Sunday, 7 June 2026

VIJANA NA WASOMI MKOANI MWANZA WAHIMIZWA UZALENDO NA UJASIRIAMALI KATIKA KONGAMANO

...
Na Mwandishi Wetu

​Katika jitihada za kuimarisha chachu ya maendeleo, Kongamano la Wasomi lililoandaliwa na Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Seneti Mkoa wa Mwanza, limefanyika leo, Juni 07, 2026, katika Chuo cha Uvuvi Nyegezi, likilenga kuwajengea vijana uwezo katika nyanja za uongozi, uchumi, afya, na itikadi ya chama.

​Akizungumza katika kongamano hilo, Mgeni Rasmi ambaye ni Mwenyekiti wa Vyuo na Vyuo Vikuu Seneti Mkoa wa Mwanza, Kenneth Geremia, amewasisitiza vijana kuonesha mapenzi ya dhati kwa Chama Cha Mapinduzi. Kiongozi huyo mwenye maono mapana, amewataka wanachama kudumisha mshikamano na ushirikiano imara baina ya matawi yote ndani ya mkoa wa Mwanza ili kujenga chama chenye nguvu zaidi.

​Katibu wa Vijana UVCCM Kata ya Luchelele, Omary Msuya, aliyekuwa mratibu wa hafla hiyo (MC), ametoa wito mzito kwa kila kijana kufanya uwajibikaji na uzalendo kuwa kipaumbele chao cha kwanza katika ujenzi wa taifa, akisisitiza kuwa vijana ndio uti wa mgongo wa maendeleo.

​Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Vijana UVCCM Wilaya ya Ilemela, Salum Mtatulu, amewahimiza vijana kujitolea kwa hali na mali katika shughuli za kijamii na kisiasa, akibainisha kuwa uwajibikaji thabiti ndio msingi mkuu wa mafanikio ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

​Katika kipengele cha elimu ya afya, Dkt. Misana Mulemwa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Sekou Toure, ametoa elimu muhimu kwa vijana kuhusu umuhimu wa kulinda afya zao dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la damu, kisukali na maradhi ya moyo. Dkt. Mulemwa amewataka vijana kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza huku akisisitiza kuwa uzima wa kijana ndio nguvu ya uzalishaji taifa.

​Katika sekta ya uchumi, Pius Mtenya, mfugaji wa samaki kwa njia ya vizimba katika mtaa wa Sylvini, ameeleza namna mradi huo ulivyokuwa ukombozi wa kiuchumi kwa vijana wilayani Nyamagana. Mpenya, ambaye ni kielelezo cha mafanikio, amewahimiza vijana kuondokana na hofu na badala yake waunde vikundi ili kufaidika na mikopo yenye riba nafuu inayotolewa na serikali.

Nae, ​Mlezi wa Tawi Bi. Immaculata Ndalawa, ambaye ni Mwalimu katika Chuo cha Uvuvi Nyegezi, amewashauri vijana kuhudhuria mara kwa mara makongamano kama haya. Ndalawa amesema kongamano hizo zinawajengea uwezo wa kipekee vijana katika kuelezea na kusimamia vyema mafanikio ya serikali katika miradi ya maendeleo nchi nzima.

Pamoja na mambo mengine, Katibu Hamasa wa Kambarage SAUT, Perus Leonard, ametoa mwongozo kwa wanafunzi vyuoni kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii. Leonard, kijana mbunifu, amewataka vijana kugeuza mitandao hiyo kuwa fursa za kiuchumi kupitia uandaaji wa maudhui (content creation), biashara za mtandaoni, na kuanzisha asasi zisizo za kiserikali zitakazosaidia kutatua changamoto za kijamii kama vile kulea watoto yatima na utunzaji wa mazingira.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger