Monday, 13 July 2026

WIZARA YA ELIMU YAANZA MAGEUZI MAKUBWA KUJIBU MAHITAJI YA SOKO LA AJIRA

...



Na Dotto Kwilasa,Dodoma

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeanza utekelezaji wa mkakati mpya unaolenga kuifanya sekta ya elimu izalishe wahitimu wenye ujuzi, ubunifu na uwezo wa kushindana katika soko la ajira la ndani na kimataifa, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Mkakati huo unajumuisha maboresho ya mitaala, matumizi makubwa ya teknolojia ya habari na mawasiliano, ushirikishwaji wa sekta binafsi katika uwekezaji wa elimu pamoja na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa takwimu kwa ajili ya kupanga na kufanya maamuzi.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Caroline Nombo,amesema mafanikio yaliyofikiwa katika sekta ya elimu yanapaswa kuwa chachu ya kuharakisha mageuzi yanayolenga kuandaa rasilimali watu itakayokidhi mahitaji ya uchumi wa kisasa.

Akizungumza leo July 13,2026 kwenye Kikao cha mwaka cha Menejimenti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda,Prof.Nombo amesema sekta ya elimu ndiyo msingi wa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hivyo ni muhimu mipango yote ya wizara ikaendana na matarajio ya taifa ya kujenga uchumi unaotegemea maarifa, sayansi na teknolojia.

“Tumekutana kufanya tathmini ya tulikotoka, tulipo na tunapokwenda. Ni wajibu wetu kuhakikisha sekta ya elimu inatoa mchango mkubwa katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” amesema.

Profesa Nombo amesema moja ya maeneo yatakayopatiwa kipaumbele ni kupitia upya kozi na programu za elimu ili ziweze kujibu mahitaji halisi ya jamii na soko la ajira.

Amesema mjadala unaoendelea katika mitandao ya kijamii kuhusu kozi zinazofaa kusomwa na wahitimu wa kidato cha sita unaonyesha wazi kuwa jamii inahitaji mfumo wa elimu unaobadilika kulingana na mahitaji ya wakati.

“Mrejesho tunaoupata unatufanya tujitathmini na kuangalia aina ya kozi tunazotoa,tunahitaji kuongeza ubunifu na unyumbufu katika kuwapa wanafunzi fursa ya kusoma taaluma zinazojibu mahitaji ya maendeleo ya taifa,” amesema.

Aidha, ameagiza taasisi zote zilizo chini ya wizara kuhakikisha mifumo yao ya TEHAMA inaunganishwa na Mfumo wa Taarifa za Usimamizi wa Elimu (ESMIS) ili kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa takwimu na kurahisisha maamuzi ya kisera.

Amesema hatua hiyo pia inatekeleza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha mifumo ya Serikali inasomana na kufanya kazi kwa pamoja.

Katibu Mkuu huyo pia amesisitiza umuhimu wa kushirikisha sekta binafsi katika uwekezaji wa elimu ili kuongeza ubora wa huduma, kuimarisha miundombinu na kupanua fursa za kujifunza kwa Watanzania wengi zaidi.

Amesema pamoja na kuendelea kuboresha mitaala, wizara itaweka mkazo katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ili wahitimu wawe na maarifa na ujuzi unaokidhi mahitaji ya taifa na dunia.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Daniel Mushi, amewataka viongozi wa taasisi mbalimbali kuendelea kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu mafanikio yanayopatikana kupitia utekelezaji wa miradi na programu za Serikali katika sekta ya elimu.

Katika kikao hicho, viongozi wa wizara, wakurugenzi, wakuu wa vitengo na wakuu wa taasisi waejadili nafasi ya elimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma, mfumo wa ESMIS, Mpango Mkakati wa Wizara wa mwaka 2026/27 hadi 2030/31 pamoja na utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27.





Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger