Sunday 5 July 2020

Waziri Mkuu: Tuongezee Bidii Ili Tufikie Uchumi Wa Juu

...
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka Watazania waendelee kufanya kazi kwa bidii ili nchi iendelee kukua kiuchumi na kufikia uchumi wa juu kwa kuwa tayari imekuwa ya uchumi wa kati.

“Kama ni mkulima lima kwa bidii, mtumishi wa umma fanya kazi kwa bidii, mlio viwandani fanyeni kazi na mamalishe nanyi pikeni sana ili mzunguko wa fedha uweze kuendelea kuwa mkubwa nchini.”

Alitoa kauli hiyo jana (Jumamosi, Julai 04, 2020) alipozindua jengo la ofisi na biashara la Mpanda Plaza lililojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Mpanda kwa gharama ya sh bilioni  2.8.

Waziri Mkuu alisema Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani pato la mwananchi kwa mwaka lilikuwa dogo na baada ya miaka mitano limeongezeka na kufikia sh, milioni mbili.

Alisema ongezeko hilo la pato la mwananchi kwa mwaka limeliwezesha Taifa kuingia katika uchumi wa kati kabla ya matarajio yaliyopendekezwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo.

Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Tanzania ililenga kuifikisha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda ifikapo mwaka 2025 lakini nchi imewezeka kufikia uchumi wa kati 2020.

Baada ya kuzindua jengo hilo, Waziri Mkuu alitembelea kijiji cha Kasekese kilichoko wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi ambapo alizindua msimu wa ununuzi wa zao la pamba kwa mwaka huu.

Waziri Mkuu alisema lengo la Serikali ni kurudisha ushirika  ili uweze kuwa na tija kwa wakulima, aliwataka viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) wawasaidie wanachama wao.

Vilevile, Waziri Mkuu aliwaagiza Maafisa Kilimo nchini wawaelimishe viongozi wa vyama vya ushirika namna bora ya uendeshaji wa vyama hivyo ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Aliwahakikishia wananchi hao kwamba Serikali itaendelea kuwasaidia kwa kuhakikisha Maafisa Ugani wanawafikia katika maeneo yao na kuwapa elimu itakayowawezesha kujiongezea tija.

Mwisho.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger