Tuesday, 16 June 2026

TUNAYAKUMBUKA YA OKTOBA 29, HATUSHIRIKI MAANDAMANO- W/BIASHARA WA MWENGE

...

Na mwandishi wetu, Dar

Wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama Machinga pamoja na waendesha pikipiki za kubeba abiria maarufu kama bodaboda wa eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam wameweka msimamo mkali wa kutoshiriki maandamano yaliyopangwa na kuhamasishwa kufanyika Julai 07, 2026, wakisema hawatashawishiwa na mtu yeyote kujiingiza kwenye fujo hizo zinazoweza kuvuruga usalama na amani ya nchi.

Maamuzi hayo yamekuja baada ya kufanya vikao vya ndani na kukubaliana kulinda usalama wa maeneo yao ya kazi, msimamo unaotokana pia na hofu ya kurejea kwa athari kubwa zilizojitokeza wakati wa machafuko ya Oktoba 29, 2025. Katika kipindi hicho kibaya, wengi wakisema kuwa walipoteza ndugu na jamaa zao wa karibu huku biashara zikiharibiwa vibaya. Maduka mengi yalivamiwa, kuibiwa bidhaa zote na mengine kuchomwa moto na kusababisha hasara kubwa sana ya mitaji.

"Sisi wafanyabiashara wa Mwenge kwa kauli moja tunapinga maandamano yanayohamasishwa ya Tarehe saba Julai kwasababu hakuna faida ya maandamano haya hasa kwa tulivyojifunza katika maandamano yaliyopita ikiwemo kupoteza ndugu, marafiki na wengine biashara zao kuathirika kabisa. Sisi hiyo tarehe saba tutakuwa kwenye biashara zetu kama kawaida na tuiombe serikali kuimarisha ulinzi na usalama siku hiyo ya tarehe saba mwezi ujao." Amesema Bi. Tumaini Ulotu, mfanyabiashara soko la Mwenge.

Wafanyabiashara hao wameeleza pia namna ambavyo wao na familia zao walitaabika kupata mahitaji muhimu ya kibinadamu baada ya serikali kuweka amri ya kutotoka nje, waendesha bodaboda wengi wakikosa kipato kwa sababu hawakuweza kubeba abiria barabarani. Hali hiyo ilisababisha uhaba mkubwa wa chakula majumbani mwao na kuwaletea ugumu mkubwa wa maisha.

Kundi hili limesisitiza kuwa halitakubali kutumika kisiasa kwa ajili ya maslahi ya watu wachache wenye nia mbaya, wakitoa wito kwa vijana wote nchini kutokubali kurubuniwa na wanasiasa wanaotafuta umaarufu kwa kutumia nguvu kazi zao.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger