Na,Naomi Milton Serengeti. Mwanamke mmoja aitwaye Penina Petro(20) mkazi wa Kijiji cha Nyamakendo wilayani hapa amefikishwa mbele ya mahakama ya wilaya ya Serengeti kwa kosa la kumfanyia ukatili mtoto mwenye umri wa miaka 6(jina limehifadhiwa). Mwendesha mashtaka wa Jamhuri Faru Mayengela mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa wilaya Ismael Ngaile alisema katika shauri la Jinai namba 5/2019 mshitakiwa anakabiliwa na kosa moja la utesaji wa mtoto kinyume na kifungu namba 169 A cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002. Mshitakiwa alitenda kosa hilo Januari 12…
Monday, 14 January 2019
BIBI ANUSURIKA KUFA AKIPAMBANA NA MAMBA AKIOGA ZIWA VICTORIA
Mkazi wa kitongoji cha Mwibale wilayani Serengeti, Chibona Matoyo (64) akihojiwa na Mwandishi wa gazeti la Mwananchi, Daniel Makaka (kushoto) baada ya bibi huyo kunusurika kifo kufuatia kushambuliwa na mamba alipokuwa akioga ndani ya Ziwa Victoria, wilayani humo.
Chibona Matoyo (64), mkazi wa Kijiji cha Kanyala Wilaya ya Sengerema, Mara amenusurika kifo baada ya kujeruhiwa na mamba wakati akioga katika Ziwa Victoria.
Katika tukio hilo lilitokea Alhamisi iliyopita, Chibona alivunjika mikono na kujeruhiwa paji la uso na sasa anapatiwa matibabu kwenye Kituo cha Afya Mwangika, Buchosa wilayani humo.
Akizungumza na Mwananchi jana, mama huyo mwenye watoto watano na wajukuu tisa, alisema wavuvi ndio waliookoa maisha yake baada ya kupiga kelele akiomba msaada.
“Walipoona napiga kelele walifika eneo la tukio na kunikuta napambana na mamba, walinisaidia kujinasua, walifanikiwa,” alisema.
Baada ya kupata taarifa za tukio hilo, mume wa Chibona, Ernest Majula (81) aliangua kilioakisema mkewe amepata kilema na kuiomba Serikali kuchukua hatua kuwadhibiti wanyama hao.
Mtoto wa mama huyo, Agnes Majula alisema wamekuwa na mazoea ya kwenda kuoga ziwani wakiamini kuwa kufanya hivyo ni vizuri zaidi kuliko majumbani mwao.
Daniel Makaka - Mwananchi
MSTAAFU ADAIWA KUUAWA KWA KUCHOMWA MKASI NA 'HOUSE BOY' WAKE
Tunsume Sakajinga (60), mkazi wa wilayani Temeke jijini Dar es Salaam ameuawa baada kupigwa na kitu kizito kichwani kisha kuchomwa na mkasi shingoni na mtu anayedaiwa kuwa kijana wake wa kazi za nyumbani.
Msemaji wa familia ambaye ni kaka wa marehemu, Kisa Mwankusye amelieleza Mwananchi kuwa mauaji hayo yametokea juzi Januari 12, 2019 saa tano asubuhi na kwamba marehemu alikutwa amechomwa mkasi shingoni na kupigwa na kitu kizito kichwani.
“Tulipata taarifa hizo saa tano asubuhi, jambo hili linaumiza sana kwa sababu lipo chini ya mikono ya polisi tunawaachia wao,” amesema Mwankusye.
Amesema dada yake alistaafu Desemba 31, 2018 na kwamba nyumbani alikuwa akiishi na kijana huyo.
Na Tumaini Msowoya, Mwananchi
ALIYEZINI NA DADA YAKE AKANA MAELEZO YA AWALI MWINGINE ASOMEWA SHTAKA LA MAUAJI.
Na,Naomi Milton Serengeti. Gabriel Nyantori(25) mkazi wa Kijiji cha Kibeyo wilayani hapa ambaye ni mshtakiwa katika shauri la jinai namba 138/2018 amekana maelezo ya awali mara baada ya kusomewa maelezo yake katika mahakama ya wilaya ya Serengeti. Mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa wilaya Ismael Ngaile mwendesha mashtaka wa Jamhuri Faru Mayengela kabla ya kusoma maelezo ya awali alimkumbusha mshitakiwa makosa yake . Mwendesha mashtaka alisema katika shauri hilo mshtakiwa anashitakiwa kwa makosa mawili kosa la kwanza ni Kuzini kinyume na kifungu 158(1)(a) cha kanuni ya adhabu sura ya 16…
MAHAKAMA KUU YATUPILIA MBALI KESI YA ZITTO KABWE NA WENZAKE
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeifuta kesi iliyofunguliwa na Kiongozi wa ACT Wazalendo na wenzake wa vyama vya upinzani waliyokuwa wakiitaka mahakama hiyo kuzuia kusomwa kwa Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa wakidai kuwa uko kinyume na katiba ya nchi.
Mahakama imetoa uamuzi huo leo Jumatatu, Januari 14, 2018 ambapo walalamikaji, Zitto na wenzake wamekubali maamuzi hayo na kusema sasa nguvu yao ni kwenda kuupinga muswada huo kwenye kamati za bunge.
Jaji Benhajo Masoud amesema Mahakama imeliondoa shauri hilo baada ya waombaji kuchanganya mashataka mawili kwa pamoja.
“Mahakama imeondoa shauri letu dhidi ya serikali kupinga muswada wa sheria ya vyama vya siasa na kifungu cha 8(3) cha sheria ya Haki na Wajibu ( BRADEA ) kwa sababu ya maombi hayo mawili kuunganishwa. Kufuatia uamuzi huo wa mahakama tumeagiza mawakili leo wafungue kesi mpya ya BRADEA.
“Tunaheshimu maamuzi ya mahakama na tunaamini mahakama imetenda haki. Hivyo tumeamua kurudi mahakamani kwa ombi moja la kupinga kifungu cha 8(3) cha sheria ya Haki na Wajibu. Kifungu hiki kinakiuka katiba kwa kuzuia mashauri ya kupinga miswada ya sheria. Mahakama ni chombo cha haki.
“Tutaendelea kuupinga muswada wa sheria ya kurekebisha sheria ya vyama vya siasa mbele ya kamati za bunge na ndani ya bunge. Muswada ukipita kuwa sheria kama ulivyo au kuwa mbaya zaidi, tutaupinga mahakamani tena. Hatutakata tamaa katika kudai haki,” amesema Zitto.
Picha : CHUO KIKUU MZUMBE CHAANZISHA SAFARI YA MABADILIKO WEZESHI KATIKA SEKTA YA AJIRA NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof.Lughano Kusiluka,akizungumza na Wahadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe waliohudhuria warsha ya mabadiliko katika Sekta ya ajira kwa manufaa ya Jamii Afrika Mashariki (TESCEA) inayoendelea Morogoro.
Mwezeshaji wa warsha hiyo kutoka nchini Kenya Prof. Charles Kingsburry akifafanua kuhusu mradi huo kwa Waandishi wa Habari.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe (Taaluma) Prof. Ganka Nyamsogoro akiwasisitiza washiriki umuhimu wa warsha hiyo katika kubadili mbinu za ufundishaji.
Baadhi ya washiriki wakiwa katika majadiliano.
Mratibu wa mradi wa TESCEA Dkt. Albogast Musabila akifafanua kuhusu mradi huo kwa Waandishi wa Habari.
Mwezeshaji toka Chuo Kikuu, Afrika Nazarene cha nchini Kenya Dkt. Kendi Muchungi akieleza umuhimu wa mpango huo na jinsi unavyoweza kunufaisha wasomi na Jamii zao.
Mratibu Msaidizi wa mradi wa TESCEA wa Chuo Kikuu Mzumbe Dkt. Jennifer Sesabo akitambulisha mpango wa mradi huo kwa Washiriki.
Washiriki wakifuatilia maelekezo yanayotolewa katika warsha hiyo inayoendelea Hoteli ya Morogoro.
Washiriki wa warsha ya TESCEA katika picha ya pamoja baada ya ufunguzi rasmi.
***
Chuo Kikuu Mzumbe kupitia mradi wake mpya wa ‘TESCEA’ kimeendesha warsha ya kuwajengea uwezo wahadhiri katika mbinu bora za ufundishaji zinazosaidia wanafunzi kuweza kujiajirika pindi wanapohitimu masomo yao ya elimu ya juu.
Akizungumza katika uzinduzi wa warsha hiyo inayoendelea katika hoteli ya Morogoro, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof.Lughano Kusiluka amesema Chuo Kikuu Mzumbe ni mahiri katika kufundisha masomo ya biashara na menejimenti na sasa kinakwenda hatua ya mbele zaidi kwakuwaandaa wahitimu wa ndani na hata nchi nyingine kutengeneza ajira kabla ya kuhitimu masomo yao.
Prof.Kusiluka ameeleza kuwa kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa waajiri dhidi ya wahitimu wa vyuo vikuu nchini na kuonekana kutokuwa na ujuzi wa kutosha na umahiri katika fani walizosomea pindi wanapotaka kuajiriwa.
Hivyo, Chuo Kikuu Mzumbe kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma na vyuo vikuu viwili kutoka Uganda (Uganda Martys na Gulu), pamoja na asasi za AFELT, LIWA, ASHOKA kutoka Kenya na INASP kutoka Uingereza, wameanza kwa kuwajengea wahadhiri ili kubadili mbinu za ufundishaji zitakazowawezesha wahitimu kuwa na maarifa, ubunifu na ujuzi zaidi kutambua na kutumia fursa zilizopo ili kutengeneza ajira au kuajiriwa.
Kwa upande wake mwezeshaji wa warsha wa asasi ya umoja wa Vyuo vikuu vinavyofundisha mbinu zinazohitajika katika kuboresha ufundishaji Afrika Mashariki (AFELT) na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Daystar cha Kenya Prof.
Charles Kingsburry, amesema ni muhimu sasa kubadili mfumo wa ufundishaji unaowafanya wahitimu kujua vitu kulingana na elimu wanayofundishwa darasani pekee na kwa kutegemea mitandao ya intaneti na badala yake mbinu mpya za ufundishaji ziwajenge katika ubunifu ,maarifa,mbinu na stadi halisia zitakazowawezesha kujiajiri wao na kuweza kuajiri watu wengine.
Hii ina lengo si tu la kuwafanya wahitimu kujua vitu tofauti bali kuwajenga kuwa watu tofauti wanaoleta mabadiliko chanya kwa jamii nzima na kujinufaisha wao na jamii zinawazunguka kupitia elimu waliyopata.
Naye mwezeshaji mwingine kutoka Asasi ya AFELT na mhadhiri wa Chuo Kikuu, Afrika Nazarene cha nchini Kenya Dkt. Kendi Muchungi amesema wahitimu wa Vyuo Vikuu vyote vya Afrika Mashariki hawatofautiani na wamekuwa wakikosa uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa na hivyo kushindwa kuisaidia jamii katika suala la ajira kupitia elimu waliyopata,badala yake wamekuwa wakitegemea kuajiriwa. Hivyo ni imani yake kuwa mpango huo utaleta mabadiliko kwa wahadhiri wa vyuo vikuu katika ufundishaji na kunufaisha jamii nzima ya Afrika Mashariki kupitia wasomi wachache.
Wakati huo huo mratibu wa Mradi wa ‘TESCEA’ kutoka Chuo Kikuu Mzumbe,Dkt.Albogast Musabila amesema pamoja na lengo kuu la mpango wa mradi huo la kuwajengea wahitimu uwezo wa kujiajiri na kuajiri,Chuo Kikuu Mzumbe kwa ushirikiano na wadau wa Sekta ya ajira, wahadhiri na wanafunzi kimeanza mchakato wa kukusanya maoni ya wadau kwa ajili ya kuandaa mapendekezo yatakayozingatiwa wakati wa kuboresha mitaala na kuanzisha mitaala mipya.
PAKA ATUMWA KAMA KIFURUSHI POSTA..ALIYETUMA ALIMWA FAINI
Bwana mmoja nchini Taiwan amepigwa faini baada ya kumsafirisha paka wake kama kifurushi kwa njia ya mawasiliano ya posta.
Kwa mujibu wa mtandao wa habari wa habari wa UDN bwana huyo mwenye miaka 33 aliyetambulika kwa jina lake la ukoo la Yang amepigwa faini ya dola za Taiwan NT$60,000 ( sawa na dola za Marekani 1,952) kwa kuvunja sheria ya Ulinzi wa Wanyama ya Taiwan.
Tukio hilo lilitokea wiki iliyopita ambapo bw Yang alimfungasha kwenye kifurushi paka wake aina ya Scottish fold kwenda kwenye kituo kimoja cha kuhifadhi wanyama nchini humo katika wilaya ya Banciao. Yang amedai kuwa hakuwana mahitaji tena ya kuendelea kumfuga paka huyo.
Kutokana na kosa hilo, alilipishwa faini ya ziada ya NT$30,000 kwa kuvunja sheria ya kuzuia na kupambana na magonjwa ya kuambukiza ya wanyama sababu wafanyakazi wa kituo cha wanyama alipopokela paka huyo waligundua kuwa hakupewa chanjo ya kichaa na kuzuia hasira kali.
Maafisa wa ulinzi wa wanyama wa mjini Taipei walifanikiwa kumnasa mtuma kifurushi hicho kupitia kampuni ya posta na mkanda wa kamera za ulinzi za polisi.Mamlaka ya ulinzi wa wanyama inasema paka huyo ana afya njema na baada ya uchunguzi zaidi anaweza kuchukuliwa na mmiliki mpya.
Baada ya kufanya uchunguzi wao, wakamtia mikononi mwao bw Yang ambaye alijitetea kuwa alijaribu kumgawa paka huyo bila ya mafanikio. Yang pia alidai hakuwa na muda wa kutosha wa kumuangalia mnyama huyo na kumtunza. Paka huyo pia ana matatizo ya kutembea baada ya kujeruhiwa, na licha ya kupatiwa matibabu kadhaa, yakiwemo ya kimila bado hali yake haijatengemaa.
Mkurugenzi wa mamlaka ya wanyama, Chen Yuan-chuan, amelaani vikali mkasa huo akisema: "Mnyama anaweza kupatwa na hali mbaya kwa kukosa hewa ndani ya kifurushi na kupandwa na ghadhabu pia hakukuwa na maji safi na salama."
Bw Yuan-chuan amewataka watu kufuata taratibu halali za kisheria pale wanapoona hawawezi tena kuendelea kuwatunza wanyama wao wa nyumbani.
Chanzo- BBC
KESI YA 'UCHOCHEZI' INAYOMKABILI ZITTO YAOTA MBAWA
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (mwenye nguo nyeusi) akiwa na viongozi wengine kutoka vyama vya upinzani leo katika Mahakama ya Kisutu.
Kesi ya 'uchochezi' inayomkabiili Mbunge wa Kigoma Mjini, Zito Zuberi Kabwe imeahirishwa mpaka Januari 29, itakapoitwa kwa ajili ya kwenda kusikilizwa.
Kesi hiyo ya Jinai namba 327 ya Mwaka 2018 inayomkabili Kiongozi huyo leo tarehe 14 Januari 2019 katika Mahakama ya Kisutu, Jijini Dar es salaam ilifika kwa ajili ya kutajwa na kutolewa maamuzi ambayo yalitolewa na Hakimu Mkazi, Janeth Mtega baaada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili .
Upande wa Mashtaka ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Adolf Kissima ulidai kwamba kesi hiyo leo ilikwenda kwa ajili ya kutajwa lakini upande wa mashtaka hawakuwa na jalada halisi la kesi hiyo.
Upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili wa Zitto, Steven Mwakibolwa uliikumbusha mahakama kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa na mahakama hiyo kupitia Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama, Huruma Shaidi na ilishapanga tarehe ya kuanza kusikilizwa, ambayo ni Januari 29, 2019.
Inadaiwa kuwa Oktoba 28,2018 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za makao makuu ya chama cha ACT Wazalendo, kiongozi huyo alitumia maneno yenye kuleta kuleta chuki miongoni mwa wananchi wa Tanzania dhidi ya Jeshi la Polisi.
Mbunge huyo alifikishwa Mahakama ya Kisutu kwa mara ya kwanza, Novemba 2, 2018, bado anaendelea na dhamana.
Chanzo:Bbc
SERIKALI YAPIGA 'STOP' BOMOA BOMOA KWENYE MAKAZI YASIYO RASMI
Rais, John Pombe Magufuli.
Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli ametoa fursa kwa wananchi waliojenga bila ya kufuata mipango miji na hawana hatimiliki za ardhi kufanyiwa urasimishaji wa makazi na kuelekeza kuwa wasibomolewe nyumba zao tena kwakuwa hayakuwa makosa yao kujenga maeneo hayo.
Hayo yamesema na Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maendeleo na Makazi, William Lukuvi, wilayani Simanjiro mkoani Manyara alipofanya ziara ya kusikiliza na kutatua migogoro ya ardhi kwa wakazi wa mji huo, ambapo amewataka wananchi wote wachangamkie fursa hiyo iliyotolewa na Rais.
Amesema kwamba Serikali ya awamu ya tano kuanzia sasa haitabomoa tena nyumba za wananchi waliojenga maeneo ya makazi yasiyo rasmi badala yake itarasimisha makazi holela.
“Serikali ya awamu ya tano inajali sana wananchi wake kwakuwa zamani wananchi ambao hawakujenga kwa kufuata mipango miji wangebomolewa nyumba zao, lakini kwa sasa imeanzisha mpango kurasimisha makazi holela na kuwapatia hati wananchi wote waishio mijini ili waishi katika makazi rasmi”, amesema Lukuvi.
Pamoja na hayo Lukuvi amewataka wananchi wote waishio mijini kuwa wazalendo kwa kurasimisha maeneo yao waweze kujipatia hati na ili walipe kodi ya pango la ardhi jambo ambalo litaiongezea Serikali mapato.
Chanzo:Eatv
TATIZO SUGU LA SIMBA NA YANGA LAITAFUNA AFRIKA
Klabu ya soka ya Simba inawakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa na tayari ipo katika hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa Afrika ikiwa inaongoza kundi D, baada ya kushinda 3-0 dhidi ya JS Saoura.
Pamoja na kuwakilisha nchi lakini, Simba inaacha manyanyaso kwa vilabu vingine vinavyoshiriki ligi kuu ya soka Tanzania bara ambavyo havijui lini vitacheza mechi zake dhidi ya klabu hiyo ambayo tangu ianze kucheza mechi za kimataifa imejikusanyia viporo takribani 6.
Wiki hii ambapo baadhi ya timu zitakuwa zinacheza mzunguko wa 21, Simba wao hawatakuwa sehemu ya ratiba hiyo ya ligi kuu kwani watakuwa wanajiandaa kwaajili ya mchezo wa pili wa hatua ya makundi dhidi ya AS Vita Club, utakaopigwa Januari 19 huko DR Congo.
Vinara wa ligi kuu msimu huu, klabu ya Yanga huenda wakawa hawafurahishwi na Simba kuwa na viporo vingi lakini msimu uliopita Yanga walifika hatua ya makundi ya Kombe la shirikisho Afrika na walikuwa na viporo kama ilivyo kwa Simba msimu huu.
AFRIKA
Kwa upande wa timu ziliopo kundi moja na Simba, Al Ahly nao wamecheza mechi 14 tu kati ya 17 ambazo timu nyingine zimecheza huku pia ikiwa haipo kwenye ratiba ya ligi wiki hii ambapo itasafiri kuifuata JS Soura ambayo imecheza mechi 16 kati ya 17 za ligi.
Kwa upande wa DR Congo, AS Vita Club wao wamecheza mechi 14 kati ya 15 za ligi. Nchini Afrika Kusini Mamelodi Sondowns ambao wapo kundi A klabu bingwa Afrika wamecheza mechi 13 pekee kati ya 17 ambazo tayari timu nyingine zimecheza.
Chanzo:Eatv
TRUMP AIONYA UTURUKI DHIDI YA WAKURDI
Vikosi vinavyoungwa mkono na Uturuki wako tayari kushambulia wapiganaji wa Kikurdi kaskazini mwa Syria.
Rais wa Marekani Donald Trump ametishia 'kuiangamiza Uturuki kiuchumi' iwapo taifa hilo litavishambulia vikosi vya wakurdi nchini Syria baada ya wanajeshi wa Marekani kuondoka Syria.
Katika ujumbe wake alioutuma kwenye mtandao wa kijamii Twitter, Trump amesema hakutaka Wakurdi kwa upande wao nao pia waichokoza Uturuki.
Vikosi vya Marekani vimepambana kwa ushirikiano na wanamgambo wa Kikurdi kaskazini mwa Syria dhidi ya kundi la Islamic State (IS).
Uturuki hatahivyo inatazama wapiganaji hao wa vitengo vya YPG kama magaidi.
Rais Recep Tayyip Erdogan amezungumza kwa hasira kuhusu Marekani kuliunga mkono kundi hilo, na kuapa kuliangamiza.
Chanzo:Bbc
SADC YATOA WITO WA SERIKALI YA MUUNGANO DRC
Muungano wa maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC, umetoa wito wa kuundwa kwa serikali ya muungano nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kufuatia mzozo uliokumba matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika mwezi uliyopita.
Afrika Kusini pia inaunga mkono wazo la kubuniwa kwa serikali ya muungano.
Hatua hii ya SADC inakuja siku moja baada ya mgombea wa upinzani katika uchaguzi mkuu uliyofanyika nchini Jamhuri ya kidemocrasia ya Congo kuwasilisha kesi katika mahakama ya katiba kupinga matokeo ya uchaguzi huo.
Martin Fayulu amesisitiza kuwa alishinda uchaguzi huo lakini tume ya uchaguzi ikamtangaza mshindani wake Felix Tshisekedi kuwa mshindi.
Chanzo:Bbc
FAHAMU KIKOSI BORA ZAIDI BARANI ULAYA 2018
England walifika nusu fainali katika Kombe la Dunia nchini Urusi mwaka 2018, lakini hakuna mchezaji hata mmoja wa timu hiyo ya taifa aliyejumuishwa kwenye kikosi bora cha wachezaji 11 Ulaya, chaguo la mashabiki kwa mwaka huo.
Ingawa kuna wachezaji watatu wanaocheza Ligi ya Premia kwenye kikosi hicho, hata nahodha wa England Harry Kane aliyeshinda tuzo ya mfungaji bora zaidi Urusi, hajajumuishwa.
Kiungo wa Liverpool Virgil van Dijk na wachezaji wawili wa Chelsea N'Golo Kante na Eden Hazard wamo kwenye kikosi hicho cha wachezaji XI.
Cristiano Ronaldo ni miongoni mwao, ambapo amejumuishwa kwa mara ya 13 sasa, na kuwa mchezaji aliyejumuishwa mara nyingi zaidi.
Mshambuliaji huyo wa Ureno ambaye sasa huchezea Juventus ya Italia, aliisaidia klabu yake ya zamani Real Madrid kushinda Kombe la Klabu Bingwa Ulaya kwa mara ya tatu mtawalia mjini Kiev, Ukraine mwezi Mei ambapo waliwalaza Liverpool.
Chanzo:Bbc
DE GEA KUWA KIPA BORA ZAIDI MAN UNITED??
David de Gea huenda akajijengea hadhi ya kuwa mlinda lango bora zaidi kuwahi kuichezea klabu ya Manchester United hasa baada ya ustadi wake Jumapili, kwa mujibu wa kaimu meneja wao Ole Gunnar Solskjaer.
Mhispania huyo mwenye miaka, 28, aliokoa mipira 11 na kuwawezesha United kuwalaza Tottenham 1-0 katika mechi iliyochezewa uwnaja wa Wembley.
Kwa mujibu wa BBC, katika miaka 11 aliyokuwa Old Trafford akiwa mshambuliaji, Solskjaer alicheza na magolikipa stadi kama vile Edwin van der Sar na Peter Schmeichel.
"Tumekuwa na magolikipa wazuri sana katika klabu hii na nafikiri kwa sasa anawatishia wote wawili Edwin na Peter katika nafasi hiyo ya kipa bora zaidi [kuwahi kuchezea United] katika historia," Solskjaer alisema.
De Gea aliokoa mipira 11 langoni katika mechi hiyo ya Ligi Kuu ya England na pia akawawezesha kumaliza mechi hiyo bila kufungwa.
Ushindi wao uliwawezesha United sasa kukamilisha ushindi wa mechi sita kati ya sita walizocheza chini ya Solskjaer.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uhispania alijiunga na United kutoka Atletico Madrid mwaka 2011 na ameshinda tuzo ya mchezaji bora klabu wa mwaka katika misimu minne kati ya mitano ya karibuni zaidi.
"Alifaa kudaka mipira kadha," Solskjaer alitania.
"Tulikuwa na mabeki wazuri na David nyuma yao mambo yalikwenda vyema ajabu. Unaruhusiwa kuwa na kipa mzuri.
"Nimecheza na magolikipa kadha wazuri sana. Tumekuwa na utamaduni wa kuwa nao na amekomaa na kukomaa hata zaidi. Alistahiki tuzo hiyo ya mchezaji bora wa mechi ya leo (jana)."
Solskjaer ameshinda mechi tano za ligi mfululizo akiwa na United matokeo ambayo sasa yamewawezesha kutua nafasi ya sita wakiwa sawa kwa alama na Arsneal walio nafasi ya tano, wakiwa mbele kwa wingi wa mabao.
United wamo alama sita pekee kutoka nafasi ya nne inayowezesha klabu kufuzu kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
"Bado tunaamini kwamba tunaweza kumaliza katika nne bora," alisema De Gea.
"Sisi ni United, tuna wachezaji wazuri na tunang'ang'ania kumaliza katika nne bora.
"Ilikuwa mechi nzuri sana, hata zaidi ukizingatia tulikuwa uwanja wa Wembley. Zilikuwa alama tatu muhimu sana. Ninafurahia sana uchezaji wangu na timu inacheza vyema sana pia, na kuunda nafasi na kucheza soka ya kushambulia zaidi.
"Tumecheza mechi tatu sasa mtawalia bila kufungwa, jambo ambalo ni zuri sana. Wachezaji wana furaha, na unaweza kuliona hilo uwanjani, wanachezaji wa kujituma sana, kama Manchester United."
TIMU 9 ZILIZOTOA VIPIGO VIKUBWA ZAIDI ENGLAND
Katika mchezo wa soka timu kufunga mabao ni jambo muhimu zaidi. Ukifanya hivyo ndio unashinda. Bila shaka kwamba kama unataka kuwa na uhakika wa kushinda kwenye kila mchezo wa soka, ukifunga mabao mengi zaidi ndiyo yanayokuwezesha kukufanya uwe mshindi.
Baada ya Manchester City kuonyesha kiwango cha juu na kufunga mabao 9-0 dhidi ya Burton Albion kwenye mchezo wa Carabao, hapa tunakuchambulia timu zilizowahi kupata ushindi mkubwa zaidi katika historia ya mchezo wa soka nchini England.
9. Manchester United 9-0 Ipswich (Machi 4, 1995)
Mashetani Wekundi hao waliibuka na ushindi wa mabao 9-0 dhidi ya Ipswich na hadi sasa imebakia kuwa rekodi kwenye zama za Ligi Kuu ya England.
Andy Cole alifunga mabao matano – akiweka rekodi ya kufunga mabao mengi kwenye mchezo mmoja wa Ligi Kuu, huku Roy Keane akifunga, Mark Hughes (mawili) pamoja na Paul Ince akifunga moja.
Kichapo hicho kilikuwa cha kushangaza kwa kuwa Ipswich iliichapa United 3-2 kwenye mchezo wa mwanzoni mwa msimu huo.
8. West Ham United 10-0 Bury (Oktoba 25, 1983)
Ushindi mwingine wa kushangaza ni kwenye mchezo wa Kombe la Ligi, wagonga nyundo hawa wa London walipata ushindi mkubwa zaidi katika historia yao.
Tony Cottee ambaye alikuwa na umri wa miaka 19 peke yake alitikisa nyavu mara nne, huku Trevor Brooking aliyekuwa na miaka 36 alifunga mawili dhidi ya Bury, ambao walikuwa vinara wa ligi daraja la kwanza na walikuwa wakipewa nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo.
7. Liverpool 10-0 Fulham (Septemba 23, 1986)
Huu ulikuwa ni mchezo wa Kombe la Ligi na wekundu hawa wa Anfield walitoa kichapo cha kihistoria.
Uwanja ukiwa na watazamaji 13,498 pale Anfield ulishuhudia Steve McMahon na Ian Rush wakiiangamiza Fulham. McMahon alifunga mabao manne, lakini alikosa penalti kwenye mchezo huo. Liverpool walitinga fainali ya Kombe la Ligi lakini wakaja kufungwa na Arsenal magoli 2-1.
6. West Brom 12-0 Darwen (Aprili 4, 1982)
Darwen FC ilikuwa ni timu kutoka pale mitaa ya Lancashire, ambayo ilionekana kuwa na matarajio makubwa kwenye soka la England.
Lakini walipokutana na West Brom kwenye Ligi Daraja la Kwanza wakajikuta wakikumbana na kipigo cha mabao 12-0.
5. Nottingham Forest 12-0 Leicester City (Aprili 21, 1909)
Nottingham Forest ilikuwa ni timu tishio wakati huo na walipokutana na Leicester waliitandika bila huruma mabao 12. Gwiji wa Forest na ambaye ndiye mfungaji wa wakati wote wa timu hiyo, Grenville Morris, alifunga mabao mawili kwenye mchezo huo.
4. Newcastle United 13-0 Newport County (Oktoba 5, 1946)
Wakati huo wakiwa wanacheza Ligi Daraja la pili, Newcastle walitoa kipigo cha aina yake, huku kipindi cha kwanza wakiongoza kwa mabao saba.
Mchezaji, Len Shackleton ambaye ndio alikuwa ametoka tu kujiunga na klabu hiyo kwa ada ya pauni 13,000, alifunga mabao sita peke yake na kuwafanya vijana hao kuondoka uwanjani wakiwa na shangwe kubwa.
3. Stockport County 13-0 Halifax Town (Januari 6, 1934)
Miaka 85 iliyopita Stockport waliweka historia kwenye soka la England ambao hawajawahi kuifikia tena hadi leo.
Stan Milton alikuwa akicheza mchezo wake wa kwanza kwenye Ligi Daraja la Tatu na hadi kipindi cha kwanza kinamalizika ubao ulikuwa unasomekana 2-0 Stockport wakiwa wanaongoza. Lakini kipindi cha pili Milton alifunga mabao 11 peke yake na kuweka historia yake kwenye mchezo huo hadi leo.
2. Clapton 0-14 Nottingham Forest (Januari 17 January 1891)
Forest waliweka tena historia nyingine. Huu ulikuwa mchezo wa raundi ya nne ya Kombe la FA wakaifunga Clapton mabao 14-0 na kujiandikia historia yao.
1. Preston North End 26-0 Hyde FC (Oktoba 15, 1887)
Hii ndio historia iliyoshindwa kuvunjwa hadi leo kwenye soka huko England na itachukua miaka mingi kuweza kuivunja.
Ni miaka 131 iliyopita, Preston wakiwa kwenye dimba la nyumbani waliifumua Hyde FC mabao 26-0 kwenye uwanja wa Deepdale ukiwa ni mchezo wa raundi ya kwanza ya Kombe la FA.
North End kwenye mchezo huo iliweka rekodi ya aina yake katika historia ya soka la Uingereza: Kufunga mabao mengi kwenye mchezo mmoja, kupata ushindi mkubwa zaidi nyumbani ambao ni rekodi hadi leo.
Cha kuchangaza licha ya ushindi huo mnono na kuweza kutinga fainali, lakini wakaja kufungwa na West Brom 2-1.
MATATANI KWA KUGAWA SARE ZA JESHI
Vyombo vya ulinzi na usalama mkoani Kigoma vimemtia mbaroni kiongozi wa Shirika la Danish Refugees Services linalotoa usaidizi wa huduma za kibinadamu kwa wakimbizi wa Burundi wanaohifadhiwa kwenye kambi za Nduta wilayani Kibondo na Mtendeli wilayani Kakonko.
Kiongozi huyo anatuhumiwa kuhusika na uingizwaji na uwagawaji wa nguo zinazofanana na sare za jeshi ndani ya kambi hizo za wakimbizi.
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Samson Anga akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Emmanuel Maganga wakati wa uchomaji wa nguo uliofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Kawawa mjini Kigoma, ambapo alisema kuwa kiongozi huyo anashikiliwa na vyombo vya ulinzi na usalama kwa uchunguzi zaidi.
Bila kumtaja jina kiongozi huyo, Anga amesema kukamatwa kwake kunatokana na Mkuu wa Makazi katika kambi ya Wakimbizi ya Nduta wilaya Kibondo kutilia shaka uwepo wa nguo hizo na mgawanyo wake.
Ndipo baada ya kufuatilia kwa kina akagundua kuwa nguo hizo zinafanana na sare za jeshi hivyo kuarifu kamati za ulinzi na usalama na nguo hizo kukamatwa kabla hazijaanza kugawanywa.
“Katika hatua ya awali tunamshikilia kiongozi wa Taasisi ya Danish Refugees Services ambaye kwa namna moja au nyingine anahusika na uingizwaji wa nguo 1,947 kwenye hizo kambi za wakimbizi na uchunguzi zaidi unaendelea, taarifa itatolewa baadaye kuhusiana na yale yanayoendelea kwenye suala hilo,” alisema.
Na Fadhili Abdallah - Habarileo Kigoma
KAULI YA KANGI LUGOLA KUHUSU VIDEO YA TRAFIKI KUMSHAMBULIA 'KUMNG'ATA MENO' DEREVA WA LORI
Wakati video inayoonyesha askari watatu wa Kikosi cha Usalama Barabarani wakimshambulia dereva wa lori ikizua mjadala mitandaoni, Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limesema litatoa tamko la tukio hilo haraka iwezekanavyo.
Katika video hiyo, askari hao wanaonekana wakimshambulia dereva huyo kabla ya kundi la wananchi waliokuwa wakiwashangaa awali, kuamua ugomvi huo.
Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola alisema, “Nimemtumia kipande hicho cha video Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Muslimu ili afuatilie kujua undani wake na taarifa itatolewa.”
Hata hivyo, alipotafutwa kwa simu jana, Kamanda Muslimu hakupatikana kwani simu yake iliita bila kupokewa.
Lakini akizungumza na Mwananchi jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Mathias Nyange alisema tayari wameshapewa maelezo na watatoa ufafanuzi kuhusu jambo hilo.
“Mimi mambo yote huwa yanatolewa ofisini kwa njia ya ‘Press’ (mkutano na waandishi wa habari) sio kwa njia ya simu hivyo mtafahamu ni kitu gani,” alisema.
Tukio hilo limeibua mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii kutokana na jinsi askari hao walivyotumia nguvu kubwa kumkamata dereva huyo ambaye haikufahamika mara kosa alilotendana alikokuwa akitokea au kuelekea.
Katika video hiyo, askari wanaonekana wakimshambulia dereva huyu katika jitihada za kutaka kumkamata na kumdhibiti lakini alionekana kufanikiwa kujinasua katika mikono yao.
Katika patashika hiyo, dereva huyo anasikika akipiga kelele kuomba msaada akilalamika kung’atwa shingoni na mmoja wa askari.
Baada ya kufanikiwa kutoka katika mikono ya askari dereva wa lori alionekana kukimbilia katika gari na kuchukua panga jambo ambalo liliwafanya watu kutimua mbio.
Na Aurea Simtowe, Mwananchi
Angalia video hapa chini
Angalia video hapa chini