Saturday, 19 August 2023

NELSON MANDELA YAPOKEA BETRI 64 ZA KUHIFADHI NISHATI YA JUA




Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ubunifu Profesa Anthony Mshandete (katika) pamoja na Balozi wa India Nchini Tanzania Binnaya Srikanta Pradhan (Kulia) wakikata utepe kuashiria mapokezi rasmi ya Betri 64 zenye uwezo wa kuhifadhi nishati jua kwa saa nane kutoka Serikali ya India.


Balozi wa India nchini Tanzania, Binnaya Srikanta Pradhan akiongea na wajumbe waliohudhuria hafla ya makabidhiano ya Betri 64 zenye uwezo wa kuhifadhi nishati jua kwa saa nane zilizotolewa na Serikali ya India kwa Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia


Balozi wa India nchini Tanzania, Binnaya Srikanta Pradhan (katikati) akiongozana na menejimeti ya Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia wakielekea katika eneo la kukata utepe katika hafla ya makibhiano ya betri 64.


Balozi wa India nchini Tanzania, Binnaya Srikanta Pradhan (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe waliohudhuria hafla ya makabidhiano ya Betri 64 zenye uwezo wa kuhifadhi nishati jua kwa saa nane kutoka Serikali ya India kwa ajili ya Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia.

Balozi wa India nchini Tanzania, Binnaya Srikanta Pradhan (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia wakati wa hafla ya makabidhiano ya Betri 64 zenye uwezo wa kuhifadhi nishati jua kwa saa nane kutoka Serikali ya India kwa ajili ya Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia.

Na Mwandishi wetu

Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia (NM-AIST) imepokea betri 64 zenye uwezo wa kuhifadhi nishati jua kwa saa nane kutoka Ubalozi wa India nchini Tanzania, zitakazowezesha kompyuta yenye uwezo mkubwa wa kuchakata data kwa kasi kubwa (Param Kilimanjaro Super Computer) ambayo ina uwezo wa kufanya kazi kwa saa 24.


Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo leo tarehe 19 Agosti,2023 Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ubunifu Profesa Anthony Mshandete alisema kompyuta hiyo inauwezo wa kuchakata data kwa kasi ya hali ya juu na tangu ilipozinduliwa miaka sita iliyopita ilikumbana na changamoto ya nishati pale umeme unapokatika.


Alisema upatikanaji wa Betri hizo utawezesha kompyuta hiyo kufanya kazi kwa ufanisi kwa manufaa ya taasisi ambapo hutumika kwa ajili ya kufundisha shahada ya pili ya (Master’s Degree) , kuchakata data za Kibailojia pia itatumika kuchakata data kutoka katika taasisi mbalimbali za Serikali na itasaidia katika kuhifadhi data nyeti za serikali.


"Kompyuta hii itasidia kuhifadhi data ndani na nje ya Tanzania kwani inauwezo mkubwa katika ufanisi wenye tija katika masuala ya Tehama, na tunashukuru kwa betri hizi ambazo zitawezesha upatikanaji wa uhakika wa umeme katika kufundishia masomo mbalimbali chuoni hapa ", anasema Profesa Mshandete.



Kwa upande wake Balozi wa India nchini Tanzania, Binnaya Srikanta Pradhan alikipongeza kituo cha Umahiri cha Teknolojia Afrika Mashariki, katika masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika kutoa elimu zaidi katika masuala ya TEHAMA (ICT).


Alisema India inatambua mchango mkubwa wa masuala ya teknolojia na kuipongeza taasisi hiyo kwa kutoa elimu katika masuala ya kompyuta.



"India itaendelea kuhakikisha masuala ya Tehama yanakua zaidi na chuo hiki ni sehemu ya kutoa elimu ya Tehama kwani Dunia hii ina mabadiliko mengi katika masuala ya TEHAMA , nawapongeza kwa kuimarisha masuala ya teknolojia " ,alisema Balozi Pradhan.

Naye Kaimu Mkuu wa Shule ya Masuala ya Tehama, Hesabati na Mawasiliano Dkt, Judih Leo aliishukuru Serikali ya India kwa kuendeleza Ushirikiano na Kituo hicho na kwa kuwezesha upatikanaji betri utakaosaidia Kompyuta hiyo kubwa (Super Computer) inayoyofanya kazi za tafiti kufanya kazi kwa bidii kwani awali walikuwa na changamoto ya umeme pale wanapotaka kufanya kazi zao, lakini sasa uwepo wa betri hizo utawezesha ufanisi zaidi katika utoaji wa mafunzo kwakutumia kompyuta hiyo.


Serikali ya India na Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia imekuwa ikishirikiana kwa karibu katika kuhakikisha teknolojia inakuwa kwa kasi katika kuleta maendeleo kupitia masomo ya TEHAMA.

Share:

MARYPRISCA AIPONGEZA DAWASA KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA UONGOZI WA WILAYA KUTATUA CHANGAMOTO YA MAJI



NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

NAIBU Waziri wa Maji Mhe.Maryprisca Mahundi amefanya ziara kutembelea Mradi wa Usambazaji wa Majisafi kati ya Makongo na Mji wa Bagamoyo ambapo amewapongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), kwa jitihada ambazo wanazifanya katika maeneo ambayo yamenufaika na mradi huo.

Akizungumza kwenye ziara hiyo leo Agosti 19,2023 mpaka sasa kwa kiwango kikubwa wananchi wameweza kupata maji kwa uhakika katika maeneo mengi ambayo mradi huo umepita na wataendelea kuwafikia wale wote ambao hawajafikiwa na huduma ya majisafi na salama ili wananchi waweze kuwa na uhakika na upatikanaji wa maji kwenye maeneo yao.

Aidha Naibu Waziri amesema Wizara inaendelea kusambaza mita ambazo utakuwa unalipia kabla ya matumizi ili kuondokana na ulimbikizaji wa bili.

Amesema wasomaji wa mita wa DAWASA wanatakiwa kushika taratibu ambazo wamejiwekea kuondokana na malalamiko yasiyo ya lazima kutoka kwa wateja wao.

Pamoja na hayo amewapongeza DAWASA kwa kuendelea kushirikiana na uongozi wa Wilaya ya Kinondoni katika kuhakikisha wanashughulikia kero ambazo zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara kwa wananchi hususan kwenye masuala ya maji.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uzalishaji na Usambazaji Mhandisi Shabani Mkwanywe ambaye amemuwakilisha Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA kwenye ziara hiyo, amesema maeneo kuanzia Makongo mpaka Bagamoyo asilimia 80 hadi 90 ya wananchi wamepata huduma ya majisafi na bado kuna sehemu chache ambazo hawajakamilisha na wanaendelea na jitihada za kukamilisha hususan yale maeneo ambayo yalikuwa nje ya mradi.

"Tupo tayari wakati wowote kushirikiana na wadau katika kuhakikisha kwamba huduma ya maji inakuwa bora zaidi na ingawa bado kuna changamoto chache ambazo tunaamini ndani ya mwaka huu wa fedha tunaenda kuzimaliza na wananchi wapate maji kwa uhakika". Amesema

Nae Mwakilishi wa Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Goba, Bw. Emirick Msuya amesema kwasasa upatikanaji wa majisafi ni mzuri ukilinganisha na kipindi cha nyuma ambapo maji yalikuwa yanapatikana kwa shida na ukizingatia katika zahanati hiyo uhitaji wa maji ni mkubwa.

Kwa upande wa wananchi wa Mivumoni Wazo Jijini Dar es Salaam, wameipongeza Serikali kwa kuwaondolea kero ya upatikanaji wa maji katika maeneo hayo, ambapo kwa sasa maji yanapatikana kwa uhakika.

Share:

PROF. KIPANYULA AWASILI NELSON MANDELA TAYARI KUTEKELEZA MAJUKUMU




Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia Professa Maulilio Kipanyula akiongea na watumishi wa taasisi hiyo mara baada ya kuwasili


Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia Professa Maulilio Kipanyula akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika taasisi hiyo


Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia Professa Maulilio Kipanyula (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa taasisi wa kwanza kulia ni Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Bw. Sylvester Kazi , wa pili kulia ni Makamu Mkuu wa Taasisi aliyemaliza muda wake Professa Emmanuel Luoga na wa kwanza Kushoto ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Mipango,Fedha na Utawala Professa Suzana Augustino na wa pili Kushoto ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Elimu, Utafiti na Ubunifu Professa Anthony Mshandete.


Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia Professa Maulilio Kipanyula (katikati aliyekaa) akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Taasisi.

Na.Mwandishi Wetu.

Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia Profesa Maulilio Kipanyula amewataka Watumishi wa taasisi hiyo, kumpa ushirikiano katika kufikia lengo la kuanzishwa kwa Taasisi hiyo.

Professa Kipanyula ameyasema hayo tarehe 18 Agosti, 2023 alipotembelea Taasisi ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia tangu kuteuliwa kwake na Mkuu wa Taasisi hiyo Bw. Omari Issa mnamo tarehe 14 Agosti ,2023.

“Naomba ushirikiano ,umoja na upendo mliouonesha leo uendelee kati yetu ili kwa pamoja tuweze kuendeleza taasisi hii kwa misingi na malengo ya kuanzishwa kwake" anasema Professa Kipanyula

Profesa Kipanyula ameeleza kuwa katika kutekeleza majukumu ya Taasisi atahakikisha vipaumbele vya Taasisi vinazingatia mipango mikubwa ya Serikali hususani Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.

Vilevile Professa Kipanyula alipata wasaa wa kukabidhiwa ofisi na Makamu Mkuu wa Taasisi aliyemaliza muda wake Professa Emmanuel Luoga kwa kukabidhiwa vitendea kazi ambavyo ni dira na muongozo wa utekelezaji wa majukumu yake.

"Natambua kazi nzuri iliyofanywa na mtangulizi wangu Professa Emmanuel Luoga, kwa uongozi mahiri alioufanya na kufanikisha kukifikisha chuo mahali pazuri" Amesema Profesa Kipanyula

Naye Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Bw. Sylvester Kazi amempongeza Professa Kipanyula kwa uteuzi wake na kumuahidi kuendeleza ushirikiano kama ambavyo walikuwa wakishirikiana awali katika baraza la chuo.
Share:

Tazama : MAHAFALI YA NNE MOREGAS ENGLISH MEDIUM SCHOOL 2023

 

Share:

Friday, 18 August 2023

BENKI YA CRDB YAMTANGAZA MSHINDI WA TATU WA TOYOTA CROWN KATIKA KAMPENI YA BENKI NI SIMBANKING

Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Dar es Salaam, Badru Idd (wa pili kulia), akimkabidhi Robert Masala kadi ya gari aina ya Toyota Crown baada ya kushinda katika kampeni ya Benki ni SimBanking katika hafla iliyofanyika nyumbani kwa mshindi, Goba jijini Dar es Salaam Agosti 17, 2023. Wanaoshuhudia kutoka kushoto ni Meneja wa CRDB Tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Donath Shirima na Balozi wa Benki ya CRDB Stephane Aziz Ki.
Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Dar es Salaam, Badru Idd (katikati), akimkabidhi namba ya gari aina ya Toyota Crown mteja wa benki hiyo, Robert Masala (wa pili kulia) baada ya kuibuka mshindi wa kampeni ya Benki ni SimBanking katika hafla ilifyoanyika nyumbani kwa mshindi huyo Goba jijini Dar es Salaam Agosti 17, 2023. Wanaoshuhudia kutoka kushoto ni Meneja wa CRDB Tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Donath Shirima, Balozi wa Benki ya CRDB, Stephane Aziz Ki na kulia ni Meneja Mwandamizi wa Huduma Mbadala za Kibenki, Mangire Kibanda.


========= ========= =========


Benki ya CRDB imemkabidhi Robert Masala, mkazi wa Goba jijini Dar es Salaam gari jipya aina ya Toyota Crown baada ya kuibuka mshindi katika awamu ya tatu ya kampeni ya Benki ni Simbanking.


Masala aliyeibuka kidedea kwa mwezi Julai anaungana na Jared Awando Ojweke aliyekuwa mshindi wa shinda gari Juni na Mayani Yahaya Hassan aliyekuwa wa kwanza mapema Mei.


Akieleza namna anavyoitumia huduma za SimBanking, Masala amesema amekuwa mteja wa Benki ya CRDB tangu mwaka 2005 na huduma hiyo imekuwa ikimrahisishia kufanya miamala hasa ya biashara zake kwa urahisi na kwa wakati.


“Mimi ni mwajiriwa hapa Dar lakini nina biashara Mwanza ambako ndio nyumbani. Simbanking huwa inanisaidia sana kwenye usimamizi wa mapato na matumizi ya biashara. Kati ya mwezi Mei na Juni nilikuwa na miradi naikamilisha hivyo nilitumia sana Simbanking nje ya utaratibu wa kawaida. Nadhani hii imechangia kwa namna au nyingine mimi kushinda gari hili,” amesema Masala.


Tangu alipofungua akaunti ya Benki ya CRDB, Masala ambaye ni baba wa watoto wawili anasema amekuwa akitumia huduma za Simbanking tangu tangu mwanzoni ilipokuwa ikitumia teknolojia ya USSD pekee kwa kubofya *150*03# mpaka ilipoanzishwa programu ya kidijitali ya SimBanking App ambayo amesema ni rahisi na ina ufanisi mkubwa.


Kwa waajiriwa wenzake, Masala amewashauri kuitumia Benki ya CRDB pamoja na Simbanking ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kushinda zawadi kemkem zinazotolewa kila mwezi kuanzia fedha taslimu, simu za mkononi hata gari hasa Toyota Crown linalotolewa kila mwezi na Vanguard atakalokabidhiwa mshindi wa jumla.
Kama ilivyokuwa kwa washindi waliomtangulia, Masele naye amekabidhiwa gari hilo lenye thamani ya TSZ 20 milioni likiwa limekatiwa bima kubwa na kujaziwa mafuta “full tank.”


Akimkabidhi zawadi hiyo, Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Mashariki, Badru Idd amesema kwa hali ilivyo sasa hivi ni ngumu kuuepuka uchumi wa kidijiti hivyo Watanzania hawapaswi kubaki nyuma watumia huduma za Simbanking, jukwaa bora zaidi nchini na linaloongoza kwa kutumiwa kati ya programu za benki zilizopo.


“Leo tunamtangaza Robert Masala aliyeibuka mshindi wa gari kwenye droo iliyochezeshwa tarehe 3 mwezi huu. Yeye ni ni mshindi wa tatu kuondoka na gari baada ya Jared Awando Ojweke wa hapa Dar es Salaam na Mayani Yahaya Hassan wa mkoani Dodoma kushinda miezi miwili iliyopita. Simbanking ni ya kila mtu, unaweza kumaliza mahitaji yako ukiwa mahali popote,” amesema Idd.


Ikiwa benki kiongozi nchini, meneja huyo amesema Benki ya CRDB inahakikisha wakati wote inaboresha huduma zake ili kukidhi mahitaji ya wateja ikitambua kwamba matarajio yao yanabadilika kila siku.


Hivi karibuni Benki ya CRDB ilizindua SimBanking App mpya ikiwa ni sehemu ya jitihada za benki katika kuboresha huduma na kuleta mapinduzi katika sekta ya fedha nchini.


SimBanking mpya imetengenezwa kwa muunganiko wa teknolojia za kisasa na za hali ya juu ikiwamo akili mnemba (Artificial intelligence), jambo linaloifanya kuwa na uwezo mkubwa katika utambuzi wa tabia na mahitaji ya mteja pindi anapotumia.
Mshindi wa gari aina ya Toyota Crown wa kampeni ya Benki ni Simbanking ya Benki ya CRDB, Robert Masala akiwa na mkewe, Esther Itule baada ya kukabidhiwa gari hilo na Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Mashariki, Badru Idd.

Share:

TGNP YAWAKUTANISHA WANAHABARI NA VIONGOZI WA VITUO VYA TAARIFA NA MAARIFA



******************

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) imewakutanisha Waandishi wa habari na viongozi wa Vituo vya Taarifa na Maarifa kwaajili ya kujadili ni namna gani wanaweza kushirikiana katika kuhakikisha wanatokomeza masuala ya Ukatili wa kijinsia pamoja na upatikanaji wa huduma bora za kijamii kwenye maeneo wanayoishi.

Akizungumza katika kikao hicho Jana Agosti 17,2023 Jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Vituo vya Taarifa na Maarifa Bi. Jachrine Mtesha amesema mpaka sasa kuna vituo vya Taarifa na Maarifa 75 katika mikoa 15 hapa nchini na bado wanaamini vitaendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka.

Aidha amesema umuhimu wa vituo hivyo ni kujenga uwezo wa jamii kupata habari,taarifa na kuendesha/kushiriki mijadala mbalimbali inayohusu utu na usawa wa kijinsia na haki za kijamii kazi ambayo vituo hivyo imeendelea kuifanya kwa ufanisi mkubwa.


Nae Mwenyekiti wa Kituo cha Majoe Bi. Tabu Ally amebainisha changamoto aliyowahi kukumbana nayo ya kukamatwa na baadhi ya Viongozi wa ngazi ya Serikali ya mtaa na kuwekwa Kituo cha Polisi kwa siku kadhaa kutokana na viongozi hao kutoelewa na kuhisi analengo la kuwa juu yao.

Ameongeza kuwa baada ya kadhia hiyo kupita hivi sasa wamewaelewesha viongozi hao na wanafanyakazi kwa ukaribu zaidi katika kupigania maendeleo ya jamii zao hasa katika maeneo ambayo yanawazunguka.

Mwenyekiti wa Kituo cha Taarifa na Maarifa, Kivule Bi Zahara Mohamed Mzee amesema awali walipokuwa wanaanza kazi katika jamii walikumbana na changamoto ya Viongozi wengi kutokuwa na Imani nao na kudhania kuwa Wanamalengo ya kuwapindua katika nafasi zao katika siku za usoni hivyo kukosa ushirikiano wa kutosha kutoka kwao.

Aidha Bi Zahara ameyataja mafanikio waliyoyapata ikiwa ni pamoja na kujenga Ushirikiano wa karibu na viongozi hao kuanzia ngazi ya Serikali ya mtaa na hadi Polisi,pia wamefanikiwa kuianisha vipaumbele mbalimbali vya jamii vilivyosaidia kujengwa kwa zahanati,shule,matundu ya vyoo,barabara,ununuzi wa vifaa na ukamilishaji wa Ujenzi wa chumba cha upasuaji katika hospital ya Wilaya Ilala kivule.

Mwaka 2010 mtandao wa kijinsia hapa nchini TGNP ulianzisha vituo vya taarifa na maarifa kwa lengo la kutatua changamoto mbalimbali za kijamii kwa kuhakikisha changamoto hizo zinafika katika mamlaka husika na kupatiwa ufumbuzi

Tangu wakati huo yapata Miaka 13 vituo hivyo vimeleta mafanikio makubwa kwa jamii katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwa kuipa jamii hususan wanawake sauti ya kusemea vitendo mbalimbali vya ukatili wa kijinsia na hata kupeleka maendeleo katika maeneo yaliyo nyuma katika nyanja mbalimbali ikiwemo miundombinu ya barabara,shule na hata upatikanaji wa huduma za afya

Huku mtandao huo ukiwa unatimiza miaka 30 tangu kuanzishwa kwake mwezi oktoba mnamo mwaka 1993 ni wazi vituo vya taarifa na maarifa ni moja ya mambo ambayo unaweza kujivunia nayo.

Share:

WHATSAPP YAONGEZA UFANISI KATIKA UPIMAJI WA MAPEMA WA VVU KWA MTOTO ALIYEZALIWA NA MAMA MWENYE MAAMBUKIZI YA UKIMWI (VVU)

Muuguzi katika hospitali ya Nyerere DDH, Nyanchamba Mulaga Musiba akichukua sampuli ya damu kavu kutoka kwa mtoto ambaye mama yake anaishi na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI

Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog

Imeelezwa kuwa matumizi ya mtandao wa kijamii wa WhatsApp  yameongeza viwango vya ukaguzi wa ubora wa sampuli ya damu kavu (DBS)  katika hospitali ya wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara (Nyerere DDH) hali inayochangia upatikanaji wa taarifa sahihi za sampuli za damu kavu wakati utambuzi wa awali wa Virusi vya UKIMWI kwa watoto walio chini ya miezi 18 ili kujua hali zao kutokana na wazazi wao kuishi na maambukizi ya VVU.



Akizungumza Agosti 17,2023 na Waandishi wa Habari waliotembelea Hospitali ya Nyerere ambayo ni hospitali teule ya wilaya ya Serengeti, Muuguzi katika hospitali ya Nyerere DDH, Nyanchamba Mulaga Musiba amesema uanzishwaji wa matumizi ya jukwaa la WhatsApp kama ukaguzi wa ubora wa sampuli za damu kavu ulifikiwa kwa ajili kuboresha sampuli za damu kavu na kuondoa tatizo la sampuli zinazokataliwa maabara(rejected samples).

“Mnamo mwaka Mwaka 2021 Mkoa wa Mara uliripotiwa kuwa na kiwango kikubwa cha kutokuwa na sampuli bora za damu kavu katika maabara ya taifa ya upimaji (BMC). Taarifa hizo hazikuwa njema kwetu, lilikuwa ni jambo la kusikitisha kwa programu na kuchukuliwa kama kikwazo katika utoaji wa huduma bora za upimaji na utambuzi wa awali wa VVU kwa watoto chini ya miezi 18 (EID) na jitahada za kutokomeza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto”,ameeleza .


Ameeleza kuwa, waliamua kuunda kikundi cha WhatsApp kwa ajili kufuatilia ubora wa ukusanyaji wa sampuli za damu kavu (DBS) katika ngazi ya mkoa huku akiongeza kuwa matumizi ya kundi la WhatsApp kama ukaguzi wa ubora wa sampuli za DBS umefikiwa kwa ajili kuboresha sampuli za damu kavu na kuondoa tatizo ya sampuli zinazokataliwa maabara.
Muuguzi katika hospitali ya Nyerere DDH, Nyanchamba Mulaga Musiba

“Kikundi chetu cha WhatsApp cha mkoa cha damu kavu kina wahusika wakuu wakiwemo wataalamu wa afya katika ngazi ya mkoa na wilaya kama vile maafisa programu, mshauri wa PMTCT, Mratibu wa Afya ya Uzazi wa Mtoto ngazi ya mkoa na waratibu Afya ya Uzazi na wa wilaya kwa kila halmashauri na watoa huduma za afya wanaohusika na ukusanyaji wa sampuli za damu kavu. Pia wataalamu wa maabara ambao ni wazoefu kwenye upimaji wa damu kavu wameunganishwa kwenye jukwaa letu la WhatsApp”,ameeleza.

Ameongeza kuwa kupitia kundi hilo la Whatsapp wamekuwa wakibadilishana mawazo, ushauri na kupeana elimu hivyo kufanya mitandao ya kijamii hususani Whatsapp kama njia rahisi ya kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Amesema Kikundi hicho kinatumika kama nyenzo shirikishi kutoka kwa kila mtaalamu kuhakikisha kuwa kila sampuli ya mtoto mchanga inakuwa katika ubora unaotakiwa kabla ya mama na mtoto hajaondoka kituoni na kwamba pindi kunapokuwa na wasiwasi wa ubora wa sampuli iliyochukuliwa hupata mrejesho kupitia kikundi cha whatsApp, sampuli ya mtoto mchanga inachukuliwa tena kwa ajili ya kukidhi vigezo vya ubora.

“Ninapopata mtoto anatakiwa kuchukuliwa kipimo cha damu kavu katika ngazi ya kituo, kila sampuli ya damu kavu inapochukuliwa moja inatumwa kwenye kikundi cha WhatsApp, hii inaruhusu ukaguzi wa kina wa ubora, huku wataalamu wengi wakitoa maoni kwa wakati mmoja kabla ya mama na mtoto wajaondoka kutoka kituoni kurudi nyumbani.

Kama Sampuli ya DBS iko vizuri,namruhusu mama aondoke,kama haijatoka vizuri narudia kumpima mtoto ili kupata majibu sahihi ili kujua hali ya mtoto ambaye mama yake anaishi na maambukizi ya VVU. Haya yote tunataka mtoto asipate maambukizi”, ameeleza Nyanchamba Muuguzi ambaye tangu aanze kufanya kazi Hospitali ya Nyerere DDH miaka 11 sasa hajawahi kupata kesi ya mtoto kupata maambukizi kutoka kwa mama anayeishi na VVU.


Amebainisha kuwa Matumizi ya teknolojia kupitia Kundi la Whatsapp yamesaidia kupungua kwa sampuli za damu kavu ambazo hazikidhi vigezo katika maabara ya BMC kutoka sampuli tano (5) kipindi cha Oktoba - Desemba 2021 mpaka sasa kituo hakina sampuli inayorudishwa sababu ya kutokidhi vigezo (zero rejection) wakati wa Q1FY21 hadi sampuli 0 zilizokataliwa wakati wa Q2FY21.


Katika hatua nyingine amesema kundi hilo la WhatsApp pia limesaidia kuboresha mawasiliano ngazi ya wilaya au Mkoa pamoja na wadau pindi pindi wanapopata changamoto mfano vitenganishi vinapoisha ambapo wamekuwa wakituma tu ujumbe mfupi (SMS) wanaletewa au kupewa majibu na wahusika mara moja.

Mratibu Msaidizi wa Afya ya Mama na Mtoto Hospitali ya Nyerere Monica Nyasale amesema tangu mwaka 2018 hadi mwaka huu wamefanikiwa kutoa huduma kwa akina mama 31,000 kati yao 196 walibainika kuwa na maambukizi ya VVU ambao tayari wameanzishiwa huduma ya dawa ili kuwakinga watoto wasipate maambukizi ya VVU.
Mratibu Msaidizi wa Afya ya Mama na Mtoto Hospitali ya Nyerere Monica Nyasale

“Nyerere DDH ni kituo cha matunzo na matibabu ambacho hutoa huduma kamili za VVU. Upimaji wa viwango vya VVU na huduma za kinga kama vile PrEP na usambazaji wa kondomu pia hutolewa kupitia usaidizi wa PEPFAR na CDC na kumekuwa na mipango kadhaa ya utoaji wa huduma bora za utambuzi wa awali wa VVU kwa watoto (EID)”,amesema Nyasale.


Naye Mtaalamu wa Maabara katika Hospitali ya Nyerere DDH Serengeti, ambayo inatumika kama Hospitali teule ya Wilaya ya Serengeti, Paschal Wamwaro Magayane amesema mbinu hiyo ya kibunifu imekuwa na mafanikio makubwa kwa sababu hivi sasa wanapata Sampuli zenye ubora na sasa hakuna Sampuli inatakaliwa baada ya kupelekwa Hospitali ya Rufaa Bugando Mkoani Mwanza.

“Kabla ya matumizi ya whatsApp kwenye ukaguzi wa sampuli za damu kavu kituo kilikuwa na changamoto ya kuwafuatilia wa mama ambao sampuli zao zilikataliwa. Hali hii ni tofauti kwa sasa kwa sababu sampuli zisizokidhi vigezo zinarudiwa kabla ya mama kuondoka kituoni. Tunapata sampuli safi tu sasa hivi”, amesema Magayane.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Nyerere DDH Serengeti Dkt. Edgar Saulo Mganyizi

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Nyerere DDH Serengeti Dkt. Edgar Saulo Mganyizi ameishukuru Serikali ya Marekani na Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mkubwa wanaotoa kwenye hospitali hiyo iliyoanzishwa mwaka 1980 ikimilikiwa na Kanisa la Mennonite katika ikiwemo kutokomeza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto


Mkoa wa Mara ni miongoni mwa mikoa minne inayofadhiliwa na PEPFAR kupitia CDC. Tangu Oktoba 2010, CDC inatoa huduma kamili za VVU ili kufikia udhibiti wa janga la VVU na kufikia lengo la 95-95-95 ifikapo 2030.


Mpango huu unasaidia Wizara ya Afya (MoH) kufikia lengo la kitaifa la kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT) hadi chini ya asilimia nne (<4%) ifikapo mwaka 2026 ikiwa malengo ya programu ni pamoja na kuongeza idadi ya wajawazito na wanaonyonyesha wanaojua hali zao za maambukizi ya VVU, kuongeza idadi ya wanawake wajawazito na wanaonyonyesha walio na VVU wanaopata dawa za kufubaza makali ya VVU (ARVs).

Malengo mengine ni kuhakikisha upatikanaji wa huduma za matunzo na matibabu kwa akina mama na watoto wachanga wanaoishi na VVU sambamba na kuboresha maisha ya watoto walio zaliwa na mama mwenye VVU na wale watoto tayari wana maambukizi ya VVU..

Katika Mkoa wa Mara kuna vituo vya afya 358, ambapo vituo vya afya 107 vinasaidiwa kupitia PEPFAR kutoa huduma za matunzo na matibabu pamoja na kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ( PMTCT).

Huduma za utambuzi wa awali wa VVU kwa watoto walio chini ya miezi 18 (EID) hutolewa na wafanyakazi waliofunzwa, na afua muhimu zinasaidiwa ili kuboresha ubora wa huduma za EID, ikiwa ni pamoja na vituo vya kusaidia huduma za EID, usafirishaji wa sampuli za damu kavu (DBS) hadi mahali pa uchunguzi, na urejeshaji wa matokeo ya sampuli kavu (DBS) kwa kutumia mfumo wa barua pepe na kutumia mfumo wa kielektroniki wa rufaa wa sampuli (eSRS).

Juhudi hizi zinalenga kutambua watoto walioambukizwa VVU mapema na kuwaunganisha na huduma za dawa za VVU (ART).

Mtaalamu wa Maabara katika Hospitali ya Nyerere DDH Serengeti, Paschal Wamwaro Magayane

Share:

UVCCM KATA YA MJINI WAFANYA MASHINDANO YA MICHEZO MTAA KWA MTAA,VIWANDANI WASHINDA KWA PENATI DHIDI YA KAUNDA

Diwani wa viti maalum,Ester Makune akizungumza na  wachezaji wa timu mbili kwenye uzinduzi wa mashindano ya UVCCM FOOTBALL CUP 2023 kabla ya kuanza mtanange wa kwanza  katika uwanja wa chuo cha ualimu Shy Com.

Na Halima Khoya,Shinyanga

Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi Kata ya Mjini Manispaa ya Shinyanga (UVCCM) umezindua mashindano ya mpira wa miguu “UVCCM FOOTBALL CUP 2023” yanayohusisha timu nne za ya mpira wa miguu kwa kila mtaa katika kata hiyo ili kutafuta timu moja itakayokuwa timu ya Kata.

Mashindano hayo yamezinduliwa leo Agosti,17,2023 Katika uwanja wa chuo cha ualimu Shy Com na kuhitimishwa agosti,19,2023 ambapo itakua fainali kati ya timu iliyoshinda leo Town stars ya mtaa wa viwandani dhidi ya Stjoseph ya mtaa wa Kaunda na timu itakayoshinda kesho.

Akifungua mashindano hayo,Diwani wa viti maalum,Ester Makune amesema michezo kwa vijana ni tiba na huimarisha afya hivyo amewataka kucheza mpira wenye nidhamu na kuchukua kama faida mashindano hayo ili kutengeneza njia ya mafanikio.

Kwa upande wake,Mwenyekiti wa UVCCM Kata ya Mjini,Abdul aziz Said amesema mashidano hayo yatasaidia vijana kuepukana na makundi yasiyofaa (Vibaka,watiumiaji wa madawa ya kulevya) sambamba na kupunguza wimbi la vijana wasiokuwa na ajira mtaani.

“Kauli mbiu ya mashindano haya ni “Mpira ni ajira”,vijana mchukue nafasi hii kuonyesha vipaji vyenu,mpira unalipa mpira unaajiri,timu mbili za kwanza zimeshacheza na mshindi ni Town stars ambaye atacheza na mshindi wa kesho” amesema” Said.

Nae Mwenyekiti wa Mtaa Viwandani,Ashraf Majaliwa,amesema amefurahishwa na ushindi walioupata na kwamba ameupokea kwa furaha na kwamba wanamatumaini makubwa juu ya timu yao hivyo wanatarajia kushinda fainali.
Diwani wa viti maalum,Ester Makune akikagugua wachezaji wa timu mbili kwenye uzinduzi wa mashindano ya UVCCM FOOTBALL CUP 2023 kabla ya kuanza mtanange wa kwanza  katika uwanja wa chuo cha ualimu Shy Com.
Viongozi wakifuatilia mpira wa miguu uliochezwa leo Agosti,17,2023 kwenye uwanja wa Shy Com majira ya saa 10 kati ya timu ya mtaa wa kaunda na viwandani.
Mwenyekiti wa UVCCM Kata ya Mjini,Abdul aziz Said akizungumza mara baada ya kumalizika mechi ya awamu ya kwanza iliyochezwa Agosti,17,2023 katika uwanja wa Shy Com Mkoani Shinyanga.
Mwenyekiti wa Mtaa Viwandani,Ashraf Majaliwa akizungumza mara baada ya kumalizika mechi ya awamu ya kwanza iliyochezwa Agosti,17,2023 katika uwanja wa Shy Com Mkoani Shinyanga ambapo ushindi umeenda katika Mtaa wake.
Share:

MIAKA 20 YA PEPFAR : WAZEE WA MILA SERENGETI WAGEUKIA TOHARA SALAMA ‘HAKUNA KISU KIMOJA TENA’



Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog

Juhudi za kukabiliana na Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI yanayotokana na wanaume kufanyiwa tohara za kimila katika Wilaya ya Serengeti Mkoani Mara zinazidi kuzaa matunda baada ya Wazee wa Kimila kupata mwamko chanya juu ya tohara kinga ya kitabibu ambayo imekuwa ikitolewa katika vituo vya afya na katika jamii.


Matokeo hayo chanya yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na nguvu ya Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani (PEPFAR), kupitia Kituo cha Udhibiti na Uzuiaji wa Magonjwa cha nchini Marekani (CDC) kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania na Shirika la Amref Health Africa Tanzania ambalo linatekeleza huduma za kupambana na VVU/UKIMWI katika jamii kulingana na ushahidi wa kitafiti kwa makundi ya watu yaliyo katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya VVU ambapo pia limo kundi la wanaume wanaofanyiwa tohara za kimila.

Inaelezwa kuwa mbali na Wilaya ya Tarime, Wilaya ya Serengeti Mkoani Mara pia inatajwa kuwa na idadi kubwa ya wazee wa kimila na mangariba ambao wamekuwa wakifanya tohara za kimila kwa vijana lakini sasa wameanza kubadilika kwa kuachana na utamaduni huo wa tohara za kimila na kuhamasisha tohara kinga za kitabibu.

Akizungumza na Waandishi wa habari waliofanya ziara Mkoani Mara ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 20 ya PEPFAR tangu ilipoanzishwa mwaka 2003, Mmoja wa Wazee wa Kimila aliyejitambulisha kwa jina la John Marwa kutoka Nyamoko Wilaya ya Serengeti amesema hivi sasa wameikubali tohara kinga ya kitabibu.

Mzee wa Kimila Wilaya ya Serengeti (aliyevaa kofia) akielezea hatua walizochukua kuondokana na tohara ya kimila kwa vijana. Mwingine ni Mratibu wa Tohara Wilaya ya Serengeti Dkt. Mary Yohana Kisiri.

“Amref Health Africa Tanzania ambao wanatekeleza Mradi wa Afya Kamilifu wametoa wamefika katika jamii na kutoa elimu ya tohara kinga ya kitabibu, elimu hii imetusaidia kubadilika. Lakini pia wamekuwa wakitupatia vifaa vya kisasa vya kufanyia tohara salama kwa vijana”,amesema Mzee Marwa.

Amesema licha ya kutumia dawa za kienyeji kuzuia damu nyingi zisitoke wakati wa tohara, vijana wamekuwa wakitokwa damu nyingi, hivyo kusababisha baadhi ya kuzimia na wakati mwingine kusababisha kifo na wengine kupata maambukizi ya VVU kutokana na kutumia kifaa kimoja cha kufanyia tohara ya kimila.

“Wakati tunafanya tohara za kimila tulikuwa tunatumia kisu kimoja, vijana walikuwa wanatokwa damu nyingi. Kipindi cha nyuma kijana wa kiume akifanyiwa tohara akavuja damu nyingi akafariki, tulikuwa hatumziki, tulikuwa tunawatupa ili ukoo usipate laana”,ameeleza Mzee Marwa.

“Sasa hivi vijana wanaopata tohara hospitali/kwenye kituo cha afya hawatengwi kwenye jamii kama ilivyokuwa mwanzo ambapo kama kijana hajafanyiwa tohara ya kimila alikuwa anatengwa, anachekwa hali iliyosababisha baadhi ya vijana ili kuepuka kutengwa hata kama amefanyiwa tohara ya kitabibu alilazimika kufanyiwa tena tohara ya kimila. Sasa hivi hatutahiri mara ya pili, mambo ni shwari hivyo, waliofanyiwa tohara hospitalini na waliofanyiwa kimila wote ni sawa”,ameongeza Mzee huyo kutoka Serengeti.
Mhamasishaji wa masuala ya tohara salama kutoka kwa Wazee wa Kimila wilaya Serengeti, Charles Mwita.

Kwa upande wake, Mhamasishaji wa masuala ya tohara salama kutoka kwa Wazee wa Kimila wilaya Serengeti, Charles Mwita amesema wanaendelea kutoa elimu na uhamasishaji wa tohara kinga ya kitabibu kwa wazee wa kimila ili kukabiliana na maambukizi ya VVU kwani vifaa vinavyotumika katika tohara ya kimila vinachangia maambukizi ya VVU.


“Kupitia PEPFAR tumewapa elimu na kuwaaminisha wazee kuhusu tohara salama. Hata tohara za kimila zinazoendelea tunawapa vifaa vya kufanyia tohara salama. Kwa kweli Serengeti imebadilika, itaendelea kubadilika na hatimaye jamii itaachana kabisa na tohara za kimila”,ameeleza Mwita.


“Tohara ya kimila ni hatari, hebu fikiria kisu kimoja kilikuwa kinatumika kuwafanyia tohara vijana 1000, damu nyingi zinatoka hapo tutakwepaje maambukizi ya VVU?...Sasa hivi jamii imebadilika sana, imefikia hatua hadi baadhi ya vijana waliofanyiwa tohara ya kinga ya kitabibu hospitalini wanafanyiwa sherehe kama walivyokuwa wanafanyiwa sherehe vijana waliofanyiwa tohara ya kimila kwenye jamii. Haya ni mafanikio makubwa tunayoweza kujivunia kupitia PEPFAR”,ameongeza Mwita.

Naye Mratibu wa Tohara Wilaya ya Serengeti Dkt. Mary Yohana Kisiri amesema wakati wanaanzisha huduma ya tohara ya kitabibu mwitikio ulikuwa mdogo lakini sasa mwitikio ni mkubwa ambapo licha ya wanaume kupata huduma ya tohara kinga kwenye jamii kupitia Mkoba, wengi wamekuwa wakifika kwenye vituo vya afya kupata huduma hiyo bure.
Mratibu wa Tohara Wilaya ya Serengeti Dkt. Mary Yohana Kisiri.

“Tunaishukuru Serikali ya Marekani kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuleta huduma ya tohara bure kwa wanaume katika vituo vya afya na hospitali. Mwitikio ni mzuri, kwa mfano tangu mwaka 2021 mpaka sasa jumla ya vijana 7832 wamepatiwa huduma ya tohara kinga katika wilaya ya Serengeti”,anaeleza Dkt. Kisiri.

“Mwanzo vijana waliopata tohara kinga ya kitabibu walikuwa wanapata changamoto ya kunyanyapaliwa, lakini sasa unyanyapaa umepungua. Wazee wa kimila wanatoa ushirikiano mkubwa , hata ikitokea kijana aliyefanyiwa tohara ya kimila akapata changamoto wanashiriki kumleta hospitali. Tunashukuru wazee wa mila pia wanawaleta vijana kupata tohara salama”,amesema Dkt. Kisiri.

Kwa upande wake, Mratibu wa UKIMWI wilaya ya Serengeti, Dkt. Damas Ngwegwe anaishukuru Serikali ya Marekani na Serikali ya Tanzania kwa hatua walizochukua kukabiliana na maambukizi ya VVU katika jamii ikiwa ni pamoja na kutoa huduma ya tohara kinga kwa wanaume.

“Tumekuwa tukitoa elimu ya kubadili jamii, mwitikio ni mzuri. Jamii imekuwa na utaratibu wa kufanya tohara za kimila, vijana walikuwa wakifanyiwa tohara ya kimila wanafanyiwa sherehe na sisi tukaanzisha sherehe kwa vijana waliofanyiwa tohara kinga ya kitabibu/tohara salama. Mambo yanaendelea kuwa mazuri”,amesema Dkt. Ngwegwe.

Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Zabron Masatu, kupitia PEPFAR mpaka sasa wamefanikiwa kuwafanyia tohara kinga ya kitabibu wanaume wapatao 63,000 mkoani humo ambapo hayo yote yanatokana na uhamasishaji wa tohara ya kitabibu inayotolewa bure kwa wanaume ikiwa ni juhudi za kukabiliana na maambukizi ya VVU.

Mhamasishaji wa masuala ya tohara salama kutoka kwa Wazee wa Kimila wilaya Serengeti, Charles Mwita akielezea kuhusu tohara salama kwa wanaume
Mratibu wa UKIMWI wilaya ya Serengeti, Dkt. Damas Ngwegwe akizungumzia masuala ya tohara kinga za kitabibu
Mratibu wa UKIMWI wilaya ya Serengeti, Dkt. Damas Ngwegwe akizungumzia masuala ya tohara kinga za kitabibu
Mratibu wa Tohara Wilaya ya Serengeti Dkt. Mary Yohana Kisiri akielezea kuhusu huduma ya tohara kinga/tohara salama kwa wanaume
Bango likionesha huduma zinazotolewa katika Hospitali ya Wilaya ya Serengeti Mkoani Mara
Muonekano wa mbele Hospitali ya Wilaya ya Serengeti Mkoani Mara

Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger