Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Katika juhudi za kuimarisha utoaji wa huduma serikalini na kutekeleza ndoto ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhamisha ofisi za wizara na taasisi katika Mji wa Serikali Mtumba, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi, amezitaka taasisi zote husika kuongeza kasi ya usimamizi na kuhakikisha kazi za ujenzi wa majengo yanakamilika kwa wakati.
Akizungumza jijini Dodoma alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo 34 ya wizara na taasisi katika Mtumba, Lukuvi amesisitiza kuwa licha ya fedha zote muhimu kutolewa, kuna baadhi ya wakandarasi ambao bado wanachelewesha kukamilisha miradi yao, jambo ambalo linapaswa kusitishwa haraka.
“Ujenzi huu ni kipaumbele cha serikali yetu ya Awamu ya Sita, na tunataka uendelee kwa kasi. Tunatakiwa kuhakikisha majengo yote yanakamilika kabla ya Oktoba 2025 ili kufanikisha malengo ya kuwahamisha watumishi na kuleta mabadiliko ya kiutendaji serikalini,” amesema Lukuvi.
Mradi huu una gharama ya jumla ya shilingi bilioni 738, na hadi sasa ujenzi umekamilika kwa asilimia 92.2. Mratibu wa Kikosi cha Kuhamishia Serikali Mtumba, Noeli Mlindwa, ameongeza kuwa serikali imeshatoa shilingi bilioni 544.7 kwa ajili ya ujenzi na tayari majengo 10 yamekamilika na yanatumika kwa huduma kwa wananchi.
Lukuvi pia alisisitiza umuhimu wa kuzingatia matumizi ya samani na vifaa vinavyotengenezwa ndani ya nchi, akitoa mfano wa Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo tayari imehamia Mtumba kwa kutumia fanicha za mbao za ndani.
Katika ziara hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA), Mhandisi Benjamini Maziku, aliripoti kuwa ujenzi wa barabara kilomita 51 ndani ya mji huo umekamilika, pamoja na ufungaji wa taa za barabarani na kamera za usalama.
Aidha, serikali imepanga kupanda miti zaidi ya 253,000 katika mji mzima ili kuufanya Mtumba kuwa mji wa kijani na rafiki kwa mazingira.
Ziara ya Waziri Lukuvi ni sehemu ya mikakati ya serikali kuhakikisha mji wa Mtumba unakuwa kituo cha kiutendaji chenye miundombinu imara na huduma bora kwa wananchi, kulingana na malengo ya serikali ya sasa.






0 comments:
Post a Comment