Friday 22 January 2021

Breaking : APIGWA NA WALINZI WA HOSPITALI YA RUFAA MKOA WA SHINYANGA AKIHUDUMIA MAMA YAKE WODINI

...
Mlinzi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga ambaye hajajulikana mara moja jina lake akimshambulia Daudi Lefi leo jioni ambapo video ya tukio hilo imesambaa mtandaoni 
Mlinzi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga akimshambulia Daudi Lefi
Mlinzi wa hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Shinyanga akiamua ugomvi uliotokea mlinzi mwenzake akiendelea kumshambulia Daudi Lefi.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Katika hali isiyotarajiwa mwanaume aliyejulikana kwa jina la Daudi Lefi (40) amejikuta katika wakati mgumu baada ya kushambuliwa na Walinzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga wanaodaiwa kumtaka aondoke wodini kwamba muda wa kusalimia wagonjwa umeisha. 

Tukio hilo lililozua gumzo la limetokea leo Ijumaa Januari 22,2020 majira ya saa 11 na dakika 45 jioni wakati kijana hiyo akiwa aktika wodi ya wanawake namba 1 ambako mama yake mzazi Victoria Lugano Mwakagari aliyelazwa hospitalini hapo jana. 

Akisimulia kuhusu tukio hilo, ndugu wa kijana huyo Lydia Lefi amesema kuwa kaka yake amekutwa na mkasa huo wakati akiwa katika harakati za kulipia dawa za mama yao ambaye amelazwa katika hospitali hiyo jana Januari 21,2021. 

“Kaka alikuwa alipie dawa, alipewa karatasi ya kwenda kulipia dawa, alipoenda kufuata Control number ili alipie, jina likawa halionekani , ikabidi aende wodini kwa mgonjwa kuangalia amesajiliwa kwa jina gani,akiwa wodini hao walinzi ndipo walipoingia wodini na kumtaka aondoke kwamba muda umekwisha. 

"Walivyomtaka aondoke wodini akawaambia amekuja kuangalia jina gani mgonjwa ameandikishwa, wale walinzi wakamwambia aondoke muda huo huo, akawaomba lakini wakamwambia huwezi kutupangia kazi. Kaka akasema nitaondokaje mama hajapata huduma ,wale walinzi wakaanza kumsukuma ndipo mlinzi mmoja akachomoa mkanda wa suruali na kuanza kumshambulia huku mwingine akimsukuma, baadae akaja mlinzi wa kike akasogea na kuwaachanisha”,ameeleza Lydia.

Daudi Lefi amesema walinzi hao hao walidhani amefika muda huo huo hospitalini wakati yeye alikuwa  amefika hospitalini hapo muda mrefu lakini Computer za Hospitali zikawa hazisomi jina la mgonjwa wake wakati anataka kununua dawa.

"Sikurusha ngumi kwa sababu ni eneo la hospitali wangesema nimeenda kufanya vurugu. walionishambulia walikuwa wawili lakini mmoja ndiyo aliyeanza kwa kunichapa na mkanda", amesema Daudi.

"Wamenifuata na mkubwa wao na kuniomba tuyamalize kwamba kijana wao amekosea nami nimeamua kuwasamehe. Katika hali ya ubinadamu nimeamua kumsamehe kijana huyo baada ya kuomba radhi",ameongeza. 

 Baadhi ya wagonjwa na watu wanaouguza wagonjwa wameeleza kusikitishwa na kitendo cha mlinzi kumpiga ngumi na mkanda na kuongeza kuwa baadhi ya walinzi katika hospitali hiyo wana lugha mbaya na wanatumia ubabe hawaangalii utu.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga, Luzila John Boshi amekiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa atatoa taarifa baadae na kwamba yupo kwenye kikao.

Tutawaletea taarifa zaidi hivi punde
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger