Thursday, 18 June 2026

NBS YAAHIDI KUENDELEA KUTOA TAKWIMU SAHIHI KUSAIDIA UTEKELEZAJI WA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 20250

...



Na Wellu Mtaki, Dodoma

OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema itaendelea kuhakikisha takwimu rasmi zinapatikana kwa wakati, kwa ubora unaohitajika na kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa ili kusaidia juhudi za maendeleo ya taifa katika kipindi chote cha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa NBS, Daniel Masolwa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali.

Amesema NBS ni miongoni mwa taasisi za serikali zinazoshiriki maadhimisho hayo kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma zake, majukumu yake pamoja na umuhimu wa takwimu rasmi katika maendeleo ya taifa.

Masolwa alisema kuwa takwimu rasmi zitakuwa nyenzo muhimu katika kufuatilia, kutathmini na kupima utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inalenga kuifikisha Tanzania katika uchumi wa dola trilioni moja na kuongeza ustawi pamoja na kipato cha wananchi.

Alieleza kuwa takwimu zenye ubora na zinazopatikana kwa wakati zinasaidia serikali, sekta binafsi, taasisi za utafiti na wadau mbalimbali kufanya maamuzi sahihi yanayochochea ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu.

Aidha, amesema kaulimbiu ya mwaka huu ya Wiki ya Utumishi wa Umma inayosema, “Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu,” imeipa NBS fursa ya kuendelea kuhamasisha wananchi kuhusu nafasi ya takwimu rasmi katika upangaji wa maendeleo, ugawaji wa rasilimali na ufuatiliaji wa utekelezaji wa mipango ya taifa.

Amefafanua kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu, Sura ya 351, NBS imepewa mamlaka ya kukusanya, kuchakata, kuchambua na kusambaza takwimu rasmi zinazotumika katika sekta mbalimbali za maendeleo nchini.

“Takwimu rasmi ni msingi wa upangaji wa maendeleo. Serikali, sekta binafsi, watafiti na wadau wengine hutegemea takwimu hizi katika kufanya maamuzi sahihi, kuandaa sera, kupanga bajeti na kupima matokeo ya mipango inayotekelezwa,” amesema.

Masolwa alitaja baadhi ya takwimu zinazozalishwa na NBS kuwa ni pamoja na takwimu za mfumuko wa bei zinazotolewa kila mwezi na kuonesha mwenendo wa bei za bidhaa na huduma nchini, hali inayosaidia kutathmini mazingira ya uchumi na gharama za maisha kwa wananchi.

Pia alisema ofisi hiyo huzalisha takwimu za Pato la Taifa (GDP) kwa vipindi vya robo mwaka ambazo huonesha thamani ya bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini, kiwango cha ukuaji wa uchumi pamoja na mchango wa kila sekta katika maendeleo ya uchumi wa taifa.

Kwa upande wa ajira, alisema NBS hutoa takwimu zinazoonesha hali ya soko la ajira, kiwango cha ukosefu wa ajira, idadi ya watu walio katika ajira na wale walio nje ya nguvu kazi, jambo linalosaidia katika uandaaji wa sera na mikakati ya kukuza fursa za ajira.

“Tunaendelea pia kuzalisha takwimu za kilimo, uzalishaji viwandani, biashara ya nje pamoja na takwimu za kijamii zinazotokana na Sensa ya Watu na Makazi. Takwimu hizi zinaonesha mwenendo wa idadi ya watu, mgawanyo wa umri, hali ya makazi na rasilimali watu iliyopo nchini,” amesema.

Aliongeza kuwa takwimu hizo ni muhimu katika kukokotoa viashiria mbalimbali vya maendeleo ikiwemo wastani wa pato la mwananchi, viwango vya umaskini, maendeleo ya sekta mbalimbali na hali ya uchumi kwa ujumla.

Akizungumzia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Masolwa alisema mafanikio ya utekelezaji wake yatategemea kwa kiasi kikubwa uwezo wa nchi kutumia takwimu sahihi katika kupanga, kufuatilia na kutathmini hatua zinazopigwa kuelekea malengo yaliyowekwa.

Alisisitiza kuwa katika dunia ya sasa inayotegemea maarifa na teknolojia, matumizi ya takwimu yamekuwa nguzo muhimu katika kufanya maamuzi yenye tija na kuongeza ushindani wa uchumi.

“Lengo la Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni kuwa na uchumi mkubwa zaidi unaotoa ustawi kwa wananchi. Ili kufikia malengo hayo tunahitaji jamii inayojifunza, inayozalisha maarifa, inayotumia ujuzi na inayofanya maamuzi kwa kuzingatia takwimu sahihi na zenye kuaminika,” amesema.


Amesema NBS itaendelea kuimarisha mifumo ya ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu ili kuhakikisha wadau wote wanapata taarifa sahihi zitakazosaidia kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger