Monday, 6 April 2026

POLISI TANGA WAOKOA VIJANA 87 WALIOINGIZWA KWENYE MTEGO WA UTAJIRI WA HARAKA MTANDAONI

...

Na Hadija Bagasha - Tanga

Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga kupitia Kikosi cha Upelelezi wa Makosa ya Jinai (CID), limefanikiwa kuwaokoa vijana wapatao 87 waliokuwa wametapeliwa fedha zao kupitia mtandao  baada ya kushawishiwa kujiunga na kampuni inayojinasibisha kufanya biashara ya mtandao inayofahamika kwa jina la Champions E-Commerce Education ambapo katika tukio hilo vijana hao walihamasishwa kujiunga na kampuni hiyo kwa ahadi ya kupata utajiri wa haraka kupitia biashara za mtandaoni. 

Kwa mujibu wa Taarifa za awali zinaeleza kuwa vijana hao ni kutokea Mikoay a Mtwara, Iringa, Daresalaa na Morogoro ambao walishawishiwa kujiunga na Kampuni hiyo kwa ahadi ya kupata utajiri wa haraka kupitia biashara za mtandaoni, ambapo walielezwa kuwa wangeanza kupata faida kubwa ndani ya muda mfupi mara baada ya kukamilisha mafunzo.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa polisi Mkoa Tanga Almachius Mchunguzi ameeleza kuwa kila kijana alitakiwa kuchangia kiasi cha fedha kuanzia shilingi laki sita (600,000) hadi kufikia shilingi milioni nne (4,000,000) kama mtaji wa awali pamoja na gharama za mafunzo, fedha ambazo walidaiwa kuambiwa ndizo zingewapa fursa ya kuanza biashara na kupata faida  kwa haraka.

Hata hivyo, baada ya kujiunga na mfumo huo, vijana hao walikutwa wakiishi katika mazingira yasiyoridhisha huku wakiendelea kupatiwa mafunzo yanayodaiwa kuwajengea uwezo, wakisubiri kupata utajiri waliokuwa wameahidiwa.

Katika operesheni hiyo, Jeshi la Polisi limekamata na kuwashikilia kwa mahojiano zaidi watu wawili waliokuwa wakisimamia kundi hilo ambao ni Mohammed Hamis Idrisa (24) mkazi wa Masiwani Jijini Tanga, na Fidolini Hamisi Rashidi (21) mkazi wa Mbugani.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limetoa wito kwa wananchi kuwa makini na aina ya uwekezaji unaohusisha ahadi za kupata faida kubwa kwa muda mfupi bila kuwa na taarifa sahihi, pamoja na kufanya uhakiki kama kampuni husika imesajiliwa na mamlaka halali.

Polisi imewataka wananchi kufanya uchunguzi wa kina kabla ya kujiunga na taasisi au kampuni yoyote inayojihusisha na uwekezaji hususan kupitia mitandao, ili kuepuka kuingia kwenye mitego ya utapeli.

Uchunguzi wa tukio hilo unaendelea huku Jeshi la Polisi likisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kuhusika na utapeli wa aina hiyo.




Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger