Thursday, 9 April 2026
SANGU ASISITIZA UMUHIMU WA TAASISI ZA KIDINI KATIKA KULINDA AMANI YA NCHI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, ametoa wito kwa taasisi za kidini nchini kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhubiri na kulinda amani, akitambua mchango wao mkubwa katika kudumisha utulivu wa kijamii.
Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 19 ya Kanisa la WRC huko Kivule, Dar es Salaam, Waziri Sangu alibainisha kuwa ushirikiano kati ya serikali na viongozi wa kiroho ni nguzo imara inayohakikisha wananchi wanaishi kwa mshikamano na upendo, jambo ambalo ni msingi wa maendeleo ya taifa.
Katika kutilia mkazo umuhimu wa amani, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa, aliwasihi viongozi wa dini kutumia nafasi zao kukemea vitendo vyote vinavyohatarisha usalama, ikiwemo matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yanayoweza kuchochea taharuki.
Alisisitiza kuwa serikali inategemea maombi na malezi ya kiroho kutoka kwa madhehebu mbalimbali ili kujenga jamii yenye maadili mema, ambayo itakuwa vigumu kushawishika kujiingiza katika uhalifu au uvunjifu wa amani.
Kwa upande wao, viongozi wa kisiasa waliohudhuria hafla hiyo, akiwemo Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya na Mbunge wa Kivule, Ojambi Massaburi, walikiri kuwa malezi ya kiroho yamekuwa na mchango mkubwa katika kuandaa viongozi waadilifu.
Walibainisha kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anatambua thamani ya taasisi hizi na anaendelea kuunga mkono juhudi zao za kuliombea taifa. Kupitia maadhimisho hayo, ilibainika kuwa elimu ya uzalendo na mshikamano, hasa kuhusu Muungano, itaendelea kutolewa kwa vijana ili kuhakikisha tunu ya amani inarithishwa kwa vizazi vijavyo bila kutetereka.
GAVANA TUTUBA :TANZANIA IMEPIGA HATUA MIFUMO YA MALIPO YA KIKANDA
Na mwandishi wetu,Morocco
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuunganishwa na mifumo ya malipo ya kikanda, hatua inayorahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha ndani na nje ya nchi pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Akizungumza leo Aprili 3, 2026 jijini Tangier, nchini Morocco, wakati wa mjadala wa mawaziri katika Kikao cha 58 cha Tume ya Uchumi ya Afrika (ECA), Gavana Tutuba amesema hatua hiyo inaifanya Tanzania kuwa sehemu muhimu ya mtandao wa malipo barani Afrika.
“Tanzania ni sehemu ya mifumo ya malipo ya kikanda ikiwemo Mfumo wa Malipo wa Afrika Mashariki (EAPS) na Mfumo wa Malipo wa Ukanda wa Kusini mwa Afrika (SADC RTGS). Kwa sasa benki za biashara nchini zinaendelea kujiunga na Mfumo wa Malipo wa Afrika (PAPSS), unaowezesha miamala ya kifedha kati ya nchi za Afrika kwa haraka na ufanisi,” amesema Bw. Tutuba.
Ameeleza kuwa kuimarika kwa mifumo hiyo kutachochea biashara ya mipakani na kuongeza ushirikiano wa kiuchumi barani Afrika, huku akibainisha kuwa hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kutumia teknolojia ya fedha kuboresha sekta hiyo.
Aidha, amesema uwepo wa mifumo hiyo ni matokeo ya maendeleo ya teknolojia ya fedha (fintech), akisisitiza kuwa BoT inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana wabunifu kupitia majukwaa mbalimbali ili kuibua suluhisho za kidijitali zitakazoboresha huduma za kifedha nchini.
Akizungumzia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Gavana Tutuba amesema teknolojia ya fedha pamoja na ubunifu wa kidijitali vitaendelea kuwa nguzo muhimu katika kujenga uchumi imara, jumuishi na wenye ushindani.
Kikao hicho kimewakutanisha mawaziri wa fedha, mipango na maendeleo ya uchumi pamoja na magavana wa benki kuu kutoka nchi mbalimbali za Afrika kujadili mwelekeo wa uchumi wa bara hilo na namna ya kuimarisha mifumo ya kifedha.
JAMII YATAKIWA KUSHIRIKIANA NA VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA KULINDA AMANI
Jamii imetakiwa kushirikiana kwa karibu na Vyombo vya ulinzi na usalama na mamlaka nyingine za uongozi zilizopo nchini katika kutoa taarifa za matukio ya uvunjifu wa amani, uhalifu na wahalifu pamoja na kutumia vyema mitandao ya Kijamii ili kudumisha na kuendeleza amani, utulivu na usalama wa nchi kama msingi mkuu wa uhai, maendeleo ya kiuchumi, kijamii na ustawi wa haki.
Kadhalika Waandishi wa habari hapa nchini wamehimizwa kutumia kalamu zao vyema na kuandaa maudhui kwenye majukwaa yao ya habari ya kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kudumisha amani nchini ili kuhakikisha kuwa amani hiyo inaendelea kuwepo pamoja na kuendeleza mshikamano wa Watanzania kwa kuuhabarisha kuhusu hatua mbalimbali za maendeleo na namna wanavyoweza kunufaika na amani na utulivu unaoendelea kuwepo nchini.
Wito huo umetolewa na Epimark Aqwesso na Gabriel Hilonga Silo, wakazi wa Wilayani Karatu Mkoani Arusha, wakitahadharisha watanzania kurejea katika matukio ya uvunjifu wa amani wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 na kadhia waliyokutana nayo kutokana na kukwama kwa shughuli za kiuchumi na kijamii.
"Amani tuliyonayo hapa nchini kwetu ndio inatufanya tuendelee kukusanyika na kufanya shughuli zetu nyingine za kijamii na kiuchumi. Mnakumbuka tukio la Oktoba 29, 2025? wengi wetu tulishindwa kufanya shughuli zetu, hofu ilitanda na wengi waliingia mitini na kujificha, hali hii isijirudie tena, Vijana wa sasa (GenZ) tukumbuke kuna maisha kesho na kamwe tusiharibu amani ya nchi yetu." Amesema Bw. Aqwesso.
Kwa upande wake Bw. Silo amehimiza Vijana kutumia vyema fursa ya amani iliyopo nchini kwa kujiendeleza kiuchumi, akieleza namna ambavyo serikali imeendelea kuwezesha wananchi kiuchumi kupitia sekta mbalimbali ikiwemo kilimo na ufugaji, akisisitiza kuwa amani ndio uhai wa Nchi na wananchi wake na kutaka jamii kushirikiana kuilinda.
Wednesday, 8 April 2026
SERIKALI YAINUA UTALII WA TIBA: WAGONJWA WA NJE WAFIKIA 3,018
Na Shaban Juma, WAF – Dodoma
Serikali ya Tanzania inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kukuza utalii wa tiba, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuongeza uchumi wa sekta ya afya na mchango wake wa pato la Taifa.
Hayo yamesemwa leo Aprili 08, 2026, na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, bungeni jijini Dodoma, akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Dkt. Catherine Canute Joachim, katika Bunge la Kumi na Tatu, Mkutano wa Tatu, Kikao cha Nne.
Akijibu swali kwa niaba ya Waziri wa Afya,.Mhe. Mohamed Mchengerwa, Dkt. Samizi amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imewekeza zaidi kwenye uboreshaji wa miundombinu ya hospitali, ikiwemo kujenga majengo mapya na kukarabati yale yaliyochakaa.
Aidha, amesema Serikali inaendeleza upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa kama PET/CT Scan, Angio Suite, Cathlab, na CT Scan, sambamba na kuendeleza mafunzo ya kitaaluma kwa wataalamu wa afya ili kuhakikisha huduma zinakuwa za ubora wa kimataifa.
“Serikali pia inaanzisha huduma mpya za ubingwa bobezi na kuhakikisha hospitali zinapata ithibati za kimataifa, na kuzitangaza katika masoko ya kimataifa ili kuvutia wagonjwa kutoka nje ya nchi,” amesema Dkt. Samizi.
Takwimu zinaonyesha ukuaji wa utalii wa tiba: katika kipindi cha Julai 2025 hadi Februari 2026, wagonjwa 3,018 kutoka nje ya nchi walipatiwa huduma za ubingwa bobezi katika hospitali za rufaa za mikoa, kanda, maalum na taifa.
Aidha, Dkt. Samizi ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika rasilimali watu kupitia Samia Health Super-specialization Program, ambapo wataalamu 1,483 wanafadhiliwa kusomea fani za ubingwa na ubingwa bobezi ndani na nje ya nchi, hatua inayolenga kuongeza ubora na uwezo wa hospitali zetu.




























