Tuesday, 8 July 2025

MTEMI MAKWAIA WA III AHIMIZA UPENDO KUWA NI NGUZO YA MAENDELEO BUSIYA

...

Chifu wa Utemi wa Busiya Faustine Makwaia wa III akizungumza kwenye sherehe za tamasha la utamaduni la Sanjo ya Busiya katika viwanja vya Ikulu ya utemi huo uliyoko Ukenyenge Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Julai 7,2025

Na Sumai Salum – Kishapu

Mtemi Faustine Makwaia Makani (Makwaia wa III) wa Utemi wa Busiya, uliopo katika kata kumi za Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga, ametoa wito kwa wakazi wa utemi huo pamoja na jamii zingine kuenzi na kuishi kwa upendo, akisema kuwa upendo ni silaha muhimu ya kuondoa chuki na kuleta maendeleo katika familia, jamii, na taifa kwa ujumla.

Akizungumza Julai 7, 2025, katika kilele cha Tamasha la Utamaduni wa Kisukuma “Sanjo ya Busiya”, lililofanyika kwenye viwanja vya Ikulu ya Busiya Ukenyenge, Mtemi huyo amesisitiza kuwa hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana bila kuwa na upendo na maono ya pamoja.

"Tukiwa na upendo ndipo maendeleo yatakuwepo Kknyume cha upendo ni chuki, na tunafahamu kuwa pale panapokuwepo chuki hakuna maendeleo kwa kuwa hakutakuwepo na maono ya pamoja, hivyo tupendane ili tushirikiane kwa nia moja ya kukuza utemi wetu wa Busiya kwa kipindi chote nitakachoongoza," amesema Mtemi Makwaia wa III.

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi, amewataka wananchi waliopata mbegu zilizobarikiwa katika Tamasha hilo kuzitumia kwa tija msimu ujao wa kilimo, ili kuboresha uchumi wa kaya zao.

"Ndugu zangu, niwapongeze kwa sherehe hizi nzuri na zilizofana. Wote mtakaochukua mbegu hizi zilizobarikiwa hakikisheni mnalima kwa wingi na baada ya kuvuna, watoto wasome na familia zenu zinufaike kwanza la sivyo mkiitumia kwa anasa zisizo na tija kwa familia fedha hizo zitakuwa laana badala ya baraka," amesema Masindi.

Mhe.Masindi amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, anayejulikana pia kwa jina la heshima la “Chifu Hangaya”, itaendelea kuhimiza jamii kuenzi na kudumisha tamaduni zao nzuri.

Tamasha hilo la Sanjo ya Busiya limehusisha mashindano ya ngoma na muziki wa asili kutoka ndani na nje ya Wilaya ya Kishapu, maonesho ya vyakula vya asili ya Kisukuma, pamoja na mashindano ya mavazi ya asili na geni rasmi akiwa ni Mtemi Makwaia wa III, ambaye pia ametoa zawadi kwa vikundi vyote vilivyoshiriki ngoma, wanawake walioonesha mavazi ya asili na waliotayarisha vyakula vya na vyombo mbalimbali vya asili ya Kisukuma.


Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe.Peter Masindi (kulia) akizungumza kwenye tamasha la utamaduni la Sanjo ya Busiya lililofanyika Julai 7,2025 katika viwanja vya ikulu ya utemi huo Ukenyenge Wilayani humo huku mgeni rasmi wa sherehe hizo akiwa ni Faustine Makwaia Makani(Makwaia wa III).




















































Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger