliokuwa wakiwachunga walibaki salama kwa kuwa imetokea ni bahati mbaya hawana budi kulipokea hilo.

Naye Filbert Chibedese aliyepoteza ng'ombe sita amesema tukio hilo limewasikitisha kwa kuwa litawarudisha nyuma sana kiuchumi lakini hawana namna kwa kuwa ni majanga ya kiasili yanayojitokeza bila kutarajia.

Akizungumza na wananchi hao wakati alipofika katika eneo la tukio, Mkuu wa Wilaya ya Kakonko,Kanali Hosea Ndagala amesema tukio hilo ni kama matukio mengine halikutegemea litojee hivyo watu wanatakiwa kuwa wavumilivu na kujua kuwa mambo hayo ni mpango wa mwenyezi Mungu na kutoa pole kwa wote walioingia hasara katika kupoteza ng'ombe hao.

"Nitoe pole kwa wote mliondokewa na mifugo hii, ni kweli inaumiza sana na ni hasara kubwa mmeipata, jambo kubwa ni kumshukuru Mungu kwa kuwaponya watu waliokuwa wanawachunga ng'ombe hao, kikubwa ni uvumilivu msikate tamaa muendelee kupambana haya mambo yanatokea hatuna sababu ya kukata tamaa katika utafutaji poleni sana", amesema Kanali Ndagala.

Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala akizungumza na wananchi waliojitokeza katika tukio la ng'ombe kupigwa radi.Picha zote na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog
Mkuu wa wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala akiangalia ng'ombe waliokufa kwa kupigwa radi.
Share:

RAIS MAGUFULI AWAPA RUNGU WATENDAJI WA KATA KUWATWANGA MAWAZIRI,WAKURUGENZI, MA RC WANAOFANYA MAMBO YA HOVYO


Rais wa Tanzania, John Magufuli amewataka watendaji wa kata nchini kutoa taarifa kuhusu wakurugenzi, mawaziri na wakuu wa mikoa wanaofanya matendo yanayokiuka misingi ya utawala bora.


Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Septemba 2, 2019 Ikulu jijini Dar es Salaam alipokutana na watendaji hao kutoka mikoa yote nchini.

Amebainisha kuwa mtendaji wa kata ndio bosi wa eneo lake, “Hata kama kuna kiongozi wa nafasi gani yuko chini yako na anapoonekana kuenenda visivyo unapaswa kumwajibisha au kutoa taarifa kwa mamlaka yake.”

“Katika kata kuna mkurugenzi wa halmashauri, RC (mkuu wa Mkoa), waziri au nani, wewe (mtendaji kata) ndio msimamizi, kama wewe upo katika kata na ambayo kuna waziri, RC, mkurugenzi sijui nani wewe ndiyo msimamizi,” amesema Magufuli.

Ameongeza, “Usiogope kumlima (barua) na kumwandikia maoni, hata kama anakuzidi cheo kwamba katika kata hii namwona mtumishi huyu anakwenda kinyume na maadili. Na ukimwona ni mkubwa sana, piga nakala hapa kwangu, lazima watu tujifunze kuogopana.”

Huku akizungumza zaidi kwa mifano amesema, “Kila siku anapigana (kiongozi) baa katika kata yako kwa sababu ni mkubwa unaacha kumripoti, chalaza kalamu na ndio maana watendaji kata wana kalamu na saini zao.”

Huku akiwataka kutokubali kudharaulika katika maeneo yao, Magufuli amesema, “Hapa (Ikulu) ni kwenu na mimi ni mpangaji tu hapa na mnaoamua nani aende Ikulu ni nyinyi na wananchi.”
Via Mwananchi

Share:

Angalia Picha : RAIS MAGUFULI AKIZUNGUMZA NA WATENDAJI WA KATA ZOTE


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Watendaji wa Kata zote za mikoa ya Tanzania Bara Ikulu jijini Dar es Salaam. PICHA NA IKULU

Share:

MWAKYEMBE AFURAHISHWA UANZISHWAJI WA SHULE YA MICHEZO 'KAHAMA UNITED SPOTS ACADEMY'

Na Salvatory Ntandu 
Waziri wa Habari Sanaa na Utamaduni, Dkt. Harrison Mwakyembe ameupongeza uongozi wa (Kahama United Sports Academy) kwa kuanzisha shule maalumu ya michezo yenye lengo la kuinua na kukuza vipaji vya mipira wa miguu hapa nchini.

Pongezi hizo amezitoa jana wilayani Kahama mkoani Shinyanga katika hafla maalum ya uzinduzi wa shule hiyo na kusema kuwa endapo kila mkoa hapa nchini utaanzisha shule za michezo Tanzania itakuwa na hazina kubwa ya vijana wenye vipaji maalumu vya michezo tofauti tofauti ambayo iwasadia kupata ajira.

Amefafanua kuwa Michezo kwa sasa ni ajira hivyo kuwepo kwa shule hizo kutatoa fursa kwa wachezaji kuajiriwa na vilabu mbalimbali vinavyoshiriki mashindano ya ndani ya nchi na kimataifa kutokana na kupata maarifa sahihi katika shule hizo.

Waziri Mwakyembe amesema serikali itaendelea kuwaunga mkono wadau wote wa michezo watakaokuwa tayari kuanzisha shule za michezo ili kuhamasisha vijana kupenda kushiriki katika michezi mbalimbali na kuwawezesha kutojiunga na makundi hatarishi katika jamii.

Aidha Mwakyembe amekubali kuwachukua wachezaji wawili wa shule hiyo ambao ni pamoja na Delphinius Dikson,Raphael Kevin na Peter Nzogoya na kuwapeleka kufanyiwa majaribio katika timu ya taifa ya vijana ya Serengeti.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya Usaji wa shule hiyo,Hamis Mgeja ameiomba serikali kuziwezesha shule hizo kwa kuzipa vifaa vya michezo vya kisasa ili kuendana na soka la ushindani hapa nchini.
Waziri wa Habari Sanaa na Utamaduni, Dkt. Harrison Mwakyembe akikata keki wakati wa uzinduzi wa shule ya  Kahama United Sports Academy
Mwenyekiti wa bodi ya Usaji wa shule ya  Kahama United Sports Academy, Hamis Mgeja akizungumza wakati wa uzinduzi wa shule hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Kahama,Anamringi Macha akizungumza wakati wa uzinduzi wa shule ya  Kahama United Sports Academy
Share:

OFISI YA MAKAMU WA RAIS YAWAPA MAFUNZO KAMATI YA BUNGE


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. George Simbachawene amesema mchakato wa Mkataba Minataka kuhusu Zebaki unaenda hatua kwa hatua ili kuwaandaa watu kuweza kupokea mabadiliko.

Mhe. Simbachawene amesema hayo jana Septemba mosi, 2019 wakati wa semina kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira ya Mkataba wa Minamata kuhusu Zebaki na Uwajibikaji kisheria na fidia kwa madhara yanayoweza kutokea kutokana na matumizi ya bioteknolojia iliyofanyika Jijini Dodoma.

Alisema Serikali iliridhia Mkataba wa Minamata ili kulinda afya ya binadamu na mazingira dhidi ya madhara yanayotokana na uchafuzi wa mazingira unaotokana na Zebaki. 

"Umoja wa Mataifa ulikaa na kuona kwa fundisho lililotokea Minamata huko Japan hivyo madhara hayo yasiendelee kutokea duniani pamoja na hayo lakini bado zebaki ina kazi ya kufanya unapotaka kuwatoa watu kutoka utamaduni mwingine mabadiliko yanakuwepo. 

"Pengine mnaweza kusema kwanini zebaki isipigwe marufuku mara moja mambo yanayobadilika yanafanywa polepole si kwa haraka na hatimaye watu wataelewa tu," alisema.

Awali aakiwasilisha mada hiyo, Mhandisi wa Viwanda kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais ambayo imeandaa semina hiyo Julius Enock alisema madhara yanayotokana na zebaki ni kuathiri mfumo wa neva za fahamu.

Katika kuathiri kwa mfumo huko inasababisha kusikia, kuongea, kuona, kumeng’enya, kumeza chakula, kutembea kuathiriwa pamoja na ukakamavu wa mwili. 

Aidha madhara mengine aliyotaja Enock ni kuathiri viungo muhimu vya mwili ambayo ni moyo, mapafu, ini, figo na hata mimba.


Share:

Mahakama kuamua leo kuhusu Hatima ya Mrithi wa Ubunge Jimbo la Tundu Lissu

Hatima ya kuapishwa kwa mbunge mteule wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu (CCM), itajulikana leo baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuamua iwapo itatoa zuio la kuapishwa kwa mbunge huyo ama la.

Katika maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo na kaka wa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Tundu Lissu, Alute Mungwai Lissu, pamoja na mambo mengine, ameiomba Mahakama hiyo itoe zuio la kuapishwa kwa mbunge huyo mpya na ruhusa ya kumshtaki Spika wa Bunge, Job Ndugai, kwa kumvua ubunge pasipo sababu za msingi.

Awali Mahakama hiyo ilitupilia mbali mapingamizi yaliyowekwa na upande wa Jamhuri uliotaka kesi hiyo isisikilizwe mahakamani hapo, kutokana na walichodai ni mapungufu ya kisheria ya maombi hayo, hivyo kutaka yasisikilizwe.

Jaji wa Mahakama Kuu, Sirilius Matupa, aliyatupa mapingamizi hayo baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili kwa maelezo kwamba upande wa Jamhuri haukuwa na hoja za msingi za kuizuia kesi hiyo isisikilizwe mahakamani hapo, hivyo kukubaliana na hoja za Wakili wa Lissu, Peter Kibatala.


Share:

LIVE: Rais Magufuli Azungumza Na Watendaji Wa Kata Zote Tanzania Bara Ikulu Dar es Salaam

LIVE: Rais  Magufuli Azungumza Na Watendaji Wa Kata Zote Tanzania Bara  Ikulu Dar es Salaam


Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger