Sunday, 21 January 2024

MAKONDA AWATUMIA SALAMU WATUMISHI WAZEMBE TANGA

...

 













Na Oscar Assenga, TANGA

KATIBU wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Paul Makonda amewatumia salamu watumishi wa Serikali wazembe mkoani Tanga wasiowajibika kwamba hawatakubali kuwavumilia kwa sababu wao ndio wamekuwa chanzo cha kumchonganisha Rais na wananchi wake.

Alitoa kauli hiyo wakati alipozungumza na wananchi kwenye mkutano wa Hadhara kwenye viwanja vya Lamore Jijini Tanga mara akitokea wilayani Pangani akiwa kwenye ziara yake ya kichama mkoani hapa.

Alisema kwamba chama hicho hakiwezi kukubali kuwafumbia macho watumishi ambao wamekuwa wakishindwa kuwajibika huku wananchi wakiendelea kuteseka wakati wanapokwenda kupata huduma katika maeneo yao.

Makonda alisema moja kati ya maelekezo kumi aliopewa na Rais Samia baada ya kupendekezwa na hatimae kuteuliwa ni kuwa sauti ya wananchi wa hali ya chini na wasio na pesa vyeo wala elimu .

Alisema Serikali imekuwa na utaratibu wa kutoa fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kimaendeleo na wajibu wa chama ni kuhoji miradi hiyo inatekelezwa kwa wakati na iendane na thamani ya fedha zilizotengwa.

"Nina maelekezo kumi toka kwa Rais Samia,moja ni kuhakikisha je miradi inajengwa kwa wakati?kazi yangu na wenzangu kushughulika na wanaofanya ubadhilifu wa fedha hizo"Alisema Makonda.

Aidha alisema katika ziara yake ya siku mbili lengo la kukiimarisha chama kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu wa 2024 na uchaguzi Mkuu wa Madiwani, Wabunge na Rais 2025 ili kukidhi matakwa ya katiba ya Chama hicho ya kushinda chaguzi zote,kuunda dola na kuunda Serikali.

Alisema mbali na hilo pia katika ziara hiyo ameitumia kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia majawabu yalikosekana kwa muda mrefu ambapo alitoa maelekezo mbalimbali kwa watumishi wa umma katika idara zilizolalamikiwa namna ya kumaliza kero za wananchi hao.

Makonda amekuwa na utaratibu wa kuwasimamisha watumishi wa Serikali toka idara zote mbele ya Mikutano yake ya hadhara moja wajibu maswali ya wananchi lakini pia wananchi wajionea wenyewe wanao wasababishia waichukie Serikali yao kwa kushindwa kuwahudumia.

Awali akizungumza wakati wa mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa Tanga Rajabu Abdurahman alimshukuru Rais Dkt Samia Suluhu kwa kutoa fedha nyingi mkoani Tanga kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Rajabu alitumia fursa hiyo kumuomba Makonda miradi yote inayotekelezwa mkoani humo iwanufaishe wazawa ili kuondoa malalamiko ya wananchi kutokupata hizo za ajira na kushindwa kunufaika na miradi hiyo inayotekelezwa katika maeneo yao.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Tanga Waziri Kindamba akizungumza wakati akitoa salamu za mkoa alisema mkoa uko salama na Serikali ina mahusiano mazuri na Chama na Wazee jambo ambalo limeufanya Mkoa huu kiendelea kuwa shwari na kutokuwa na matukio ya Uvunjifu wa amani.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger