Mshauri wa matibabu wa GGML Michael Mgonea (kulia) akionyesha jinsi ya kufanya ufufuaji wa moyo na mishipa katika maonyesho ya nne ya teknolojia ya madini yanayoendelea kwenye uwanja wa EPZA katika mji wa Geita.
Na Mwandishi wetu
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameipongeza Kampuni ya Uchimbaji Dhahabu Geita (GGML) kwa kutoa ajira zaidi ya 5000 kwa Watanzania huku asilimia zaidi ya 83 ya uongozi wa kampuni hiyo wakiwa ni Watanzania.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana tarehe 22 Septemba 2021 mkoani Geita wakati akizindua maonesho maonesho ya nne ya teknolojia za uchimbaji madini mkoani Geita.
Amesema licha ya GGML kushirikiana na Serikali na kutoa ajira za kutosha kwa Watanzania wengi, bado kumekuwapo na baadhi ya Watanzania ambao sio waamini jambo ambalo linatakiwa kushughulikiwa.
Kutokana na hali hiyo, amewaagiza maofisa madini mkoani humo, kushughulikia wafanyakazi wote ambao si waadilifu.
Aidha, ametoa wito kwa Watanzania kuchangamkia fursa katika maeneo ambayo madini mbalimbali yanagundulika ili kujikwamua kiuchumi.
Alisema Tanzania ni nchi yenye madini mengi mbali na dhahabu ambayo inachimbwa maeneo mengi.
“Huko Ulanga- Morogoro tumegundua graphite zaidi ya tani milioni 152 inatarajiwa kwa miaka 35, Kyerwa- Kagera tuna madini ya bati (Tin) ya kutosha zaidi ya tani bilioni nne zitachimbwa zaidi ya miaka 70 . Madini hayo ya bati yamepanda thamani kubwa baada ya wizara kusimamia, kg 1 ilikuwa inauzwa 6000, sasa ni 34,000 kwa kilo.
“Nimewaambia wanakerwa, Bukoba wajipange… pesa ipo Tanzania bado ni tajiri. Nitoe rai kwa vijana kuchangamkia fursa zilizopo katika maeneo yenye miradi ya madini,” alisema.
Aidha, akizungumza katika maonesho hayo, Makamu wa Rais wa GGML, Simon Shayo alisema mbali na ulipaji wa mapato ya Serikali na uwekezaji kwenye jamii, Kampuni hiyo imetoa ajira kwa Watanzania zaidi ya 5,000 ikiwa ni pamoja na wale wanaofanya kazi chini ya wakandarasi wetu.
Alisema hadi kufikia sasa takriban asilimia 98 ya wafanyakazi wa GGML na asilimia 83 ya menejimenti ni Watanzania.
"Tunafurahi pia kuona kuwa uwepo wetu mkoani Geita na Tanzania kwa ujumla umekuwa na tija kubwa kwa maendeleo.
“Lengo letu ni kuendelea kuwa mdau mwaminifu wa maendeleo kwa Tanzania na watu wake kwa miaka yote ambayo tutakuwa hapa, ikiwa ni pamoja na kuwa sehemu ya mustakabali wa kujenga uchumi wa viwanda na kufikia dira ya 2025 ambapo sekta ya madini imelengwa kuchangia walao 10% ya pato ghafi la taifa,” alisema
Hata hivyo, alisema kampuni hiyo imedhamini maonesho hayo mfululizo kwa muda wa miaka minne tangu yaanzishwe kwa kuwa yamekuwa na tija kubwa kwa Watanzania.
“Tunafurahi pia kuona eneo hili tulipo, tumeshirikiana na Halmashauri ya Geita Mji kuwekeza kiasi cha Shilingi Milioni 800 katika kuendeleza eneo hili la viwanja vya Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji na Mauzo Nje ya Nchi (EPZA) lenye ekari zaidi ya 200 ambalo litakuwa kitovu cha uwekezaji na biashara Mkoani Geita,” alisema.
Shayo alisema GGML inafarijika kutokana na ushirikiano wa kutosha wanaoupata kutoka Serikalini katika kutekeleza kwa vitendo sheria mpya ya madini ambayo imewapa mwongozo mzuri wa ulipaji kodi, mrabaha na matumizi mazuri ya fedha za wajibu wa kampuni kwa jamii sanjari.
“Pia naipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluh Hassan kwa namna ambavyo inaendelea kukuza mazingira ya uwekezaji nchini.
“Ndani ya muda mfupi tumeshuhudia dhamira yake ya dhati ya kukutana na sekta binafsi pamoja na wadau wa sekta ya madini ili kuangalia changamoto zinazokabili sekta zao na kwa kweli tunafurahi kuona mwanga mzuri zaidi katika sekta ya madini nchini Tanzania,” alisema.
Alisema kwa kipindi cha miaka minne mfululizo GGML imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo kwani kwa kushirikiana na Serikali mkoani Geita imetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kupitia fedha za wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR) zenye gharama zaidi ya Shilingi bilioni 40.
0 comments:
Post a Comment