Jeshi la Polisi linawashikilia watuhumiwa wawili kuhusiana na mauaji ya kikatili ya mwanamke Hollo Ruchanganya (60), mkazi wa kijiji cha Bunambiyu wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, huku uchunguzi wa awali ukihusisha imani za kishirikina.
Akizungumza na vyombo vya habari mjini Shinyanga leo Jumamosi Aprili 4, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Janeth Magomi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa watuhumiwa hao wanahojiwa ili kubaini ukweli wa tukio hilo.
Katika tukio hilo, marehemu Hollo Ruchanganya aliuawa kikatili kwa kukatwa shingoni na mtu asiyejulikana, kabla ya mwili wake kutupwa katika shamba la mahindi jirani na makazi yake.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, mtuhumiwa wa mauaji hayo anadaiwa kuwa mgeni aliyefika nyumbani kwa marehemu majira ya saa 3:00 usiku wa Aprili 3, 2026, ambapo alikula chakula pamoja na marehemu na wajukuu wake.
Baadaye marehemu alimsindikiza mtuhumiwa huyo kwa lengo la kumpeleka kwa mtalaamu wa tambiko linalodaiwa kuzuia kupata watoto pacha.
Inaelezwa kuwa muda mfupi baada ya kutoka, mtu huyo alirejea nyumbani na kurejesha tochi, akiwataarifu wajukuu wa marehemu kuwa bibi yao angerudi asubuhi kutoka kwa mganga anayeelezwa kuwa ni ndugu yake.
Mwili wa marehemu uligunduliwa asubuhi na mjukuu wake aliyekuwa akielekea shambani, baada ya kuona damu nyingi na nguo za marehemu njiani. Baada ya kutoa taarifa kwa ndugu, walifanikiwa kuufuatilia mwili huo uliokuwa umetupwa shambani ukiwa na jeraha kubwa la kukatwa shingoni.
Kamanda Magomi amesema uchunguzi unaendelea ili kubaini wahusika wote na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.


0 comments:
Post a Comment