Na Bora Mustafa, Karatu.
Serikali imesema itaendelea kuwalinda wawekezaji wa ndani pamoja na kuunga mkono uwekezaji unaofanywa na Watanzania kwa lengo la kuboresha huduma za kijamii na kukuza uchumi wa nchi.

Akizungumza leo Mei 29, 2026 na Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Lameck Karanga, wakati wa uzinduzi wa kituo kipya cha mafuta cha Orxy kinachoendeshwa chini ya Kampuni ya Halyaz.
Karanga amesema ujenzi wa kituo hicho ni muendelezo wa maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wawekezaji wa ndani wanapatiwa mazingira rafiki ya kufanya biashara na kuendelea kuchangia maendeleo ya taifa.
Amesema Wilaya ya Karatu ni lango muhimu la utalii nchini, hivyo uwepo wa kituo hicho utarahisisha upatikanaji wa nishati kwa wasafirishaji pamoja na wadau wa sekta ya utalii. Aidha, amesema bidhaa za kampuni ya Orxy zimeendelea kuaminika katika ukanda wa Afrika na duniani kwa ujumla.
"niwapongeze kwa uwekezaji huu. Mbali na kutuletea kituo bora cha mafuta, mmeanza kwa kutengeneza mazingira mazuri ya bustani mbele ya kituo chenu, jambo linaloonesha namna mlivyojipanga kuleta thamani kwa jamii," amesema Karanga.
Amesema usafi wa mazingira uliooneshwa na kampuni hiyo ni mfano wa kuigwa na taasisi nyingine pamoja na wadau wa biashara katika wilaya hiyo. Hata hivyo, amesisitiza kuwa mazingira safi ni sehemu ya kuimarisha utalii na kuvutia wageni wanaotembelea Karatu.
Aidha, Karanga amewataka wananchi pamoja na wafanyabiashara wa Karatu kuiga mfano wa Kampuni ya Halyaz kwa kuanzisha miradi ya uwekezaji itakayosaidia kuongeza ajira kwa vijana na kuchangia mapato ya Serikali kupitia kodi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Halyaz, Ally Abdulrazak, amesema ujenzi wa kituo hicho umetokana na maono ya kuhakikisha Karatu inapata huduma bora za nishati zinazokidhi mahitaji ya wananchi na wageni wanaofika katika eneo hilo.
Amesema kampuni hiyo iliamua kuingia ubia na Orxy kutokana na ubora wa mafuta yake pamoja na uaminifu ambao kampuni hiyo imeujenga kwa muda mrefu katika soko la nishati.
Abdulrazak amesema wateja watakaopata huduma katika kituo hicho watanufaika na huduma zenye viwango vya kimataifa kwa kuwa wafanyakazi wake wamepatiwa mafunzo ya kutosha na huduma zote zinaendeshwa kwa kuzingatia ubora.
"Nina kituo kingine katika mji wa Moshi. Wateja wetu, hususan wa sekta ya utalii, wamekuwa wakituuliza mara kwa mara wanapoweza kupata huduma za mafuta katika ukanda wa Karatu, jambo lililotusukuma kufungua kituo hiki," amesema.
Ameongeza kuwa malengo ya Kampuni ya Halyaz ni kuuza zaidi ya lita 10,000 za mafuta kwa siku pamoja na kuendelea kupanua huduma za vilainishi kwa wateja wake.
Kwa upande wake, Meneja wa Fedha wa Orxy Tanzania, Greyson Francis, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, amesema uzinduzi wa kituo hicho ni sehemu ya mkakati wa Orxy wa kuendelea kusogeza huduma zake karibu na wananchi.
Amesema Orxy kwa sasa inafanya shughuli zake katika nchi 19 barani Afrika pamoja na kuwa na mtandao mkubwa wa vituo vya mafuta nchini Tanzania. Aidha, amesema kampuni hiyo inatarajia kuzindua vituo vingine viwili vya mafuta katika Jiji la Dar es Salaam katika siku za karibuni.
Uzinduzi wa kituo hicho unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma za nishati katika Wilaya ya Karatu, pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi wa eneo hilo kupitia ajira na shughuli nyingine za kijamii na kiuchumi.

0 comments:
Post a Comment