
Na Elizabeth Cosmas - Shinyanga
Wananchi wa Mkoa wa Shinyanga wameendelea kutambua umuhimu wa ushirikiano wao na Jeshi la Polisi, wakieleza kuwa hatua hiyo imeongeza uhuru wa kutoa taarifa za kiusalama na kuchangia kwa kiasi kikubwa kupunguza vitendo vya uhalifu katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Baadhi ya wakazi wa Shinyanga wamesema ushirikiano uliopo kati ya wananchi na Jeshi la Polisi umeimarisha hali ya usalama na utulivu, huku ukiwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika kufichua na kuzuia vitendo vya uhalifu.
Mmoja wa wananchi hao, Tiffany Mswahili, mkazi wa Shinyanga, amesema hali ya kiusalama imeimarika tofauti na ilivyokuwa hapo awali, ambapo kwa sasa wananchi wamejengewa mazingira rafiki ya kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama bila hofu.
"Tunaweza kutoa taarifa za matukio ya kihalifu kwa uhuru zaidi kuliko zamani. Hii imeongeza imani kati ya wananchi na Jeshi la Polisi na imechangia kudhibiti uhalifu katika jamii," amesema Tiffany.
Akizungumza na Malunde Blog leo Julai 3, 2026, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Magomi, amesema ushirikiano wa wananchi ndiyo msingi wa mafanikio katika mapambano dhidi ya uhalifu, kwani huwezesha upatikanaji wa taarifa kwa wakati na kuchochea hatua za haraka pindi matukio yanapotokea.
Amesema Jeshi la Polisi limeendelea kuimarisha uhusiano wake na wananchi kupitia mikakati mbalimbali inayolenga kujenga imani, jambo ambalo limeongeza ufanisi katika kudhibiti uhalifu na kulinda usalama wa raia na mali zao.
Kamanda Magomi amesema mfumo wa Polisi Kata umeendelea kuleta matokeo chanya kwa kuwawezesha askari kuwa karibu zaidi na wananchi, huku wakishirikiana na viongozi wa maeneo husika, wakiwemo madiwani, wenyeviti wa mitaa na vijiji pamoja na watendaji wa kata, kutatua changamoto mbalimbali za kiusalama.
Aidha, amesema Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linaendelea kutoa elimu kwa umma kupitia njia mbalimbali ikiwemo semina mashuleni, mikutano ya hadhara, vijiwe vya bodaboda na majukwaa mengine ya kijamii, ili kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika kudumisha amani na usalama.
"Lengo letu kuu ni kulinda raia na mali zao. Hili haliwezi kufanikiwa bila ushirikiano wa wananchi wenyewe. Ndiyo maana tunaendelea kuweka mkazo katika utoaji wa elimu na kujenga ukaribu na jamii," amesema Kamanda Magomi.
Ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kuendelea kuimarisha ushirikiano na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na vitendo vyote vinavyoweza kuhatarisha usalama wa jamii, akisisitiza kuwa usalama ni jukumu la kila mwananchi.







0 comments:
Post a Comment