
Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (Mb), leo tarehe 6 Mei, 2026 amefungua rasmi Mkutano Mkuu wa Pili wa Mwaka wa Jumuiya ya Wataalamu wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma (AAPAM), unaowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta hiyo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), Waziri Ridhiwani alisisitiza umuhimu wa wataalamu wa Rasilimali watu katika kuimarisha utendaji na ufanisi wa taasisi za umma ambapo alibainisha kuwa mchango wao ni muhimu katika kufanikisha utoaji wa huduma bora ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kiutawala na kiteknolojia.
Aidha, alieleza kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wataalamu hao ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi.
.jpg)
Katika ziara yake katika mabanda ya maonesho yanayoambatana na mkutano huo, Mhe. Ridhiwani alitembelea banda la Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), ambapo alipata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na taasisi hiyo pamoja na maboresho ya huduma zake.
.jpg)
Meneja Masoko na Uhusiano kwa Umma TEMESA Bi Martha Joachim akimkabidhi zawadi Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (Mb)
Akiwa katika banda hilo, aliipongeza TEMESA kwa kumpata Mtendaji Mkuu mpya, nakusema hatua hiyo imeashiria fursa ya kuimarisha zaidi uongozi, kuongeza ubunifu na kuleta matokeo chanya katika utoaji wa huduma kwa umma.
“TEMESA kwanza nawapongeza kwa kupata mtendaji mpya naamini mabadiliko haya yataleta chachu ya kiutendaji na utoaji wa huduma bora hongereni sana.” Amesema Mhe. Ridhiwani.

Mkutano huo wa siku nne umebeba kaulimbiu isemayo: “Kufikiri upya utoaji wa huduma kwa umma: Jinsi Serikali inavyoweza kutumia teknolojia kuanzisha huduma bora na zinazomlenga mwananchi, kukabiliana na ukosefu wa ajira kwa vijana pamoja na changamoto za mazingira.”
0 comments:
Post a Comment