Sunday, 19 July 2026

KATAMBI: SERIKALI HAITAVUMILIA WANAOTUMIA HAKI ZA BINADAMU KAMA KIVULI CHA KUVURUGA AMANI

...


Na Mwandishi Wetu, Shinyanga

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amesema Serikali haitaruhusu kundi la watu wachache kutumia hoja za haki za binadamu na demokrasia kama kivuli cha kuvuruga amani na utulivu wa Tanzania, akisisitiza kuwa yuko tayari kufika mahakamani wakati wowote endapo ataitwa.

Katambi amesema kauli na vitendo vinavyochochea chuki, vurugu na machafuko haviwezi kuvumiliwa, huku akieleza kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wanaendelea kuishi katika mazingira ya amani na usalama.

Akizungumza nyakati tofauti na makundi ya walinzi wa amani katika jamii, Polisi Jamii, Sungusungu, wazee, wenyeviti wa mitaa, mabalozi na viongozi wa vitongoji mjini Shinyanga, Waziri huyo alisema wanaomtishia kumpeleka mahakamani wanafanya hivyo kutokana na kushindwa kufanikisha ajenda zao za kuhamasisha maandamano.

Katambi alisema kupotea kwa amani kuna madhara makubwa kwa uchumi wa nchi, ikiwemo kupungua kwa watalii, kukimbia kwa wawekezaji, kusimama kwa miradi ya maendeleo na kudhoofika kwa mahusiano ya kidiplomasia.

"Wanajua wakiichafua Tanzania yetu na amani ikapotea tutapoteza mvuto kwa watalii, nchi inaweza kuwekewa vikwazo, miradi mikubwa ya maendeleo itasimama, wawekezaji wataondoka na mapato muhimu ya taifa yataathirika," alisema Katambi.

Aidha, alihoji kwa nini wanaojinasibu kutetea haki za binadamu hawajawahi kukemea hadharani vitendo vya uchomaji wa shule, vituo vya mafuta, ofisi za Serikali, biashara za watu binafsi pamoja na mashambulizi dhidi ya vituo vya polisi.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, machafuko yanapoibuka waathirika wakubwa huwa ni wananchi wa kawaida, hususan wanawake, watoto, wazee na watu wenye ulemavu.

"Watoto wao na familia zao wako nje ya nchi, lakini machafuko yakitokea ni wananchi wa kawaida watakaobeba mzigo wake. Tanzania ndiyo nchi yetu pekee na hatuwezi kukubali ifikie hatua ya wananchi wake kuwa wakimbizi," alisema.

Katambi alitolea mfano baadhi ya nchi za ukanda wa Afrika zilizowahi kukumbwa na migogoro, akisema Tanzania imekuwa ikiwahifadhi wakimbizi kwa miaka mingi, hivyo hakuna sababu ya kuruhusu mazingira yanayoweza kuisukuma nchi katika hali kama hiyo.

Kuhusu madai ya kuvunja Katiba, Waziri huyo alisema Mahakama ndiyo chombo pekee chenye mamlaka ya kutoa uamuzi kuhusu tafsiri na uvunjifu wa Katiba, na si watu binafsi au taasisi nyingine.

Alisema hadi sasa hajapokea wito wowote wa kwenda mahakamani, lakini akisisitiza kuwa yuko tayari kuitikia wito huo wakati wowote, hata usiku wa manane, kwa kuwa anaamini katika utawala wa sheria na kuheshimu mamlaka ya Mahakama.

Katambi alihitimisha kwa kuwataka Watanzania kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kulinda amani, akisisitiza kuwa utulivu wa nchi ndiyo msingi wa maendeleo, uwekezaji na ustawi wa wananchi.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger