
Meneja wa taasisi ya Zidiup Mentorship John Waryuba Akizungumza na wafanyabiashara na wajasiriamali kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Iringa wakati wa kongamano hilo kubwa la wafanyabiashara na wajasiriamali ukumbi wa Gentle Hills Hotel Kongamano kubwa la
wafanyabiashara na wajasiriamali kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Iringa na wilaya zake limefanyika kwa mafanikio makubwa katikq ukumbi wa Gentle Hills Hotel tarehe 8 april 2026 chini ya uratibu wa programu ya Zidiup Mentorship, likiongozwa na Meneja wake, John Waryuba, huku mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Khery James.
Kongamano hilo limewakutanisha wafanyabiashara wakubwa, wajasiriamali wadogo pamoja na vijana waliopata nafasi ya kuuliza maswali kuhusu biashara, mikopo, teknolojia na maendeleo ya kiuchumi, ambapo viongozi na wataalamu walitoa majibu papo kwa papo mbele ya washiriki waliojitokeza kwa wingi.
Akizungumza katika kongamano hilo Mkuu wa Mkoa wa Iringa mheshimiwa Khery James ameipongeza Zidiup Mentorship kwa juhudi zake za kulea vipaji na kuwawezesha vijana kujitambua kupitia ubunifu na matumizi ya teknolojia.
Amesema vijana wa Tanzania wana uwezo mkubwa wa kufanya mambo makubwa ikiwa watapata majukwaa sahihi ya kuonesha vipaji vyao.
Mkuu huyo wa mkoa amefananisha maisha na maji yenye ladha inayotegemea maamuzi ya mtu mwenyewe, akisisitiza kuwa vijana wanapaswa kuwa na mtazamo chanya na kuamini kuwa changamoto zinaweza kuwa fursa za mafanikio iwapo wataamua kuzitazama kwa mtazamo wa maendeleo.
Katika hotuba yake Mkuu wa Mkoa Khery James amewahamasisha vijana kutumia teknolojia na mitandao ya kijamii kama nyenzo ya kujiletea maendeleo badala ya kuikimbia.
Amesema dunia ya sasa imebadilika na teknolojia imegusa kila sekta ikiwemo biashara, elimu, mawasiliano na uzalishaji, hivyo vijana wanapaswa kuitumia kimkakati ili kujitangaza na kuongeza kipato chao.
Ametoa mifano ya wafanyabiashara wanaouza bidhaa kupitia mitandao na kuwafikia watu wengi zaidi kwa muda mfupi, huku akieleza kuwa viongozi wa kisasa hutumia mitandao ya kijamii kusikiliza na kufahamu changamoto za wananchi.
Aidha amempongeza kijana Kelvin anayejishughulisha na ushonaji wa mabegi aliyegunduliwa kupitia Zidiup Mentorship, akisema hiyo ni ishara kuwa teknolojia inaweza kuwa daraja la mafanikio kwa vijana wengi.
Mbali na hilo, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka vijana wa Iringa kutumia rasilimali zilizopo mkoani humo kuongeza thamani ya bidhaa na kukuza uchumi wa mkoa.
Amesema Iringa ina fursa kubwa katika utalii kupitia Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, biashara ya mazao, usafirishaji na bidhaa za misitu, hivyo vijana wanapaswa kuwekeza katika ubunifu badala ya kuuza malighafi pekee.
Amesisitiza umuhimu wa kuongeza thamani ya mazao na mbao kwa kutengeneza bidhaa kama fenicha bora zitakazoongeza ajira na mapato kwa vijana wengi zaidi.
Pia ameahidi kuendelea kuwaunga mkono vijana kupitia mikopo, ubunifu, sayansi na teknolojia ili kuhakikisha wanapata nafasi ya kufikia ndoto zao za maendeleo.
Kwa upande wake, Meneja wa Zidiup Mentorship John Waryuba amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kukubali kushiriki katika kongamano hilo na kwa namna anavyoendelea kuwa karibu na vijana wa Iringa.
Waryuba amewahamasisha vijana na wajasiriamali wadogo kuanza biashara kwa kutumia mtaji mdogo walionao badala ya kusubiri mazingira makubwa, akisema mafanikio huanza na hatua ndogo.
Amesema kongamano hilo limekuwa jukwaa muhimu la kuwaunganisha vijana, wafanyabiashara na viongozi wa serikali kwa lengo la kujenga uchumi imara wa mkoa wa Iringa na kuwapa vijana matumaini mapya ya kujitegemea kupitia biashara, ubunifu na teknolojia
.jpg)

.jpg)


0 comments:
Post a Comment