Friday, 4 July 2025

SINGIDA YAANDIKA HISTORIA:TRILIONI 1 7 ZAFUNGUA MILANGO YA MAENDELEO

...



Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Mkoa wa Singida umeandika historia mpya ya maendeleo kwa kutumia zaidi ya shilingi trilioni 1.72 katika kipindi cha miaka mitano (2020/21–2024/25), fedha ambazo zimetumika kufanikisha utekelezaji wa miradi ya kijamii na kiuchumi katika sekta mbalimbali, ikiwemo kilimo, elimu, afya, miundombinu na utawala bora.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 4, 2025 jijini Dodoma, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, amesema mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa kupitia fedha kutoka Serikali Kuu, mapato ya ndani ya halmashauri pamoja na michango ya wadau wa maendeleo. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 1.055 zilitolewa na Serikali Kuu moja kwa moja, huku utekelezaji wa bajeti kwa kipindi hicho ukiwa wastani wa asilimia 95.

 “Kuongezeka kwa rasilimali fedha kumewezesha Singida kuimarisha ustawi wa wananchi kupitia ajira, kipato na upatikanaji wa huduma bora, hususan katika sekta ya kilimo ambacho kinategemewa na zaidi ya asilimia 80 ya wakazi wa mkoa wetu,” ameeleza Dendego.

Amebainisha kuwa katika kipindi hicho pato la ndani la mkoa (Regional GDP) limeongezeka kutoka shilingi trilioni 2.709 mwaka 2020/21 hadi trilioni 3.398 mwaka 2024/25, hali ambayo imeongeza pia pato la mtu mmoja kutoka shilingi 1,588,604 hadi 1,710,562. Aidha, mapato ya ndani ya Mamlaka ya Mapato (TRA) mkoani humo yameongezeka kwa zaidi ya asilimia 150, kutoka shilingi bilioni 11.9 hadi bilioni 30, huku mapato ya halmashauri yakipanda kutoka bilioni 14.6 hadi 24.8.

Katika sekta ya kilimo na ufugaji, mkoa umefanikiwa kujitosheleza kwa chakula kwa kuongeza uzalishaji kutoka tani 649,850 hadi tani 1,325,201 kwa mwaka, huku usajili wa wakulima kupitia mfumo wa M-Kilimo ukiongezeka kwa asilimia 289, kutoka wakulima 75,398 hadi 293,385.

Pia matumizi ya pembejeo bora yameimarika ambapo matumizi ya mbolea yameongezeka kutoka tani 1,772 hadi tani 7,948, sawa na asilimia 348.4, na matumizi ya mbegu bora yakiongezeka kwa zaidi ya asilimia 123. Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 81 kwa ajili ya miradi ya umwagiliaji, ambapo hekta 17,437 kati ya hekta 48,619 zinazofaa tayari zinatumika kupitia skimu rasmi 24.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger