Na Hadija Bagasha Tanga,
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Burian amewataka wakazi Mkoani Tanga kujiepusha na vitendo vyote vinavyoashiria uvunjifu wa amani katika kipindi hiki ambacho Taifa linaelekea katika Uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi Mkuu baadae mwakani.
Balozi Dkt. Batilda ametoa wito huo Septemba 22,2024 katika kilele cha tamasha kubwa la Utalii wilayani Lushoto la USAMBARA TOURISM FESTIVAL lililofanyika kwa siku mbili katika viwanja vya Nyerere Square, ambapo amesema ni jukumu la kila mwanatanga kuhakikisha amekuwa sehemu ya amani na utulivu kuanzia kipindi hiki ambacho wananchi wameanza kujiandikisha katika daftari la mpiga kura ili kupata nafasi ya kuchagua viongozi makini watakao waongoza na kuwaletea maendeleo ya kweli.
Katika hatua nyingine Balozi Dkt. Batilda amewataka waratibu na wasimamizi wa uchaguzi kuhakikisha wanaweka juhudi katika kutoa elimu na kuwashirikisha wananchi wa ngazi zote ikiwemo viongozi wa kimila na waandishi wa vyombo vya habari katika kutoa elimu ya uchaguzi.
Awali akizungumzia Utalii Dkt.Batilda amesema Wilaya ya Lushoto imebarikiwa kwa vivutio mbalimbali vya utalii na hivyo kuwa sehemu ya kichocheo cha maendeleo na kupongeza uongozi wa Wilaya ya Lushoto kufanikisha ujenzi wa kituo cha utalii ambacho kitasaidia upatikanaji wa taarifa muhimu za utalii.
Amewaelekeza viongozi wa Wilaya zingine za Mkoa wa Tanga kuwa na vituo vya utalii ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa kwa wageni wanaotembelea maeneo hayo.
Akizungumza kwa niaba ya Benki ya NMB Meneja Mahusiano wa Benki ya NMB na Serikali Peter Massawe amesema Benki hiyo ipo katika mchakato wa kusaidia sekta ya Utalii kwa kukaa na watenda kazi wa Sekta hiyo na kuona wanauhitaji wa mambo gani na kiasi gani ili kushirikiana kwa pamoja kukuza Sekta hii.
Tamasha la Usambara Tourism Festival limefanyika kwa mara ya kwanza Wilayani Lushoto na kuhusisha shughuli mbalimbali ikiwemo kutembelea vivutio vya utalii, maonesho ya biashara, shughuli za taasisi mbalimbali na kufanyika kwa mbio Usambara Marathoni kwa washiriki wa Km 21, Km 10 na KM 5 mbio zilizo ongozwa na mkuu wa Wilaya ya Lushoto Zephania Sumaye
0 comments:
Post a Comment