Thursday, 1 December 2022

UNESCO KUONGEZA UWEZO WA TAASISI ZA ELIMU YA JUU NA KATI KUTOA ELIMU YA STADI ZA MAISHA INAYOLENGA AFYA YA UZAZI, VVU/UKIMWI NA JINSIA KWA NJIA YA MTANDAO.

Mgeni rasmi Mhe. George Simbachawene, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) akisikiliza maelezo kuhusu Kozi mtandaoni ya Stadi za Maisha, VVU/UKIMWI na Jinsia kwa vyuo vya elimu ya juu na kati.

30 Novemba 2022, Lindi.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) imezindua kozi ya elimu ya stadi za maisha inayolenga Afya ya Uzazi, VVU/UKIMWI na elimu ya kuzuia ukatili wa kijinsia kupitia mtandao, kwaajili ya wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo vya kati.

Uzinduzi huu umefanyika tarehe 30 Novemba 2022 uwanja wa Ilulu mkoani Lindi, kwenye wiki ya maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani katika Kilele cha siku ya Vijana.

UNESCO kwa kupitia mradi wake wa “Haki zetu, Maisha Yetu, Mustakabali wetu” maarufu kama O3 Plus unaofadhiliwa na shirika la maendeleo la kimataifa la Sweden (SIDA) na mpango wa kudhibiti VVU wa Umoja wa Mataifa (UN Joint program on AIDS), inalenga kuhakikisha kwamba vijana waliopo kwenye vyuo vya elimu ya juu na elimu ya kati nchini Tanzania wanapata matokeo chanya ya afya, elimu, na usawa wa kijinsia kwa kupunguza maambukizi mapya ya VVU, mimba zisizotarajiwa na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Kwakuzingatia hili UNESCO inashirikiana na wadau mbalimbali katika kuongeza utoaji wa elimu ya stadi za maisha kwa kuzingatia umri, utamaduni na maadili kwenye suala la elimu ya afya ya uzazi kwa kina katika Taasisi za Elimu ya Juu na Elimu ya kati.

Kama sehemu ya mpango huu, UNESCO ikishirikiana na mashirika ya Umoja wa mataifa ya UNAIDS, UNFPA na ILO pamoja na Wizara husika (Wizara ya Elimu na Wizara ya Afya) na Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) na Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) vikiwemo pia vyuo vikuu (Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Chuo kikuu cha Iringa, Chuo kikuu cha Mt. Augustine na Chuo kikuu cha Dodoma) ilitengeneza kozi hii inayoweza kusomwa mtandaoni kupitia mfumo wa tehama wa chuo husika au simu ya mkononi. Kozi hii ilifanyiwa majaribio katika vyuo vikuu vinne (UDSM, SAUT, UoI na MUCE) mwaka 2021 ambapo zaidi ya wanafunzi 17,000 walijisajili na kusoma kozi hiyo.

Kwa kupitia majaribio haya, UNESCO ilipata mapendekezo muhimu ya kuzingatia katika kuboresha wa maudhui na mtindo wa uwasilishaji wa kozi kupitia mifumo ya tehama ya kujifunzia vyuoni. Michakato ya kuboresha kozi ilifanyika na kupelekea maboresho yaliyopendekezwa kufanyika kwa wakati.

Uzinduzi wa kozi ya mtandaoni ya elimu ya afya ya uzazi kwa kina inayozingatia stadi za maisha ni hatua muhimu ya kuboresha mazingira salama ya kujifunzia na kufundishia kwa Wanafunzi na Walimu wa Taasisi za elimu ya juu na kati. Wanafunzi watakaosoma kozi hii watapata uelewa na kujenga umahiri wa kukabiliana na changamoto zitakazojitokeza kwenye maisha yao wawapo vyuoni na hata baada ya kumaliza masomo hususani kwenye masuala ya VVU/UKIMWI, afya ya uzazi, jamii na uchumi.

Pia kijana atakayesoma kozi hii ataweza kufurahia maisha yake ya chuo na kuweza kufikia malengo yake ya elimu na kuweza kuchangia kwa ufanisi zaidi katika maendeleo ya nchi kama mhitimu wa elimu ya juu na kiongozi wa baadae.

Kozi hii imetengenezwa kwa maudhui na mtindo wa kuvutia ili kuwawezesha wanafunzi kuisoma kwa wepesi wakati wowote, mahali popote kwa ratiba yao wenyewe.

Katika kuchangia mipango ya Kitaifa ya sekta ya VVU/UKIMWI pamoja na Afya, baada ya kuzindua kozi hii TACAIDS kwa kushirikiana na wizara na wadau itaisambaza kwenye Vyuo vyote vya elimu ya juu na elimu ya kati nchini.

UNESCO katika kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora kama moja ya lengo la maendeleo endelevu inashirikiana na wadau wa elimu kuweka mazingira salama na jumuishi ya kusomea kwa wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu na elimu ya kati wa Tanzania, ili kufanikisha wanafunzi kumaliza safari yao ya elimu bila vikwazo.
Share:

TAKUKURU YASHIRIKIANA NA WADAU KUZIBA MIANYA YA RUSHWA, YATIA MGUU VIBANDA VYA BIASHARA MANISPAA YA SHINYANGA

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy  akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Desemba 1,2022
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy  akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Desemba 1,2022
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy  akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Desemba 1,2022


Na Kadama Malunde- Malunde 1 blog

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga imeendelea kushirikiana na wadau wa sekta za umma kudhibiti mianya ya Rushwa na kufanya uzuiaji rushwa katika miradi ya maendeleo.

Akitoa Taarifa ya TAKUKURU katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2022/2023 (Julai – Septemba 2022) leo Alhamisi Desemba 1,2022, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy amesema katika kipindi hicho walijikita katika kuziba mianya ya rushwa na kuzuia rushwa kwenye miradi ya maendeleo.


“Katika ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo TAKUKURU Mkoa wa hinyanga ilishirikiana bega kwa bega na watendaji wa Halmashauri zote za mkoa wa Shinyanga wanaousika na utekelezaji wa miradi ya maendeleo”,amesema Kessy.

Ameeleza ufuatiliaji ulihusisha kazi za kutembelea miradi na shughuli zote za ujenzi katika miradi yote inayotekelezwa inakuwa na thamani halisi na ubora unaotakiwa.

“Kwa kufanya hivyo miradi 28 yenye thamani ya shilingi Bilioni 11.5 (11,573,687,057/=) iliyotembelewa kwa kipindi cha robo ya kwanza ikiwemo ya iliyotembelewa na Mwenge wa Uhuru 2022 iliweza kukamilika kwa ufanisi na ubora na hivyo kupelekea miradi kuwa na thamani halisi ya fedha”,ameeleza.

Ameongeza kuwa, TAKUKURU pia imeendelea kushirikiana na wadau wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kuhakikisha kunakuwepo na mazingira mazuri ya kufanyia biashara ikiwemo kupangisha vibanda vya biashara kwa wafanyabiashara kwa bei nafuu.

“Tunataka kuhakikisha vibanda vinatumiwa na wafanyabiashara halisi waliogawiwa vibanda na siyo wafanyabiashara waliopewa vibanda kuwapangisha wapangaji wengine au kuviuza kwa bei kubwa na kupelekea uwepo wa mazingira magumu ya kufanya biashara yanayoweza kuathiri pato la mkoa na taifa na hivyo kupelekea mfumuko wa bei”,amesema Kessy.


Katika hatua nyingine ameitaja mikakati ya utendaji kazi wa TAKUKURU mkoa wa Shinyanga kwa kipindi cha Mwezi Oktoba hadi Desemba 2022 kuwa ni pamoja na kukamilisha majukumu yake kwa kujielekeza zaidi kwenye ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa madarasa ili kuhakikisha inatekelezwa kwa thamani halisi ya fedha iliyoletwa na serikali.

“Pia tutaendelea kutoa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa kwa wananchi kupitia Kampeni ya TAKUKURU inayotembea lengo likiwa ni kuwafikia wananchi walio maeneo ya ndani wanaoshindwa kufika TAKUKURU na kuwasaidia kutatua kero zao zinazowakabili hasa zinazohusiana na masuala ya rushwa”,ameongeza.
Share:

WAZIRI DKT MABULA ASIKITISHWA NA WATENDAJI WA SEKTA YA ARDHI IRINGA

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi mkoani Iringa wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji wa sekta ya ardhi katika mkoa huo jana. Sehemu ya watendaji wa sekta ya ardhi wakimsikiliza Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula (hayupo pichani) alipofanya ziara katika mkoa huo kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa huo jana. Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi mkoani Iringa wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji wa sekta ya ardhi katika mkoa huo jana (PICHA NA WIZARA YA ARDHI)

*************************

Na Munir Shemweta, WANMM IRINGA

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amesikitishwa na watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri za Manispaa na Wilaya ya Iringa kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kusababisha halamshauri hizo kushindwa kukusanya maduhuli ya serikali yatokanayo na kodi ya pango la ardhi.

Akiwa katika ziara ya siku moja mkoani Iringa Novemba 30, 2022 kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi, Dkt. Mabula alibaini uzembe wa baadhi ya watendaji wa sekta ya ardhi wakiwemo maafisa ardhi wateule kwa kushindwa kusimamia utoaji hati za ardhi na uingizaji milki za ardhi kwenye Mfumo wa Utunzaji Kumbukumbu za Ardhi kwa njia ya kielektroniki.

Amewataka maafisa ardhi wateule katika halmashauri hizo kujitathmini kutokana na kushindwa kwao kwenda na kasi ya serikali ya awamu ya sita ya kuhakikisha wananchi wanamilikishwa na kupatiwa hatimiliki za ardhi.

Aidha, Waziri wa Ardhi Dkt Mabula amewataka maafisa hao wa sekta ya ardhi katika halmashauri hizo mbili za mkoa wa Iringa kuhakikisha kufikia Desemba mwaka huu wa 2022 wawe wamewasilisha taarifa zao za makusanyo ya kodi ya pango la ardhi pamoja na hatua walizochukua kwa wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi.

"Maana hata idadi ya viwanja mlivyonavyo hamvijui hilo ni kosa, unawezaje kukaa bila kujua idadi ya viwanja vyako katika halmashauri yako. Nataka kabla sijaondoka hapa nijue idadi ya viwanja mlivyokuwa navyo ni vingapi, na vingapi vipo kwenye mfumo na kwa nini havijaingia kwenye mfumo kwa hundred percent" alisema Dkt Mabula.

Aliongeza kwa kusema kuwa, mtendaji wa sekta ya ardhi hajui idadi ya viwanja vilivyopo kwenye mfumo wa utunzaji kumbukumbu za ardhi anawezaje kudai madeni? na kubainisha kuwa wamiliki wa ardhi wanapotambulika kwenye mfumo inakuwa ni rahisi kwa watendaji kudai madeni.

"Huna idadi maalum ya viwanja na hujaingiza kwenye mfumo wa utunzaji kumbukumbu unawezaje kudai madeni? Alihoji Dkt Mabula

Amewataka wakurugenzi wa halmashauri katika mkoa wa Iringa kutimiza wajibu wao wa kuzisimamia sekta za ardhi kwenye halmashauri zao kwa kuwa idara za ardhi ni za kwao na si za wizara na kubainisha kuwa watendaji wa sekta ya ardhi ni chachu ya kutoa elimu katika masuala ya ardhi.

Katika ziara yake Dkt Mabula amekutana na watumishi wa sekta ya ardhi kutoka Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Iringa pamoja na wale wa halmashauri ya Manispaa na Wilaya ya Iringa lengo likiwa kuboresha utendaji kazi wa sekta ya ardhi. Mkoa wa Iringa unazo jumla ya halmashauri tano ambazo ni Manispaa ya Iringa, Mafinga Mji, Irinda DC, Kilolo DC na Mufindi DC.

Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO ALHAMISI DESEMBA 1,2022


Magazetini leo Alhamis December mosi 2022

















Share:

UTT YATOA ELIMU KWA WAJUMBE WA TFC SINGIDA



Afisa Mwandamizi Idara ya Masoko na Mawasiliano wa UTT AMAS Grace Ngailo akizungumza alipokuwa akitoa mada kwa wajumbe wa semina ya siku moja ya viongozi wa vyama vya ushirika nchini kabla ya kufanyika kwa mkutano skuu wa Shirikisho la Vyama vya ushirika Tanzania (TFC) Mkoani Singida.
Katibu Mtendaji wa Shirikisho la vyama vya ushirika Tanzania (TFC) Alex Domitius (aliyekaa) akimsakiliza Afisa Mwandamizi Idara ya Masoko na Mawasiliano wa UTT AMAS Grace Ngailo alipokuwa akiwasilisha mada kwa washiriki wa semina hiyo Mkoani Singida.

(PICHA NA; HUGHES DUGILO)
Share:

Wednesday, 30 November 2022

NDOTO ZANGU NA MPENZI WANGU ZIMETIMIA, NI KUPATA KAZI NA FAMILIA

Share:

WANAWAKE WANAOSUMBUKA KUPATA MTOTO, TUMIA NJIA HII

Share:

IDADI YA WAGONJWA YAONGEZEKA MLOGANZILA


Idadi ya wagonjwa wanaofika kupata huduma ya matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila imeongezeka kutoka 10854 kufikia 11188 kwa wagonjwa wa nje wakati wagonjwa wanaolazwa 793 hadi 1052 katika kipindi cha miezi miwili kuanzia Septemba hadi Novemba mwaka huu.

Ongezeko hilo limechangiwa na uboreshwaji wa huduma ikiwemo kuhamia kwa Kliniki ya Magonjwa ya Moyo (Cardiology) na Kliniki ya Mishipa ya Fahamu (Neurology) kutoka Muhimbili Upanga ambapo kwa sasa wataalamu wanapatikana muda wote Mloganzila.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya utoaji huduma katika Hospitali ya Mloganzila .

Prof. Janabi amesema pamoja kuhamia kwa kliniki hizo kutoka Muhimbili Upanga lakini Kliniki za Magonjwa ya Ngozi, Upasuaji, Usingizi na ganzi, Masikio, Pua na Koo zinaendelea kama kawaida na wataalamu wapo muda wote.

"Pamoja na kliniki hizo, pia kuanzia tarehe 1 Desemba Kliniki ya Magonjwa ya Sukari na Homoni itahamia hapa Mloganzila, wataalamu waliokuwa wanapatikana Upanga wote watapatikana Mloganzila" amesema Prof. Janabi

Ameeleza kwamba ongezeko hilo limekuja na changamoto ya usafiri, Magari yanayokuja Mloganzila kutoka sehemu mbalimbali yameanza kulemewa hivyo ametoa wito kwa wakala wa usafiri wa mabasi yaendayo kasi DART kuongeza idadi ya magari yanayofika Mloganzila ili kurahisisha huduma za usafiri.

Naye Bi. Marietha John ambaye ni ndugu wa mgonjwa anayehudhuria Kliniki ya Mishipa ya Fahamu ameshukuru uongozi wa MNH kwa kuhakikisha wataalamu wanapatikana muda wote na wagonjwa wanapata huduma kwa wakati.

"Mama yangu ana tatizo la kiharusi, anahudhuria hapa kliniki , kwa kweli nashukuru tunapata huduma nzuri na Mama anapata eneo kubwa na lenye utulivu la kufanyia mazoezi" ameeleza Bi. Marietha
Share:

RAIS DKT. SAMIA ATUNUKIWA SHAHADA YA UDAKTARI WA FALSAFA WA HESHIMA IKIWA NI SHAHADA YA UDAKTARI WA JUU KATIKA HUMANITIA NA SAYANSI JAMII .

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akitunukiwa Shahada ya Udaktari wa Falsafa wa Heshima ikiwa ni Shahada ya Udaktari wa Juu katika Humanitia na Sayansi Jamii na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Rais Mstaafu wa Awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete katika Mahafali ya Hamsini na mbili (52) ya Duru ya Tano ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City tarehe 30, Novemba, 2022. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akikabidhiwa Cheti mara baada ya kutunukiwa Shahada ya Udaktari wa Falsafa wa Heshima ikiwa ni Shahada ya Udaktari wa Juu katika Humanitia na Sayansi Jamii na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Rais Mstaafu wa Awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete katika Mahafali ya Hamsini na mbili (52) ya Duru ya Tano ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City tarehe 30, Novemba, 2022.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi pamoja na Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati wa Mahafali ya Hamsini na mbili (52) ya Duru ya Tano ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City tarehe 30, Novemba, 2022.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa katika Mahafali ya Hamsini na mbili (52) ya Duru ya Tano ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City tarehe 30, Novemba, 2022. Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Rais Mstaafu wa Awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika Mahafali ya Hamsini na mbili (52) ya Duru ya Tano ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City tarehe 30, Novemba, 2022. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda akizungumza katika Mahafali ya Hamsini na mbili (52) ya Duru ya Tano ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City tarehe 30, Novemba, 2022.Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Balozi Mwanaidi Sinare Maajar akizungumza katika Mahafali ya Hamsini na mbili (52) ya Duru ya Tano ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City tarehe 30, Novemba, 2022.Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof.William Anangisye akizungumza katika Mahafali ya Hamsini na mbili (52) ya Duru ya Tano ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City tarehe 30, Novemba, 2022.Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakiwa katika Mahafali ya Hamsini na mbili (52) ya Duru ya Tano ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City tarehe 30, Novemba, 2022.

(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)

*******************

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amevitaka Vyuo Vikuu nchini kutimiza wajibu wake wa kutoa mchango katika kuleta maendeleo ya Taifa.

Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wito mara baada ya kutunukiwa Shahada ya Juu ya Heshima ya Udaktari (Doctor of Letters Honoris Causa) ya Chuo Kikuu cha Dar es katika Mahafali ya 52 ya Chuo hicho yaliyofanyika Novemba 30, 2022 Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Rais ameongeza kuwa jukumu la Taasisi za elimu ya juu katika kuleta maendeleo ni kutoa elimu stahiki, kufanya tafiti na kutoa maoni katika mwenendo wa kulikuza na kuimarisha Taifa.

"Tangu kuingia madarakani Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa ikisisitiza kuwa elimu inayotolewa inapaswa kukidhi mahitaji ya jamii katika karne ya 21,"amesema Rais Samia

Ameongeza kuwa mbali ya kuongeza maarifa elimu inayotolewa katika Taasisi za elimu inapaswa kuwawezesha wahitimu kuwa na stadi zitakazowawezesha kujiajiri, kuajiriwa ama kuwa wajasiliamali na kuwa tayari kuchangia maendeleo ya Taifa wanapohitimu masomo.

Akizungumza katika Mahafali hayo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda amesema kuwa tayari Wizara imekamilisha Mapitio ya Sera na Mitaala na kwa sasa hatua inayofuata ni kuyawasilisha kwenye vikao vya ndani vya Serikali kabla ya mjadala wa wazi wa kitaifa kuhusu maoni na mapendekezo hayo.

Kuhusu uboreshaji wa elimu ya juu Prof. Mkenda amesema katika kujenga mazingira mazuri ya utoaji wa elimu ya juu, Serikali kupitia mradi wa HEET itatumia Dola za Kimarekani 425 sawa na fedha za kitanzania Bilioni 972 kupanua na kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika fani za kipaumbele cha Taifa.

Ameongeza kuwa Mradi unatekelezwa katika Vyuo Vikuu 14 vya Serikali,Taasisi 3 za Wizara zinazoshughulikia Elimu ya Juu na Taasisi 5 za Elimu ya Juu zilizopo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango.

Aidha, Prof. Mkenda amesema utekelezaji wa Mradi huo utaongeza udahili katika Fani za kipaumbele cha Taifa kutoka 40,000 mwaka 2020 hadi kufikia 100,600 mwaka 2026.

Kuhusu ufadhili wa masomo ya Elimu ya Juu, Waziri huyo amesema Serikali imekuwa ikiongeza bajeti ya Mikopo ya Elimu ya Juu mfululizo kila mwaka ambapo bajeti ya Mwaka wa fedha 2017/18 ilikuwa shilingi bilioni 427 lakini kwa Mwaka wa fedha 2022/23 bajeti hiyo imefikia Shilingi bilioni 654.

Ameongeza kuwa na kama hiyo haitoshi, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameanzisha ufadhili ujulikanao Samia Scholarship kwa lengo la kuhamasisha wanafunzi kusoma masomo ya sayansi na kwamba jumla ya shilingi Bilioni tatu zimetengwa kwa mwaka wa 2022/2023 kwa ajili ya wanafunzi 640.
Share:

WANAFUNZI WAFARIKI DUNIA AJALI YA MOTO KAHAMA


AJALI YA MOTO TENA SHINYANGA YAUA WATU WATATU – WANAFUNZI WAWILI KAMANDA MAGOMI AELEZA



Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Watoto watatu wa familia moja ya Bwana Mathayo Samson katika mtaa wa Igomelo kata ya Malunga Manispaa ya Kahama wamefariki Dunia kufuatia ajali ya moto.

Tukio hilo limetokea leo Novemba 30, 2022 majira ya saa kumi na moja alfajiri ambapo moto uliunguza Nyumba ya Mathayo Samson na kusababisha vifo vya watu watatu wakiwemo wanafunzi wawili.

Akizungumzia ajali hiyo Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi wa Polisi Janeth Magomi ambaye ameeleza juu ya tukio hilo huku akithibitisha vifo vya watu watatu waliofariki katika ajali hiyo ya moto.

“Leo tarehe 30 mwezi wa 11 ilikuwa majira ya saa kumi na moja asubuhi katika mtaa wa Igomelo kata ya Malunga Manispaa ya Kahama Mkoa wa Shinyanga Nyumba ya ndugu Mathayo Samson anaumri wa miaka 39 na mfanyabiashara Nyumba yake iliwaka moto na madhara yaliyosababisha ni vifo vya watu watatu”.amesema Kamanda Magomi

Waliofariki katika ajali hiyo ni Dotto Juma mwenye umri wa Miaka 33 mkulima, Samson Mathayo mwenye umri wa Miaka 13 mwanafunzi wa darasa la sita shule ya msingi ST. Antony of Padua pamoja na Joseph Samson mwenye umri wa miaka 7 mwanafunzi wa darasa la pili shule ya msingi ST. Antony of Padua.

Kamanda Magomi amesema jeshi hilo kwa kushirikiana na jeshi la zimamoto na uokozi limefanikiwa kufika katika eneo la tukio na kwamba jeshi la polisi linaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha moto huo.
Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMATANO NOVEMBA 30,2022










Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger