
Na Deogratius Temba
Matumizi ya jani la “sale” katika jamii ya Wachaga mkoani Kilimanjaro yameendelea kutajwa kuwa moja ya mila zinazochochea na kuficha vitendo vya ukatili wa kijinsia, huku baadhi ya wananchi wakidai kuwa utaratibu huo wa kuombana msamaha umegeuka kinga ya watuhumiwa wa ubakaji na unyanyasaji wa watoto.
Tuhuma hizo zimeibuliwa na wananchi pamoja na wadau wa kupinga ukatili wa kijinsia wakati wa mafunzo yaliyoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kupitia mradi wa kuimarisha mifumo ya jamii katika kupambana na ukatili wa kijinsia na kulinda haki za wanawake na watoto, yaliyofanyika katika maeneo ya Mabogini (Moshi DC), Kalenga (Iringa DC) na Mgagao (Mwanga DC).
Washiriki wa mafunzo hayo walieleza kuwa mila ya kutumia jani la “sale” pamoja na “ngiambii” jani dogo linalotambaa ardhini kuashiria kuombana msamaha katika jamii ya Kichaga, imekuwa ikitumika vibaya kumaliza kesi za ukatili wa kijinsia nje ya mfumo wa sheria.
Mchungaji wa kanisa la TAG, Mabogini, Lidyia Materu alisema mila hiyo awali ilikuwa sehemu ya maridhiano ya kifamilia katika migogoro ya kawaida, lakini sasa imeanza kutumiwa hata kwenye makosa ya jinai ikiwemo ubakaji na ukatili dhidi ya watoto.
“Mila hii imekuwa hatari sana kwa sababu watu wanaamini wataomba msamaha na suala litakwisha. Unakuta mtuhumiwa ameshakamatwa lakini kesho yake familia zote zimekaa pamoja zinakunywa mbege, jani la sale linawekwa pembeni, halafu wanaambiwa ‘tumeshapatana’,” alisema Mchungaji Materu.
Kwa mujibu wa Jamii ya wachaga, matumizi ya mila hiyo yamechangia familia nyingi kushindwa kufikisha kesi kwenye vyombo vya sheria kwa kuhofia kuvunja mshikamano wa kifamilia au kijamii.
Mila na ukimya wa jamii
Katika mjadala huo, wananchi walikiri kuwa jamii imekuwa sehemu ya tatizo kwa kufumbia macho vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuhalalisha baadhi ya tabia kandamizi kupitia mila na desturi.
Mjumbe wa Kamati ya MTAKUWWA Kata ya Mabogini, Elizabeth Chuwa, alisema jamii imefikia hatua ya kuona udhalilishaji wa wanawake kama jambo la kawaida.
“Unaweza kuona vijana wakimdhalilisha mwanamke barabarani na watu wote wanakaa kimya. Hakuna anayekemea kwa sababu jamii imezoea,”
Anakazia zaidi kwa kusema hali hiyo imejenga mazingira ya ukimya hata kwa makosa makubwa kama ubakaji wa watoto.
“Mtoto anabakwa lakini jamii inanyamaza. Watu wanaona ni jambo la kifamilia badala ya kosa la jinai,”
Uchambuzi wa wadau unaonesha kuwa baadhi ya mila ambazo hapo zamani zilikuwa na lengo la kuleta maridhiano ndani ya jamii, sasa zimekuwa zikikinzana na sheria za kisasa na haki za binadamu, hasa pale zinapotumiwa kuficha uhalifu.
Kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 na Sheria ya Makosa ya Kujamiiana (SOSPA), makosa ya ukatili wa kijinsia ni makosa ya jinai yasiyoweza kumalizwa kwa maridhiano ya kifamilia au kimila.
Aidha, Tanzania ni mwanachama wa mikataba ya kimataifa ikiwemo Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kutokomeza Aina Zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW) na Mkataba wa Haki za Mtoto, ambayo inaitaka jamii kuhakikisha wanawake na watoto wanalindwa dhidi ya ukatili na kunyimwa haki.
Maridhiano yanayotajwa kuficha uhalifu
Mwanasheria kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Kilimanjaro, Wakili Bora Mfinanga, anasema kwamba baadhi ya maridhiano ya kimila yanaambatana na vitendo vya rushwa.
“Haiwezekani mtu apewe pombe, fedha au mifugo halafu ikaelezwa kuwa ni msamaha wa kimila. Huo ni mchakato unaozuia haki,”
Anasisitiza kuwa sheria za Tanzania haziruhusu kesi za ubakaji au ukatili dhidi ya watoto kumalizwa kwa makubaliano ya kifamilia.
Kwa upande wake, Mratibu wa Dawati la Jinsia Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, SP Asia Matauka, anasema amii ina wajibu wa kutoa taarifa mapema badala ya kuficha matukio kwa kisingizio cha mila.
“Kesi za ukatili wa kijinsia hazipaswi kunyamaziwa wala kumaliziwa nyumbani. Manusura wanapaswa kulindwa na kupewa haki zao,” anasema.
Watoto na Wasichana wazidi kuwa hatarini
Katika majadiliano na jamii ya kata ya mabogini, walieleza kuwa ukimya wa jamii umechangia watoto wengi kubaki kwenye mazingira hatarishi, huku baadhi ya wazazi wakihofia aibu na hivyo kushindwa kutoa taarifa.
Katika Kata ya Mabogini na Tarafa ya Kibosho kwa ujumla matukio mbalimbali ya ubakaji na unyanyasaji wa watoto yalitajwa kuhusisha watu wanaofahamika ndani ya jamii, lakini hatua zikidaiwa kutokuchukuliwa ipasavyo.
Huku wakitolea mifano ya kesi za ubakaji kadhaa katika kata ya mabogini na Kibosho kati ambazo hazikufanyiwa kazi ipasavyo na watuhumiwa waliokamatwa kuachiwa huru.
Aidha, viongozi wa jamii walikosoa kuongezeka kwa vilabu vya pombe za kienyeji na baa holela, hali inayotajwa kuongeza mazingira ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Kiongozi mmoja wa kijiji cha Chekereni ambaye hakutaka kutajwa jina alisema watoto wengi wameanza kuathirika kutokana na kuishi karibu na mazingira ya ulevi na biashara ya ngono.
“Watoto wanaona kila kitu hadharani. Wapo vilabuni hadi usiku na jamii imekaa kimya kana kwamba ni kawaida,” alisema.
Afisa ustawi wa jamii wa Kata ya Mabogini, Kunti Hutta, analazea suala la ulinzi wa Watoto kwa kusema kwamba jamii inapaswa kuweka mifumo madhubuti ya ulinzi kwa watoto wa kike, hasa wanafunzi wa sekondari.
“Wasichana wengi wanabaki mitaani hadi usiku baada ya masomo. Lazima wazazi, shule na jamii kwa ujumla wawajibike kuhakikisha wanakuwa salama,”
Wito wa kubadili mila zinazoumiza jamii
Mwezeshaji wa mafunzo kutoka TGNP, Deogratius Koyanga, alisema jamii ina wajibu wa kuchambua mila zake na kuona zipi zinafaa kuendelea na zipi zinapaswa kubadilishwa kwa maslahi ya haki na usalama wa wanawake na watoto.
“Mila ni sehemu ya utamaduni wetu, lakini hazipaswi kutumika kuzuia haki. Jamii lazima ikubali kujadili kwa uwazi mila zinazochochea ukatili wa kijinsia,” anasisistiza Koyanga.
Kauli za wadau wanaotekeleza mnyororo wa kutokomeza Ukatili wa Kijinsia zinaonesha kuwa vita dhidi ya ukatili wa kijinsia haviwezi kufanikiwa bila jamii yenyewe kukubali kubadilika.
Wadau wanaamini kuwa kuendelea kutumia mila kama jani la “sale” kuficha makosa ya jinai kunadhoofisha sheria, kunyamazisha manusura, na kuendeleza mzunguko wa ukatili katika jamii.
0 comments:
Post a Comment