Friday, 31 July 2026

WAKALA WA VIPIMO WAENDELEA KUTOA ELIMU YA MATUMIZI YA VIPIMO SAHIHI MKOANI NJOMBE

...

Njombe, Julai 31, 2026
 
Wakala wa Vipimo (WMA) wameendelea na kampeni ya utoaji elimu kuhusu matumizi ya vipimo sahihi kwa wafanyabiashara, wazalishaji na wadau mbalimbali wa biashara mkoani Njombe, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha biashara zinafanyika kwa uwazi, usawa na kwa kuzingatia sheria za vipimo.

Katika mwendelezo wa kampeni hiyo, leo Julai 31, 2026, timu ya WMA imefanya ziara katika maeneo mbalimbali ya shughuli za kiuchumi ikiwemo masoko, viwanda vya mbao, eneo la madalali wa viazi maarufu kama Chaugingi, pamoja na kiwanda cha kuchakata parachichi. Katika maeneo hayo, elimu ilitolewa kuhusu umuhimu wa kutumia vipimo sahihi ili kuhakikisha biashara inafanyika kwa usahihi na haki.

Wananchi na wafanyabiashara walipata fursa ya kufahamu kuwa matumizi ya vipimo sahihi huchangia kulinda maslahi ya mlaji na muuzaji, huongeza uaminifu katika biashara, hupunguza migogoro ya kibiashara na kuimarisha ushindani wa haki sokoni.

 Zoezi hilo liliongozwa na Kaimu Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Njombe, Bw. Shabani Ikingu, ambaye alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwafikia wadau wa biashara kwa elimu ili kuongeza uelewa kuhusu matumizi sahihi ya vipimo na wajibu wa kila mfanyabiashara kuzingatia matakwa ya sheria. Alibainisha kuwa utoaji wa elimu ni nyenzo muhimu katika kujenga utamaduni wa biashara unaozingatia uwazi, uadilifu na kulinda maslahi ya pande zote mbili katika biashara.

Hata hivyo  WMA imepanga kufanya semina maalumu kwa waheshimiwa madiwani, wakulima na wajasiriamali katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe tarehe 2 Agosti 2026.

Semina hiyo inalenga kuongeza uelewa kuhusu sheria za vipimo, kuimarisha ushirikiano kati ya WMA, viongozi wa serikali za mitaa na wadau wa biashara, pia kuhamasisha matumizi ya vipimo sahihi ili kujenga mazingira ya biashara yenye haki, ushindani usawa na yanayomlinda mlaji pamoja na mfanyabiashara.

WMA itaendelea kufikisha elimu hii katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira yake ya kuhakikisha vipimo vinavyotumika katika biashara vinakuwa sahihi kwa maendeleo ya biashara yenye uaminifu na ustawi wa uchumi.

#Vipimo Sahihi, Haki kwa Mlaji na Mfanyabiashara.







Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger