Wednesday, 18 September 2024

MKOA WA TABORA TUMEPIGA VITA MAFUNDI UMEME VISHOKA”-RAS TABORA

...
Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt John Mboya, akizungumza wakati akifungua semina ya siku moja kwa mafundi umeme wa mkoa huo, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora,Paul Matiko Chacha, leo Septemba 17,2024.
Meneja wa EWURA Kanda ya Magharibi, Mha. Walter Christopher akizungumza na wadau wa sekta ndogo ya umeme wakiwamo mafundi, wakandarasi na wawakilishi wa taasisi mbalimbali wakati wa semina ya kuwajengea uwezo mafundi umeme wa mkoa wa Tabora.



MAFUNDI umeme wakimsikiliza Katibu Tawala wa Tabora, Dkt John Mboya wakati wa semina kuhusu utekelezaji wa sheria na kanuni za ufungaji umeme za mwaka 2022 iliyoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) mkoani Tabora.

Na.Mwandishi Wetu

Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt John Mboya, akifungua semina ya siku moja kwa mafundi umeme wa mkoa huo, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora,Paul Matiko Chacha, leo 17 Septemba 2024,amewasihi mafundi umeme wote mkoani humo kuhakikisha wanakuwa na leseni za ufungaji mifumo ya umeme zinazotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kwa mujibu wa Kifungu cha. 8 (h) cha Sheria ya Umeme,Sura Na. 131.

“Kuanzia leo, mkoa wa Tabora tumepiga vita mafundi vishoka, na ni imani yangu kwamba baada ya semina hii kila asiye na leseni ataomba leseni ili afanye kazi kwa uhalali, ninawasihi sana tusipoteze fursa hii kwani mkoa wetu una miradi mingi ambayo ni fursa kwa mafundi umeme na kuanzia sasa vishoka wote hawatapewa kazi mpaka pale watakapokuwa na leseni ya EWURA,” alisema.

Meneja wa EWURA Kanda ya Magharibi, Mhandisi Walter Christopher, alisema semina hiyo iliyowashirikisha mafundi umeme na wadau zaidi ya 150, ililenga kuwajengea uwezo wataalam na wadau hao kuhusu sheria, kanuni, miongozo na utaratibu wa utendaji kwenye shughuli za ufungaji wa mifumo ya umeme.

Wadau wengine walioshiriki semina hiyo ni Wakala wa Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Wakala wa Majengo (TBA) na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA).

Mafundi umeme wanaweza kuomba leseni kupitia mfumo wa LOIS unaopatikana kwenye tovuti ya EWURA www.ewura. go.tz na kupakua fomu ya kukamilisha ufungaji mifumo ya umeme katika tovuti hiyo hiyo au kuwasiliana na EWURA kwa simu 0800110030, mitandao ya kijamii au barua pepe; info@ewura.go.tz.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger