Wednesday 20 January 2021

ALIYETENGENEZA KEKI ZENYE MAUMBO YA SEHEMU ZA SIRI AKAMATWA

...

Mwanamke mmoja nchini Misri ameshikiliwa na polisi kwa muda baada ya kushutumiwa kutengeneza keki zenye maumbo ''yasiyo na heshima'' vyombo vya habari nchini humo vimeeleza.

Keki hizo zilizotengenezwa na peremende laini zilizobuniwa maumbo ya sehemu za siri na maumbo ya nguo za ndani, zililiwa katika sherehe ya kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa katika klabu ya michezo ya Cairo.

Baada ya picha kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, mtengenezaji wa keki alikamatwa kisha kuachiwa kwa dhamana ya dola 319 za Marekani. Alikana kuoka keki zenye maumbo yanayochochea ngono.

Chombo cha juu cha kidini kimetahadharisha kuwa bidhaa zinazotengenezwa kwa mtindo huo zinapigwa marufuku katika uislamu.

Dar al-Ifta kiliandika katika mtandao wa Facebook kuwa bidhaa zinazowakilisha masuala ya ngono '' ni ukiukaji wa maadili na udhalilishaji katika jamii''.

Wanawake kadhaa walioshiriki kwenye sherehe hiyo pia wanaripotiwa kuchunguzwa, huku Wizara ya vijana na michezo ikitazama namna klabu hiyo ilikofanyika sherehe ilivyohusika.

Wakili wa haki za binadamu Negad El Borai aliandika katika ukurasa wa twitter kwamba tukio hilo lilithibitisha "kuna sehemu ya jamii, kwa msaada wa serikali, ambayo inataka kuondoa nafasi yoyote ya uhuru wa watu nchini Misri kwa kisingizio cha kulinda maadili ya familia ''.

Alifananisha na kesi za wanawake kadhaa vijana wa Misri wanaotuhumiwa kwa makosa yanayohusiana na maadili kuhusiana na video zilizochapishwa kwenye TikTok na majukwaa mengine ya mitandao ya kijamii

Jumanne iliyopita, mahakama ya rufaa ilifuta hukumu ya miaka miwili ya gerezani iliyotolewa kwa washawishi wawili - Haneen Hossam, 20, na Mawada al-Adham, 22 - ambao walitiwa hatiani mnamo mwezi Julai mwaka jana kwa "kuvunja maadili na kanuni za kifamilia" na kuchapisha picha "zisizo za adabu" na video.

Lakini siku chache baadaye iliibuka kwamba mwendesha mashtaka wa umma alikuwa ameamuru kuendelea kwa kizuizini kwa wanawake kusubiri uchunguzi juu ya mashtaka ya usafirishaji wa binadamu.

Mwendesha mashtaka alidai kwamba walikuwa wamewashawishi wasichana kwa kuwahimiza watume video zinazofanana na zao.

Wakili wa wanawake hao alisema watakata rufaa dhidi ya hatua hiyo.

CHANZO- BBC SWAHILI
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger